RAIS wa FC Barcelona, Joan Laporta, ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mwenza wake, Mzee Hafidh Ameir Hassan, kilichotokea Septemba 7, 2026.
Salamu hizo zimewasilishwa kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ambaye yuko nchini Hispania kwa ziara maalum ya siku nne katika FC Barcelona kwa mwaliko wa Rais Laporta.
Laporta amekabidhi barua maalum ya rambirambi, akimtaka Rais Samia kuwa na subira, moyo wa ujasiri na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi.
Ziara ya Makonda pia inalenga kujadili fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na Barcelona katika ukuaji wa vipaji, maendeleo ya kiufundi na maandalizi ya AFCON 2027.
Barcelona inatambulika duniani kwa mfumo wake wa kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa klabu zinazotumika kama mfano katika maendeleo ya soka la kisasa.
Aidha, sehemu kubwa ya wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania iliyotwaa Kombe la Dunia 2026 wametokea FC Barcelona.