Na Mvuda Jaffer , WAF-Mwanza
TANZANIA imekuwa ikifanya maandalizi ya kukabiliana na magonjwa na majanga ya muda mrefu huku uanzishwaji na uimarishaji wa Timu za Tiba za Dharura (EMT) ukiwa ni hatua muhimu katika kuendeleza maandalizi hayo.
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kiremeji, ambapo timu hiyo imejikita katika zoezi la uigaji (simulation) linalolenga kutathmini na kuimarisha uwezo wa timu katika kukabiliana na matukio ya dharura kwa ufanisi.
“Kukamilika kwa mafunzo ya matibabu ya dharura za afya kwa Timu ya Kitaifa ni hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na timu ya wataalamu wenye uwezo na utayari wa kutoa huduma za matibabu wakati wa majanga, milipuko ya magonjwa, ajali kubwa na matukio mengine ya dharura.” amesema Dkt. Kiremeji.
Dkt. Kiremeji amefafanua kuwa timu za wataalamu iya Usimamizi wa Wagonjwa (Case Management) na ya Kinga na Udhibiti wa Maambukizi (IPC), zimekuwa zikihitajika kwenda kwenye mikoa kwa ajili ya kuandaa maeneo maalum ya kutoa huduma za matibabu endapo mlipuko wa ugonjwa utatokea.
Naye, Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Watoto, Dkt. Yakayashi Mcrice ambaye ni moja ya washiriki wa mafunzo hayo amesema mafunzo hayo ni muhimu na ya lazima kwa kuwa mara kadhaa nchi imeshuhudia majanga na matukio ya dharura ikiwemo ajali za moto, ajali za treni na maporomoko ya ardhi hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada endelevu na sahihi za kuimarisha uwezo wa wataalamu katika kukabiliana na matukio ya dharura kwa kuhakikisha wananchi wanapata matibabu stahiki na kwa wakati.