RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema kutokana na hali ya El NiƱo na mvua kubwa zinazotarajiwa, huku akiagiza taasisi za Serikali kuendelea kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 11 Septemba 2026, baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Masjid Swafaa, Gongoni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa na maelekezo rasmi kutoka kwa Serikali na mamlaka husika, kuepuka maeneo hatarishi ikiwemo mabondeni, mikondo na njia za maji, pamoja na kuhama maeneo yenye hatari pale itakapohitajika.
Aidha, amezitaka Manispaa zote za Unguja na Pemba kuhakikisha mifereji na njia za maji zinasafishwa ili kupunguza madhara ya mafuriko.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, ikiwemo kuimarisha uwezo wa uokozi, kutoa msaada kwa waathirika na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu, chakula na dawa.
Amesisitiza kuwa taasisi zote zinazohusika zinapaswa kuwa katika hali ya utayari wakati wote ili kutoa huduma na msaada kwa wananchi kwa wakati.