Mambo muhimu kuhusu Wakala wa Vipimo(WMA)

0

USIMAMIZI wa matumizi ya vipimo (measurements) ulikuwepo hapa nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka hamsini (50), kama Idara ya Serikali ikiwa na lengo la kukidhi matakwa ya Serikali na jamii kwa upande wa usimamizi wa kumlinda mlaji dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya Vipimo (consumer protection through ensuring that measuring systems result in fair tradetransactions)

Historia ya Vipimo ilianza kabla ya Uhuru, wakati wa utawala waWajerumani na Waingereza, Matumizi ya metriki (Metric System) yalianzishwa na Wajerumani wakati wa utawala wao kabla ya vita kuu ya dunia, mwaka 1914 – 1918. Waingereza nao walipokuja kututawala, baada ya vita hivyo, walianzisha mfumo wao wa matumizi ya vipimo vya impreriao ( Imperial System of Measurements) uliotumika samba,ba na vipimo vya metriki.

Kazi ilifanywa kwa mujibu wa Sheria ya wakati huo iliyokuwa ikijulikana kama Weights and Measures Ordinance, Chapter 221 ya mwaka 1931 pamoja na kanuni zake. Utendaji kazi ulikuwa ukifanywa na wakaguzi wa vipimo (Inspectors of Weights and Measures ) waliokuwa chini ya usimamizi Superintendant wa polisi.

Mwaka 1960 Sheria hiyo ya vipimo ilifutwa na kuanza kutumiwa Sheria mpya, Weights and Measures Ordinance, Chapter 426 ya mwaka 1960. Sheria hii iliweka idara ya vipimo chini ya Wizara iliyokuwa inahusika na masuala ya biashara ambayo ilikuwa Wizara ya Biashara na Viwanda. Mwaka 1964, Idara ya Vipimo ilikuwa chini ya Wizara ya Biashara na Ushirika hadi mwaka 1967 iliporudi tena kuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya uongozi wa Kamishna wa Vipimo.

Mwaka 1968, Tanzania pamoja na nchi zingine za Afrika Mashariki (Kenya na Uganda) zilianza kutumia mfumo mmoja wa vipimo wa metriki (Metric System). Mwaka 1969, Tanzania ilifungua ofisi za vipimo katika zoni 3 (Mwanza, Tanga na Mbeya) ambako huduma za vipimo zilianza kutolewa. Ilipofika mwaka 1977/78 ofisi za vipimo ziliweza kufunguliwa katika kila mkoa Tanzania Bara.

Sheria ya Weights and Measures Ordinance, Chapter 426 ya mwaka 1960, nayo ilifutwa mwaka 1982 na Sheria mpya, Weights and Measures Act No. 20 ya mwaka 1982, kuanza kutumika. Mfumo wa matumizi ya International System of Measurements nao ulianza kutumika. Jina la ofisi nalo lilibadilishwa na kujulikana kama Weights and Measures Bureau (WMB).

Kuanzia mwaka 1984, Weights and Measures Bureau ilikuwa kitengo chini ya Kurugenzi ya Biashara chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara hadi ilipobadilishwa na kuwa Wakala wa Vipimo kuanzia mwaka 2002. Kwa kipindi chote hiki (WMB) imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa mijibu wa Sheria ya Vipimo Na. 20, iliyopitishwa na Bunge mwaka 1982 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Mei, 1983 kwa Tangazo la Serikali Na. 59 la mwaka 1983.

Kufuatia mpango kabambe wa Serikali wa kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi za Umma na kupunguza baadhi ya majukumu kwa Serikali Kuu, WMB ilikuwa ni ni moja ya taasisi za Serikali zilizoingizwa katika mpango huo. kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 WMB ilibadilishwa na kuwa Wakala wa Vipimo (WMA) kuanzia tarehe 13 Mei, 2002 kwa Tangazo la Serikali (Order no.) namba 194 la tarehe 17 Mei, 2002.

Kuanzia hapo WMA imekuwa ikiongozwa na Kamishna wa Vipimo ambaye pia ndiye Afisa Mtendaji Mkuu. Vipimo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo na. 340 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 na Sheria ya Wakala za Serikali Sura na 245 kama ilivyorekebishwa mwaka 2009.

Wakala wa Vipimo ina majukumu yafuatayo:-

📌 Kumlinda mlaji katika Sekta ya Biashara, Usalama, Mazingira na Afya kupitia matumizi ya vipimo sahihi.

📌 Kuilinda jamii kuepukana na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya vipimo katika Sekta ya Biashara, Usalama, Mazingira na Afya.

📌 Kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wanaojihusisha na utengenezaji, uundaji, na uingizaji wa vipimo mbalimbali katika Biashara, Usalama, Mazingira na Afya.

📌 Kuwa kiungo kati ya Taifa letu na taasisi za kikanda na Kimataifa katika masuala ya Vipimo (Legal Metrology).

📌 Kuhakikisha vifaa vyote vitumikavyo nchini kama standards za vipimo vinaulinganisho sahihi na ule wa Kimataifa.

📌 Kukagua na kuhakiki bidhaa zilizofungashwa (Net quantity & labeling).

📌 Kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya vipimo kwa wadau

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here