TIMU ya Elimu kwa Umma kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imefanya ziara katika Kijiji cha Namhanga, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mkoa wa Morogoro, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu jitihada za Serikali za kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi katika maeneo ya vijijini na ambayo hayajahudumiwa vya kutosha.
Kijiji cha Namhanga ni miongoni mwa vijiji vilivyofikishiwa huduma za mawasiliano kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758 uliotekelezwa na Serikali kupitia UCSAF, kwa kushirikiana na makampuni ya simu nchini, mradi ambao umefikia vijiji takribani 1,400 nchi nzima.
Kupitia zoezi hilo, wananchi wameelimishwa kuhusu jukumu la Serikali katika kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kutosha kibiashara kwa watoa huduma, lakini yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.
Wananchi wa Namhanga sasa wanaweza kutumia mawasiliano kurahisisha shughuli zao za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuwasiliana, kupata taarifa kwa wakati, kutumia huduma za kifedha kwa njia ya simu na kunufaika na huduma za intaneti.
UCSAF inaendelea kutoa elimu kwa umma sambamba na utekelezaji wa miradi ya mawasiliano nchini, ikiwa ni mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa sawa za huduma za mawasiliano bila kujali maeneo wanayoishi.