SERIKALI kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kwamba kuanzia mwisho wa mwezi huu wa 9 kunaweza kutokea El nino itakayoambatana na mvua kubwa na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kanda ya Ziwa n.k itaathirika zaidi.
Kufuatia hayo, Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete ametumia ziara yake anayoendelea nayo Jimboni kuwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwaka huu ambazo zinatajwa kuwa na uwezekano wa kuathiri maeneo mbalimbali kutokana na hali ya El Nino.
Kikwete ameyasema hayo jana Jumatatu Septemba 14, 2026 akizungumza kwenye Mkutano na wananchi wa Kata ya Msata akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani mabondeni na maeneo yaliyo kandokando ya mito kuhama mapema na kwenda maeneo salama ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo za El nino zilizotabiriwa kuwa kubwa na mafuriko.
Amesema, wananchi wa Msata wanapaswa kuchukua tahadhari zaidi kwa kuwa eneo hilo limepitiwa na Bonde la Mto Wami, hivyo wananchi waishio kando ya maeneo hayo wapo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko endapo mvua hizo zitanyesha kwa wingi.
Kikwete aliendelea kuwataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya Hewa na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo kusafisha mitaro.