Na Mwandishi Wetu
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa amewahakikishia wananchi wa Mkoa Kagera kuwa, Miradi yote mikubwa ya kimkakati itaendelea kutekelezwa na hakuna mradi utakaosimama ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Bashungwa ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alisema hayo Disemba 20, 2022 katika hafla ya mapokezi yake wakati alipowasili Mkoani Kagera ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipochanguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kauli mbiu ya Kazi iendelee amehakikisha Miradi yote mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano inaenendelea kutekelezwa na hakuna mradi uliosimama,” alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kupeleka fedha nyingi za maendeleo kote nchini kuanzia ngazi ya kijiji mpaka miradi ya Kitaifa kama Ujenzi wa reli ya SGR na bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo yote inaendelea kutekelezwa.
“Nawaomba wananchi wote na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi tuendelee kumuunga mkono Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumwaga fedha za maendeleo kote nchini na ana maono makubwa ya kufikisha nchi yetu mahala pazuri,”
Aidha, Bashungwa amewakumbusha Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuisimamia Serikali katika ngazi zote na kupaza sauti pale wanapoona watu wachache wanakwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kupita miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Vile vile, amewataka Watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa wananchi na kufanya kazi kwa bidii kwa kutimiza wajibu wao na kuondokana na hali ya kujisahau, hivyo Chama Cha Mapinduzi kupitia Serikali hakitasita kumchukulia hatua Mtumishi yoyote atakayeenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Pia, Bashungwa ametumia fursa hiyo kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa katika wilaya Karagwe ikiwa ni pamoja na Mradi mkubwa wa Maji wa Rwakajunju, Ujenzi wa Barabara ya Nyakahanga mpaka benaco na miradi mingine mikubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya Karagwe.
Nae, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoa Mkoa Kagera, Karim Amri ametoa wito kwa Wanachama kutumia fursa ya uwepo wa WANEC Wawili mkoa Kagera kuwasilisha kero zilizopo mkoa Kagera ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.