Kuna umuhimu wa kuunda baraza la Vijana la Taifa?

0

𝖭𝖺 𝖲𝗍𝖺𝗇𝗅𝖾𝗒 𝖬𝖺𝗒𝗎𝗇𝗀𝖺

TAKRIBANI 80% ya watanzania ni vijana walio chini ya umri wa miaka 35. Bahati mbaya na kama ilivyo katika nchi zingine nyingi, nguvu kazi hii inakabiliana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya, ulevi wa kupindukia, magonjwa, msongo wa mawazo na hasa unaochangiwa na ukosefu wa ajira.

Kwa muda mrefu, vijana wamekuwa wahanga wa ajenda za kisiasa, mara nyingi wametumika kama mtaji kwa wanasiasa kwa ahadi za kutatuliwa shida zao baada ya uchaguzi na hatimaye kuachwa solemba baada ya wakubwa hao kuukwaa uheshimiwa. Imefika wakati Serikali ifanye mabadiliko makubwa na kuchukua hatua madhubuti kutatua shida za vijana ili na wao waishi kwa furaha na kufaidi matunda ya rasilimali za nchi yao.

Matatizo ya vijana ni mtambuka yanayohitaji utashi tu wa kiuongozi kuyatatua. Tayari vijana wana majukwaa kadhaa ya kuwasilisha, kujadili na kushauri juu ya changamoto zao ikiwa ni pamoja na Serikalini, vyama vya siasa; TYVA, YUNA, makanisani, misikitini n.k. Sioni umuhimu wa kujikita kuunda Baraza la Vijana la Taifa kwa sasa.

Wakati tukiwasihi vijana kutimiza wajibu wao wa kutunza amani, usalama na maadili mema, kwa upande mwingine Serikali siyo tu ijipange, bali ichukue hatua na maamuzi magumu kutatua changamoto za vijana hasa ajira kama ilivyofanya kwenye elimu na sekta zingine. Tukumbuke ni ngumu kwa mwenye njaa kuwa mtunza amani il-hali hana ajira ya kumpatia kipato cha kujikimu yeye na familia yake.

Pengine Serikali isifanye kama ilivyokuwa Libya ya Alhadji Muammar Gaddaf na nchi zingine ya kutoa ruzuku ya kujikimu kwa vijana wanaohitimu vyuoni kabla hawajapata ajira, lakini ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe kwa kuzingatia uchumi au bajeti yetu, mazingira na sera zetu ili tuepuke kuzalisha kizazi korofi, kisicho na tija na chenye kuleta fujo hapo baadaye.

Tulipoamua kuleta elimu ya msingi bure, kuongeza mikopo ya elimu ya juu na hivi karibuni kutoa bure mafunzo ya ufundi katika vyuo vya VETA, tulijipalia mkaa wa kuzalisha wahitimu wengi katika soko la ajira na hatuna budi kuwa na mikakati kabambe ya kuzalisha ajira mpya toshelezi.

Tukipuuza haya, ni dhahiri kuwa ni suala la muda tu kabla hatujakumbana na migogoro na hata kuzalisha wahamiaji haramu kama ilivyo kwa Ethiopia ambako ingawa wana matatizo mengine ya mipaka, ukabila, ardhi, sera na uongozi, lakini nao walianzisha elimu bure bila kujipanga kuwapokea wahitimu katika soko la ajira na sasa vijana wake wanakamatwa kila kukicha wakikimbilia nchi zingine kutafuta haueni ya maisha.

Kwa kuzingatia uwepo wa amani, rasilimali za kutosha, fursa, masoko, sera na mikakati ya sasa ya kushughulika na changamoto za vijana, naomba nishauri hatua kadhaa walau kwa uchache zinazoweza kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Kuanzishwa kwa sheria ya mfumo wa uanagenzi katika kuandaa vijana na maisha ya kazi yenye tija ndani au nje ya ajira rasmi. Ni matumaini yangu kuwa, mpango huu utahitaji au kuhimiza kampuni, mashirika na taasisi za umma na binafsi kumwezesha Mwanagenzi katika programu za ujifunzaji kwa vitendo.

Sheria za kazi zinapaswa kurekebishwa ili kutoa fursa kwa vijana kuajiriwa kwa muda ilhali wakilipwa mshahara na taasisi hizi ikiwa mafunzo yao yatachangia faida ya kibiashara. Mfumo huu umehakikisha kufanikiwa nchini Ujerumani, ambapo vijana wanapata fedha za kujikimu na uzoefu unaotakiwa kabla ya ajira za kudumu.

