Maisha ya nchi ya Togo yana mengi ya kujifunza

0

Na Yahya Msangi

TOGO ni moja ya nchi nne za Afrika zilizokuwa chini ya ukoloni wa Mjerumani. Nchi hii ilipata Uhuru wake Aprili 27, 1960, ni mwaka mmoja kabla ya Tanganyika. Togo wana mwenge wa Uhuru kama Tanzania. Mwenge huo huwashwa siku moja kabla ya siku ya Uhuru; Saa 12 kamili jioni na Rais wa nchi hiyo ili umulike maadui walikojificha gizani.

Huwashwa nje ya ukumbi mkuu wa mikutano (Parlais de Congres) ambako ndiko iliposimikwa nembo ya mapambano ya kupigania Uhuru. Nembo hiyo inaonyesha mwanaume aliyepinda kichwa na kutunisha misuli.

Ndani kuna picha ya mwanamke aliyebeba chungu kuonyesha kwamba, mwanamke alisaidia sana mapambano ya Uhuru kwa kutayarisha chakula. Mwenge upo ndani ya chungu hicho kuonyesha kuwa, mwanamke ndiye aliyemwangazia mwanaume na kumpa nguvu wakati wa kupigania Uhuru.

Ni sherehe kubwa ambayo Wananchi wa Togo wote bila kujadili tofauti ya vyama vyao vya siasa, Itikadi za Kidini, hali zao za kiuchumi, makabila yao huienzi mno. Wananchi hao kwa maelfu wanajaa kushuhudia mwenge ukiwashwa.

Ni tofauti kabisa na Tanzania ambapo wapo baadhi ya watu wachache wanataka mwenge usiwashwe tena na kukimbizwa nchi nzima, badala yake uwekwe kwenye makumbusho ya Taifa! Huu ni ujinga uliokithiri.

Mwenge haupimwi kwa fedha! Una thamani kuliko fedha kwa wanaojitambua. Wagiriki wanao mwenge na wamefanikiwa kuufanya uheshimiwe na Mataifa yote; Mwenge wa Olimpiki ambao unakimbizwa duniani kote! Kwa hiyo, Togo na Tanzania tunafanana kwa hili la mwenge na utawala wa Mjerumani.

Kuna majengo ya Mjerumani na treni kama Tanzania. Mpaka leo najiuliza ilikuwaje watu wenye majina ya ukoo wa Moshi ni miongoni mwa mashujaa wa Togo walioenziwa? Makaburi ya mashujaa hawa yapo sehemu inayoitwa WAHALA. Yapo majina mawili yenye ukoo wa Moshi!

Lakini, Togo iliwahi kuwa na sikukuu mbili za Uhuru! Nadhani ndio nchi pekee iliwahi kuwa na sikukuu mbili za Uhuru ndani ya mwaka mmoja! Wakati ilipata uhuru 1960 Rais alikuwa Olympio (rafiki wa Nyerere na Nkurumah). Muelekeo huu haukuwapendeza Wafaransa.

Mwaka 1963 rais huyo aliuawa akiwa Ikulu. Ndipo utawala ukaangukia mikononi mwa Grand Generale Eyadema. Huyu akitangaza siku aliyoingia madarakani kuwa ndio siku ya Uhuru! Ikawa wafuasi wa Olyimpio wanaendelea kuadhimisha Aprili 27 na wa Jenerali siku mpya!

Ila Aprili 27 ikawa sio sikukuu rasmi tena. Wahusika wakiidhimisha kimyakimya! Mzee Eyadema alipofariki 1985 mwanaye ambaye ndiye rais wa sasa akairejesha Aprili 27 kuwa rasmi, na ile ya Baba yake imekuwa ya kifamilia na mara nyingi huenda Kanisani kufanya misa maalum.

Ukiwa umepandikizwa fikra za Kimagharibi unaweza kudhani Eyadema alikuwa ni mtu mbaya mno asiye na mazuri. Kwa kuwa tu alikaa miaka karibu 40 Ikulu. Ukweli ni kwamba, ana mazuri mengi mno. Nikumegee machache; Mosi, japo asili ni mkristo wa Kanisa la RC alijitahidi kuwaunganisha Waislamu wa Togo.

