Na Jumbe Abdallah
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeitaka Serikali kuhakikisha inasimama kwa makini ili kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinafuatwa katika Ujenzi ili kuepuka ajali hususani za maghorofa.
Kauli hiyo ya CUF imekuja siku chache kufuatia vifo vya watu wasiopungua watano na majeruhi wasiopungua tisa walioporomokewa na jengo la ghorofa mbili lililokuwa likijengwa katika Kijiji cha Sembeti, Kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma Eng. Mohamed Ngulangwa, pamoja na kwamba Serikali imeahidi kuunda Tume kuchunguza chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo, CUF kimetoa lawama kwa Serikali na vyombo vyake kwa kushindwa kusimamia Sheria na miongozo mbalimbali inayoelekeza kwenye Ujenzi Salama.
Taarifa hiyo ilisema kwamba, mwaka 1997 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria kadhaa zilizochangia Kuundwa kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi ( Contractors Registration Board -CRB), na Bodi ya Usajili wa Wahandisi ( Engineers Registration Board- ERB) na Bodi ya Usajili wa Wasanifu na Wakadiriaji na Wathaminishaji ( Architects and Quantity Surveyors Registration Board-AQRB).
“Pamoja na Fedha nyingi kutumika katika kuendesha mijadala Bungeni kupitisha Sheria hizi, na gharama kubwa iliyotumika katika kuanzisha Bodi hizi, usimamizi wa Utekelezaji wa Misingi ya Ujenzi Salama umekuwa ni wa kiwango cha chini sana,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ya Eng. Mohamed Ngulangwa iliendelea kusema kuwa, pamoja na Serikali kuwa na Wahandisi wa wilaya na mikoa, uzoefu unaonesha kwamba ni kwa kiwango cha chini sana “tujiulize wahandisi hawa wanafuatilia miradi inayoendelea katika maeneo yao ili kujiridhisha kwamba Masuala ya Kitaalamu yanayohusu Ujenzi Salama hayachezewi?”
Iliendelea kusema, “ukirejea maelezo ya Mhandisi wa Ujenzi Ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro Lameck Bernard utabaini uzembe unaofanywa na Ofisi yake katika kuhakikisha Taratibu za Kitaalam na za Kisheria zinafuatwa kwa miradi ya Ujenzi inayofanyika mkoani humo.”
“Bwana Lameck ameweka bayana kwamba jengo hilo limejengwa mfululizo na halikupata muda wa kupumua (‘Curing’ haikufanyika kwa kuzingatia Muda wa Kitaalam). Je, ni nani aliyepaswa kukagua miradi ya Ujenzi katika mkoa wake ili kujiridhisha kwamba taratibu zinafuatwa?”
Katika kukabiliana na hali hiyo, “CUF kinatoa wito kwa Serikali kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinafuatwa katika Ujenzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Wakandarasi waliosajiliwa na wenye sifa tu ndio wanaojenga na pale ambapo Sheria zinataka awepo Mhandisi Mtaalam (Professional Engineer) kusimamia mradi, hilo lisimamiwe ipasavyo,”
Mbali na hayo, CUF kimetoa pole kwa wote walioathirika na tukio hilo ikiwa ni pamoja na waliopoteza ndugu na jamaa zao, waliojeruhiwa na hata kupoteza mali. “Tunawatakia marehemu wote mapumziko mema na tunawaombea majeruhi wapone haraka.”