Serikali isiishie kudhamini masomo, bali iende mbali zaidi katika kuandaa utaratibu wa kuendelea kuwaamini vijana na kuwakopesha fedha za ubunifu na ufadhili wa biashara. Tunajua Serikali kupitia kila halmashauri inatenga 4% ya mapato yake kwa ajili ya vijana. Changamoto ni kwamba, fedha hizi hazitoshi.

Pia, upatikanaji wake umejaa urasimu na usiri na kiwango kinachotolewa ni kidogo kinachokidhi biashara na kazi ndogondogo kama uzalishaji wa tofali, saluni, mama lishe, genge, ufundi wa nguo (cherehani), utengenezaji na uuzaji wa sabuni za maji n.k. ambazo hazina athari kubwa katika kupunguza tatizo la ajira.

Kama tunahitaji kuendelea na mpango huu, hatuna budi kushughulikia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti na kubadili taratibu za upatikanaji wake ili kuwawezesha vijana wenye mawazo makubwa ya kazi ambazo zitaajiri wengi zaidi.

Nyuma yake kusiwepo na ajenda au harufu ya kuwateka vijana kwa mihemko na mafanikio ya muda mfupi ya kisiasa jambo ambalo linasababisha biashara zao kufa na kutofikia malengo ya kujikwamua kiuchumi.

Taasisi binafsi za fedha hazikopeshi kuanzisha biashara, bali zinakopesha kuendeleza biashara na ndio sababu zinafanya uchambuzi wa uwezo wa biashara ili kujiridhisha ikiwa biashara inakopesheka na kwa kiwango gani.

Sekta hii binafsi chini ya udhamini au ushirika na Serikali inapaswa kuhimizwa kutoa urari wa fedha za ubunifu na utekelezaji wa mawazo ya vijana ya biashara yanayoweza kutumika.

Serikali iweke utaratibu na kubeba jukumu la kuwa mdhamini mkuu ili hizi taasisi ziweze kuwakopesha vijana kwa kuzingatia wazo la biashara. Kwa mfano, kikundi cha vijana wataalum (maafisa mifugo, kilimo, ugani, fundi mchundo, wahasibu, masoko n.k.), wana wazo la kilimo cha zabibu, ardhi na soko vipo isipokuwa bidhaa mtaji, kama matrekta na mashine zingine, basi Serikali iwadhamini kupata mikopo katika taasisi hizo kwa utaratibu maalumu.

Kwa upande mwingine, tuna ardhi na rasilimali nyingi ambazo hazijatumika kwa tija. Tuna soko kubwa la ndani na nje hasa Jumuiya za SADC na EAC kwa bidhaa za kilimo (nafaka) na mifugo. Serikali ianzishe miradi maalumu ya mpango wa vijana au miradi ya kimkakati ya vijana itakayo ajiri kundi kubwa la vijana wenye taaluma mbalimbali chini ya usimamizi wa idara au kitengo maalumu cha Serikali chenye wataalamu wazoefu.

Kwa mfano, kila siku tunasimulia habari za soko la mahindi katika nchi zinazotuzunguka, lakini hatuchukui hatua za kuanzisha mashamba makubwa na kuhakikisha tunaweka mtaji wa kutosha katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa ajili ya kutoa mikopo yenye tija.

Tuna uhaba wa mafuta ya kula na sukari, lakini tumeacha matreka yaliyoko pale STAMICO yasubiri mkulima mmoja mmoja badala ya mteja wa kwanza kuwa vijana wa kitanzania kupitia Serikali yao.

Hatuna japo viwanda viwili vikubwa vya samaki Pwani nzima ya bahari yetu kutoka Tanga mpaka Mtwara. Hatuna mashamba makubwa ya kisasa ya mifugo wakati kuna viwanda vinakosa malighafi hii.

Je, kuna ndoto za kurejesha walau mfano wa kilichokuwa Tanganyika Packers mara hii iwe ni rasmi kwa kusindika nyama pori? Tujiulize vivyo hivyo katika gesi, chuma na madini mengine kama tuna viwanda vya kutengeneza bidhaa zinazotokana na rasilimali hizo.

