Mchengerwa atoa agizo kwa viongozi Serikali za mitaa

0

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amewaagiza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari unafanyika bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile.

Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Januari 6, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi vyumba 18 vya madarasa vilivyogharimu Shilingi Milioni 300 katika Halmashauri ya Wiaya ya Bahi ambapo pia ametoa tuzo kwa waandishi 15 wa habari za Mradi wa Shule Bora.

“Nawaagiza mkasimamie kwa dhati zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wote bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile wenye umri lengwa kwa ajili ya kuanza darasa la awali, msingi na MEMKWA” alisisitiza.

Mchengerwa amewataka Viongozi hao kutoa takwimu sahihi za uandikishaji na jinsi wanavyoripoti wanafunzi katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Kila siku ya Ijumaa katika wiki).

Vilevile, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, kuhakikisha inatunza miundombinu ya vyumba vya madarasa yaliyokabidhiwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Elimu ambayo yameleta matokeo makubwa ikiwemo kuongeza ufaulu Dodoma kwa shule za msingi na sekondari na kupunguza utoro kutoka wanafunzi 24,000 hadi 6,000 (2024).

Akitoa taarifa kuhusu umalizaji wa ujenzi wa madarasa hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi, Zaina Mlawa alisema ujenzi wa madarasa 10 umefanyika kwa kufuata mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ambao unalengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here