Na Dkt. Raymond Mgeni
AFYA ya akili ni ajenda muhimu zinazopaswa kuwa ni ajenda za Kitaifa kutokana na umuhimu wake kwa sasa. Uwakili ni eneo muhimu la 11 katika sera ya afya ya akili na huku lengo ni kutoa uelewa kuhusu masuala yahusuyo afya ya akili na kujenga ubora wa idadi ya watu duniani kuwa na afya ya akili imara.
Uwakili wa awali huanzia na familia ambazo zinakumbana na watu waliopata changamoto ya magonjwa ya akili. Uwakili huhusisha kutoa na kuhamasisha upatikanaji haki na kupunguza kiwango cha unyanyapaa na kutengwa kwa watu wanaopata maradhi ya akili.
Uwakili husaidia kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu masuala mengi kuhusu afya ya akili. Uwakili husaidia katika kuchochea mabadiliko katika sera na utoaji wa huduma za afya ya akili nchini. Uwakili hupandisha uelewa wa jamii, utoaji wa taarifa sahihi, elimu na mafunzo pamoja na ushauri.
Sehemu nyingi duniani unapogusia afya ya akili na magonjwa ya akili sio eneo lilopewa kipaumbele kikubwa kama ilivyo afya ya mwili. Kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani, magonjwa ya akili ni kundi la magonjwa yaliyoachwa na kutopewa uzito mkubwa.
Hivyo, uwakili unahitajika kwani bado huduma za afya ya akili haziko katika kiwango cha kuridhisha, huduma ambazo sio bora kwa kiwango kinachotakiwa katika hospitali za kawaida na hata vituo vya awali vya huduma za afya ya akili.
Aidha, bado ushiriki wa jamii kuhusu afya ya akili ni mdogo, uwepo wa ukiukwaji wa haki za msingi za watu wanaopata magonjwa ya akili, unyanyapaa, ukosekanaji wa elimu katika shule, sehemu za kazi kuhusu afya ya akili.
Uwakili unawekwa katika makundi makubwa mawili; Mosi ni, Uwakili wa afya ya akili (Mental Health Advocacy) unaotoa nafasi ya elimu ili mtu mmoja mmoja, familia, vikundi na jamii kwa ujumla kujilinda dhidi ya vichochezi au mazingira yoyote yanaweza kupelekea afya ya akili kuathiriwa.
Pili, ni Uwakili juu ya magonjwa ya akili (Advocacy around mental disorders) kunakogusia nafasi ya uelewa kuhusu dalili za ugonjwa wa akili na kuwa tayari kutafuta huduma au msaada wa hatua za matibabu.
Uwakili unaweza kuwa na matokeo chanya yanayoweza kupelekea: Kuishawishi serikali kuona umuhimu wa huduma za afya akili na elimu ni ajenda za msingi na hili lipongezwe kwa serikali kuweka afya ya akili kipaumbele cha sita katika bajeti ya Wizara ya afya.
Tatu, ni kuboreshwa kwa sera na utekelezaji wa wadau wote wa afya ya akili, Nne, kuimarishwa kwa mifumo ya uwezeshaji wa utoaji na kukinga magonjwa ya akili.
Tano, utetezi wa haki za wagonjwa na familia zao bila kusahau jambo kuimarishwa kwa utoaji wa huduma za afya ya akili pamoja na matibabu kuanzia ngazi za huduma za msingi hadi hospitali za juu.
Uwakili unaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali kuanzia ngazi za Wizara ya Afya: Uwakili katika ngazi ya Wizara ya Afya kusaidia katika utoaji wa vitini vya elimu, vipeperushi na hata kuandaa vidio fupi fupi za kuelimisha umma.
Vile vile, uandaaji wa matukio yanayogusa utoaji elimu na taarifa kuhusu afya ya akili, uandaaji wa warsha mbalimbali na mikutano, uendelevu wa uaandaji wa midahalo ya kitaifa kuhusu afya ya akili (Mwaka jana Oktoba 10 ilifaa sana mdahalo wa kitaifa kuhusu afya ya akili). Uwakili wa ngazi kubwa ya Ki-wizara inasaidia katika mpango wa kisera na miongozo rafiki katika elimu na utoaji huduma.
Uwakili wa Kupitia Vyombo vya habari katika kushiriki na kuwa karibu na wataalamu juu ya wataalamu, wadau na vyombo vya habari kuzungumzia afya ya akili na magonjwa ya akili; kuandaa na kuzalisha habari nyingi kuhusu afya ya akili, huduma na uelewa wa magonjwa ya akili kwa jamii.
Lengo la uwakili wa kuzungumzia afya ya akili na magonjwa ya akili ni kuondoa taarifa zinazopotosha kuhusu afya ya akili na magonjwa ya akili.
Kwani wagonjwa wa akili wanatafsiriwa tofauti na jamii kwa kudhaniwa kuwa; hawana akili, sio salama kuwa nao, wakati wote hawawezi kujizuia, wameingiwa na roho chafu/mapepo, hawatabiriki, hawawezi kuoa na kulea watoto, hawawezi kufanya kazi au kila wakati wanahitaji kulazwa. Mtizamo huu umeongeza unyanyapaa mkubwa kwa wagonjwa na hata wagonjwa tarajiwa kuogopa kutafuta msaada.
Unyanyapaa unaathiri kwa ukubwa katika watu kupata huduma za afya ya akili kwa wakati, watu hawawi tayari kutafuta msaada kwa hofu ya kunyanyapaliwa au kutengwa, husababisha mtu kujikataa na kutojiamini, familia za wagonjwa kutengwa kijamii.
Uwakili unasaidia kupunguza unyanyapaa na kadri elimu kwa umma inapotolewa juu ya visababishi, dalili, matibabu, taarifa potofu na kiwango cha utokeaji wa visa vya magonjwa ya akili inapunguza hofu na taharuki kwa jamii.
Utoaji wa mafunzo kwa walimu na wahudumu wa afya ili kuongeza mabalozi wa kupinga unyanyapaa ni njia muhimu ya kutumia. Tatu ni utoaji wa elimu tiba kwa wagonjwa na familia na namna ya kuishi na mgonjwa mwenye ugonjwa wa akili na kuwezesha wagonjwa na familia katika huduma za utengamao
Mwisho vyombo vya habari vinapoendelea kutoa elimu kwa umma huchochea kubadilisha mitizamo hasi kuhusiana na magonjwa ya akili. Jukumu kubwa ni la kila mmoja kuwa balozi wa kutoa elimu kwa umma juu ya elimu ya afya ya akili pale tu mtu anapokuwa na taarifa sahihi ili kuwasilisha ujumbe utakaopunguza mitizamo hasi na taarifa nyingi potoshi kuhusu afya ya akili na magonjwa ya akili. Hakuna ustawi mzuri wa jamii ikiwa afya ya akili itadorora ya mtu mmoja mmoja.
*Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu wa Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya, Idara ya Afya ya Akili, anapatikana kwa Simu:+255 676 559 21, barua pepe: raymondpoet@yahoo.com.