Abood: Mikutano ya vyama isikwamishe maendeleo

0

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

MFANYABIASHARA maarufu mkoani Pwani Mohamed Saleh Abood, ameshauri mikutano ya hadhara itakapoanza ijenge umoja bila kuvuruga dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga maendeleo ya kiuchumi.

Abood alitoa rai hiyo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mara baada ya kikosi kazi cha Rais kilichokusanya maoni ya wadau wa demokrasia na kukabidhi ripoti yao kwa Rais mwishoni mwa wiki, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Abood alisema, imeshuhudiwa ndani ya kipindi kifupi Rais Samia akiwa madarakani amefanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo ikiwemo kuimarisha huduma za jamii kwa kiwango kikubwa mikoani hususan maeneo ya vijijini.

Alisema, ikiwa mikutano ya hadhara itakayoitishwa na vyama vya siasa itahutubiwa kwa nia ya kuishambulia Serikali ili kumkatisha tamaa Rais Samia kiutendaji, haitakuwa jambo la busara.

“Nimesikiza maoni ya Mwenyekiti wa kikosi kazi cha Rais Prof. Rwekaza Mukandala akishauri mikutano ya hadhara ianze. Pia matokeo ya urais yahojiwe mahakamani. Kama ni mikutano ya hadhara yenye kukwamisha juhudi za kujenga uchumi haitakuwa na mantiki yoyote,” alisema Abood.

Mfanyabiashara huyo alisema, kwa muda mfupi kwenye maeneo mengi nchini hususani vijijini, mambo yamebadilika; kuna vituo vingi vya afya, miradi ya maji safi, barabara za lami, umeme, madarasa, madawati na nyumba za kuishi walimu, waganga na wauguzi.

“Serikali imetoa nyenzo za usafiri na vitendea kazi kwa wataalam wa ugani sekta za kilimo na Afya. Mabilioni ya fedha yanayopelekwa halmashauri za Wilaya ni kikubwa kwa historia ya nchi yetu. Kuivuruga mipango hiyo kwa vijembe vya kisiasa nafikiri si jambo sahihi,” alieleza Abood.

Aidha, alivishauri vyama vya siasa viitumie mikutano hiyo kufichua kwa ushahidi watendaji wa Serikali wanaoshiriki ufisadi na uporaji rasilimali za taifa na kuepuka matamshi ya kumpaka matope Rais au kuleta hoja za udini ukabila na ukanda.

Mfanyabiashara huyo alisema, kwenye mitandao ya kijamii kuna mambo ya hovyo yanayoandikwa ambayo yanakwenda kinyume na miiko ya utamaduni wa kitanzania ikiwemo kueneza maneno yanayoweza kuleta mgawanyiko kwenye jamii.

“Lazima kufanyike marekebisho ya sheria kabla mikutano ya hadhara kuanza. Mtu akitamka neno la uongo bila kuwa na ushahidi akamatwe, afikishwe mbele ya sheria. Kila atakayetoa madai au shutuma awe na ushaidi mikononi,” alisisitiza Abood.

Hata hivyo, alimsifu Rais Samia kwa uungwana wake wa kusikiliza malalamiko ya wananchi wake hadi akaunda Kikosi kazi kilichokusanya maoni ya wadau na kuanza kuyafanyia kazi masuala kadhaa ambayo ni msingi na nyeti.

“Rais Samia amedhihirishia dunia ni muumini wa maendeoeo anayeheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora. Toka awe madarakani amefanya marekebisho makubwa ya kisheria yaliyopunguza, malalamiko, ubaguzi na maonevu,” alisema Abood.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here