Ndio maana Togo husikii Waislamu wakigombana au kushambulia wasio wa imani yao. Eyadema aliwachukua viongozi wa madhehebu mbalimbali waliokuwa wakigombana hovyo na kuwapa ndege kwenda Saudia! Akamuamuru Waziri wa masuala ya jamii aandamane nao hadi Jeddah na Mecca. Akalipia gharama zote.

Kule Jeddah ‘wakapigwa’ shule na maulamaa. Waliporudi Togo wakavunja makundi yao na kuunda umoja ambao umedumu hadi leo. Kila ukiwasikiliza mashehe hapa Togo wanamsifu na kumuomba sana Eyadema. Ingekuwa rahisi mno Al Shaabab, Touraq na Boko kuwa na matawi Togo. Lakini, imeshindikana. Yarabi salama! Eyadema alikuwa anahudhuria sherehe ya Eid na anagawa futari kwa masikini. Mungu amhifadhi!

Pili, Eyadema alikuwa mkarimu mno. Wengi wanaamini ilitokana na maisha yake. Alikuwa yatima angali mdogo mno. Akawa anaishi kwa watu mbalimbali. Lakini, akiteswa na kufukuzwa kutokana na utundu wake. Alikuwa ana misuli na mkorofi. Hatimaye akachukuliwa na Mmisionari kutoka Ufaransa aliyekuwa anaishi Togo na kumlea. Nako hakuacha ukorofi.

Mke wa huyo Mmisionari akamtesa mno mara alale na njaa, mara ampige! Wakati huo alikuwa kajifunza useremala. Mwisho Mmisionari huyo akaamua amwombee kazi jeshini. Ndipo akaenda jeshi la mkoloni enzi hizo. Kutokana na juhudi na mabavu akapanda vyeo haraka.

Eyadema alipokuwa rais akawa ni mwenye huruma sana kwa wenye shida. Alikuwa akigawa chakula kwa masikini hasa kule kijijini mwake. Na alikuwa mtu yeyote akimlilia shida hamwachi aondoke patupu.

Kuna familia nyingi mno alizisaidia hadi kuwajengea nyumba. Mtu anaweza kudai alifanya hivyo kwa fedha ambazo hazikutoka mfukoni mwake, lakini wangapi wana fedha isiyo yao na hawasaidii masikini? Au wanatumia kwa mambo ya hovyo wao na familia zao?

Tatu, asilimia 53 ya Watogo ni wenye dini ya asili. Eyadema aliwatambua. Nchi nyingine wanaitwa wachawi, makafiri, mashetani, waovu! Lakini, watu hawa husikii wakiua wenzao, wakitukana Imani za wenzao, wakitenga wasio na imani yao.

Hapa Togo wametoa michango mkubwa kuzuia maovu kama kutesa watoto, kupiga wake, kutesa wanyama, kuharibu mazingira, kuzuia wizi na vibaka, ubakaji, n.k. Sasa hao wanaowaita majina ya hivyo, ndio wanaua wenzao nyumba za ibada, wanatukanana, wanadanganya na kufufuana, wanaiba sadaka, wanachinja watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino), wanateka watoto na kuwauwa!

Kama inavyokuwa nchini kwetu, Togo wanapowasha mwenge wa Uhuru, kinachofuata ni hafla ya Kitaifa Ikulu na hatimaye wanamalizia kwa kushuhudia gwaride la Uhuru! Bendera ya Togo; Nyota nyeupe ya matumaini (Star of Hope) ndani ya damu iliyomwagika. Mistari mitano inawakilisha mikoa mitano ya Togo. Kijani ni mazingira na njano ni Mali asili. Hakika, yapo mambo tunapaswa kujifunza na kuiga kutoka nchini Togo.

Jambo kubwa zaidi, ni suala la migogoro ya kidini ambayo imekuwa ikijitokeza, ingawa kwa siku za karibuni imepungua, lakini bado chinichini wapo wanaobaguana kwa sababu ya dini zao. Kwa upande mwingine kwenye suala la kuadhimisha siku ya Uhuru, Watanzania wanapaswa kuwa kitu kimoja, tunahushuhudia baadhi ya wanasiasa wakichochea wafuasi wao kususia sherehe hizo na wao wamekuwa wakigoma kwenda kwenye viwanja vya maadhimisho au hafla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here