Na William Kapawaga, Lindi
MKUU mpya wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai amewaomba watumishi kufanyakazi kwa ushirikiano ili kujenga mshikamano.
Ngubiagai ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Tellac, Makao Makuu ya Mkoa.
Alisema, ili kazi yake ya ukuu wa Wilaya iwe nzuri, anapaswa kupewa ushirikiano na watumishi wa ngazi zote ndani ya Wilaya hiyo.
Ngubiagai alisema, nafasi hiyo Mamlaka ya kumsaidia Rais ndani ya Wilaya kwa kufahamu na kutatua matatizo ya wananchi wa wilaya hiyo, hivyo watumishi wa ngazi zote wanatakiwa kuwa kitu kimoja.
“Nashukuru narudi Kilwa kwa mara nyingine, hivyo naomba ushirikiano kama ilivyokuwa zamani kabla ya kupangiwa majukumu mengine na tukishirikiana kwa pamoja kila kitu kitawezekana,” alisema Ngubiagai.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliungana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Zainabu Kawawa kwa kuwataka wazazi wa wanafunzi waliochaguliwa kwenda kidato cha kwanza kuhakikisha wanakwenda shule na kuwataka wazazi kutoficha au kuwaozesha watoto wote wenye umri wa kwenda shule.