Kama Serikali ilivyofanya maamuzi mazito ya kuanzisha na kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati ya SGR, JNHPP n.k. basi haina budi kufanya hivyo pia kwa kutenga bajeti ya uhakika kwa miaka mitano mfululizo kwa kuanzia ili kugharamia programu za uanagenzi, mfuko wa Business Support Fund na YSPs, vitafutwe vyanzo vipya maalumu kwa ajili ya vijana ili sote tufaidi keki ya Taifa.

Ninapoongelea miradi ya kimkakati namaanisha kwa mfano wafanyakazi 489,000 wa kada tofauti wanafanya kazi pamoja kuleta kile tunachokifahamu kama Samsung. Watu zaidi ya Milioni Moja katika jiji la Foxconn nchini China wanawajibika katika utengenezaji wa simu ya iPhone ambayo ni ya kifahari zaidi duniani. Inadaiwa kuwa wakati mmoja viwanda vya Foxconn vilikuwa na wahandisi 50,000 katika karakana moja ya kiwanda.

Kwa kujiingiza huko si kwamba Serikali inajihusisha na biashara, isipokuwa ni uingiliaji wa kimkakati ili kulinusuru kundi kubwa la vijana na kama ambavyo Serikali kupitia mashirika yake imeendelea kujihusisha na njia kuu za uchumi mfano usafiri; anga, bandari na pia kushirikiana na sekta binafsi katika afya, elimu n.k. kupunguza ukiritimba.

Jambo jingine, Serikali ikae vema na sekta binafsi, iikumbushe umuhimu wake katika kujihusisha na maslahi ya jamii katika kujenga uchumi wa nchi na kwa mantiki ya andiko hili mkazo uwe ajira kwa vijana kwa kuwa na sera nzuri kuhusu sekta hii. Serikali iwe tayari kuiokoa sekta binafsi pale inapokumbana na misukosuko.

Linapokuja suala la ushindani wa ajira na raia wa nje, sheria za ajira na kazi zisisitize kipaumbele cha ajira ni kwa watanzania hasa kwa nafasi wanazozimudu. Hivi karibuni tumemsikia Mkurugenzi wa Barrick Gold Mine katika taarifa yake akikiri utekelezaji wa sera hii kwa kuongeza wafanyakazi wengi wazawa, lakini makubaliano yenye manufaa kwa pande zote mbili lazima yazingatiwe tunapojihusisha katika ubia na kampuni au taasisi za kigeni.

Pamoja na Serikali kwa pamoja kuanzisha miradi mikubwa itakayotoa ajira ni lazima kila wizara, kama si RC au DC wapewe malengo ya kila mwaka katika maeneo yao ya kuzalisha fursa mpya za ajira. Ufuatiliaji uwepo na hatua zichukuliwe kwa wasiofikia malengo kama sababu haziridhishi. Viongozi wetu hawa wasibaki na majukumu ya kisiasa ama kuwa wakuu wa ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kiutawala.

Ni muhimu pia wajikite kutumia fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo yao kukuza uchumi wa watanzania kwa kubuni vyanzo vya ajira. Unakuta Mkoa una rasilimali (malighafi), lakini hauna kiwanda cha kuzitumia. RC au DC ameshindwa kuwaleta wadau pamoja na kuuza wazo. Kama ni Serikali iendelee kuibua na kutangaza fursa zilizopo na mpya ili vijana wazichangamkie.

Lakini, pamoja na niliyoyasahau, Benki zetu zinazomilikiwa na ziongoze njia katika kujenga viwanda na kuleta mabadiliko ya uchumi chini ya sera ya viwanda na kwa muktadha wa andiko hili ni katika kutoa mikopo kwa vijana. Benki za kibiashara lazima pia zihimizwe kama si kulazimishwa kufanya hivyo kama ilivyo kule China ambapo Sura ya IV, Ibara ya 34 ya sheria ya Jamhuri ya Watu wa China ya mwaka 1995 kuhusu Benki za biashara inasema: “Benki ya biashara itaendesha biashara ya mikopo kwa mujibu wa mahitaji ya maendeleo ya Taifa ya kiuchumi na kijamii chini ya usimamizi wa sera ya taifa ya viwanda.”

Tanzania hatuna kifungu kama hicho katika katiba yetu, lakini ikiwa tutaamua kuwatoa vijana kimasomaso, Serikali haina budi kukaa na Benki na Taasisi hizi za fedha, kuuza sera na muelekeo wake juu ya kuwasaidia vijana kuhusu ajira na kuziomba kuelekeza mawazo yao katika mikopo kwa vijana.

0621 014 417

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here