Na Mwandishi Wetu, Pemba
CHAMA cha Wakulima (AAFP) kimeishauri Serikali kuifanya marekebisho sheria Namba 5 ya vyama vingi ya mwaka 1992 na kanuni zake ili kukomesha matusi, kejeli na lugha chafu itakapoanza ruksa ya mikutano ya hadhara.
Mweyekiti wa AAFP Said Soud Said ameeleza hayo jana akiwa Wilaya ya Chakechake, Kisiwani Pemba na kueleza kila mwanasiasa achuje na kupima maneno yake kabla ya kutamka.
Soud alisema, Mataifa mengi duniani yamejikuta yakiingia kwenye mivutano, mitafaruku, mapigano na hata kusababisha umwagaji damu kutokana na chuki za kisiasa, vurugu au kutumika kwa lugha chafu.
Alisema, zipo tabia za baadhi ya wanasiasa wanaposhindwa kufafanua sera, mirengo yao kisiasa na itikadi za vyama vyao hujikuta wakitoa kejeli, matusi na kebehi, jambo ambalo alidai hupandikiza chuki na ukorofi katika jamii.
“Kulingana na ripoti iliyowasilishwa na kikosi Kazi cha Rais kupendekeza ianze mikutano ya hadhara, ni lazima Serikali mapema iweke tahadhari mikutano inapohutubiwa na wanasiasa. Nashauri ndimi zetu zidhibitiwe kikanuni na kisheria,” alisema Soud.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza kusema kuwa, vyama vya siasa vitabaki milele, lakini Taifa likizanishwa kwa hitilafu za maneno yenye tashwishi za kikabila, dini au ukanda ili kusimama tena haitakuwa kazi nyepesi.
Alisema, wapo baadhi ya wanasiasa ni hodari wa kutunga uongo, uzushi na fitna na kueneza ikiwemo kuwavunjia heshima watu wengine wakiwemo viongozi wa Kitaifa bila ushahidi wa tuhuma zinazotewa.
“Ikiwa siasa zetu zitafanyika kama baadhi ya watu wanavyoandika katika mitandao ya kijamii, Taifa letu litazama. Tufanye siasa zenye ukomavu kwa kutoa hoja yakinifu. Atakayemtuhumu mwenzake au kumvunjia heshima akishitakiwa atoe ushahidi,” alieleza Soud.
Pia, alisema mfumo wa vyama vingi si kibali kwa upinzani kuukejeli utawala au utawala kuuvunja upinzani kwa maneno yanayokiuka maadili, utu au kuvunja miiko ya utamaduni wetu.
Hata hivyo, Soud alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa Serikali yake kuunda kikosi Kazi kilichokusanya maoni ya wadau wa demokrasia ikiwemo pendekezo la kuruhusiwa kufanyika mikutano ya hadhara.
“Tumpe muda Rais Samia na vyombo vyake vya dola vifanye uchambuzi utakaoendelea kuliweka pamoja Taifa letu. Bado Tunahitaji kubaki na umoja wa Kitaifa, ustawi wa amani na utulivu wa kisiasa,” alisisitiza Soud.
Hivi karibuni, Kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania, kilipendekeza mikutano ya hadhara iruhusiwe sambamba na mabadiliko ya sheria mbalimbali zitakazowezesha mikutano hiyo kufanyika kwa ufanisi.
“Kikosi kazi kinapendekeza mikutano ya hadhara iruhusiwe kufanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria ya vyama vya siasa. Mikutano ya ndani ya vyama vya siasa iendelee kufanyika bila vikwazo vyovyote.
“Yafanyike marekebisho ya sheria ili kuhakikisha mikutano ya hadhara inafanyika kwa ufanisi. Sheria hizo ni pamoja na sheria ya vyama vya siasa sura ya 258, sheria ya jeshi la polisi na huduma saidizi, sura ya 3022 na kanuni za maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2019,” alisema Prof. Rwekaza Mukandala wakati akiwasilisha mapendekezo ya kikosi hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Oktoba 21, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.