Kamari ni moja ya vyanzo vya ugonjwa wa akili

0

Na Nizar Visram

NCHI yetu imeingiliwa na utamaduni mpya wa kamari iliyoingizwa nchini na makampuni ya kigeni. Tumeona jinsi vijana wetu wakitumbukia katika mtindo huu wa maisha, wakishawishiwa na matangazo ya redio na runinga.

Hapo zamani Serikali ilianzisha kamari yake iliyoitwa Bahati Nasibu ya Taifa. Kamari haibadiliki kwa sababu unaipa jina jipya la Bahati Nasibu au mchezo wa kubahatisha.

Kamari hii ya Taifa iliendelea kwa muda mrefu. Mara tukaona tunakumbwa na kamari kutoka Ulaya. Ikapewa jina la ‘kubeti’ au ‘tatu mzuka’ na kadhalika. Ni kamari inayotegemea mtandao au simu ya mkononi au ‘mkeka’. Kamari hii ikapamba moto na vijana wetu wakaghumiwa na ahadi ya ‘kupata mshahara bure mwaka mzima bila ya kufanya kazi.’

Wengine walishinda nyumba, wengine bodaboda, wengine mamilioni mkononi. Alimradi vijana wetu waliacha masomo na kukimbilia kamari. Serikali nayo ikafurahia kodi iliyokusanya. Kigezo kikawa ni kodi, bila kujali kuwa vijana wetu wanawehuka na kuacha masomo au kazi.

Wakati fulani, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ilitangaza kuzuia ‘kwa muda’ matangazo yote ya michezo ya kubahatisha katika redio na runinga. Bodi ilisema, matangazo hayo yamekuwa mengi kiasi cha ‘kuharibu taswira’ ya michezo hiyo. Pili, sababu waliyotoa ni kuwa, matangazo yamekuwa mengi kiasi cha ‘kuharibu taswira’ ya michezo hii.

Kuna wanaosema kamari ina faida, kwani wengi wameishia wakitajirika baada ya fedha chache walizowekeza. Ukweli ni kuwa hayo matangazo hutuambia tu kuhusu walioshinda, hawataji asilani walioshindwa. Asilimia 95 ya wacheza kamari na michezo ya kubahatisha hupoteza fedha zao na hiki ni kiwango kikubwa kuliko wale wanaoshinda.

Walioshinda ni watu 19 au 20, lakini hatuambiwi waliocheza nchi nzima walikua wangapi. Ni dhahiri kuwa idadi ya washindi ni ndogo mno ukilinganisha na idadi ya washiriki wote. Ni kweli kuna washindi wenye bahati, ila wanaoliwa ni wengi zaidi.

Wengine wanasema kushinda hata kwa kiwango cha Mamilioni sio tija, kwani kamari ni ulevi. Hivyo “wewe umeshinda vilaki kadhaa, wengine? Unajua athari kiasi gani imeshaleta? Kamari ina athari za kisaikolojia za muda mrefu maishani mwako.”

Moja ya athari za kamari ni kumfanya mtu awe tegemezi wa kamari. Analemaa kimawazo. Matokeo yake ni kupunguza ufanisi na ubunifu katika shughuli za uzalishaji. Kamari inamfanya mtu aamini kwamba, ataweza kuyatatua matatizo yake ya kifedha kwa njia ya mkato na kirahisi kwa kucheza kamari. Huu ni ugonjwa wa kisaikolojia.

Suala hili la kamari halikuibuka ghafla pale Ikulu, na hao viongozi wa dini hawakuwa wakitoa hoja mpya. Kwani kwa muda wa miaka kadha kumezuka makundi ya vijana kugeukia mchezo wa kubahatisha. Kila kukicha vituo vya kamari ya soka maarufu kama ‘kubeti’ vimekuwa vikiongezeka.

Mashabiki wamekuwa wakitumia fedha kwa kubashiri mechi za mpira za mataifa ya nje. Vituo vya kuchezesha vikachipuka kama uyoga katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam na mikoani.

Takwimu za Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu, zilionyesha kuwa mnamo mwaka 2017 kwa nchi nzima kulikuwa na vituo vya kubeti 2,684 huku Mkoa wa Dar es Salaam pekee ukiwa na vituo 1,344.

Gazeti moja hapa jijini lilifanya utafiti na kutembelea maeneo ya Mwenge, Magomeni, Kariakoo, Tandale, Tandika, Manzese, Mikocheni, Msasani na Temeke na kukuta makundi ya watu wakiwa na makaratasi maarufu kwa jina la ‘mkeka’ huku wakibashiri mechi mbalimbali kwa viwango tofauti vya fedha.

Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha aliliambia gazeti hilo kuwa michezo hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwenye bodi hiyo na kuongeza mzunguko wa fedha unaozidi Sh bilioni 1.4 kwa mwezi. “Huu mchezo umekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa mwaka 2012/13 hadi Desemba 2015 Shilingi bilioni 14.0 zilikusanywa na pia kutoa ajira zaidi ya 7,000.”

Akasema michezo hiyo ya kubahatisha inafanya vizuri, kwani mapato yake kwa bodi hiyo hufikia Shilingi Bilioni 14 kwa mwaka. Swali ni iwapo Serikali iko tayari kupiga marufuku kamari inayoipatia fedha zote hizi. Kuna watakaosema hatuwezi kuharibu vizazi vyetu vijavyo kwa sababu kamari inaingiza kodi. Mpaka sasa tumezuia utangazaji tu. Huenda wahusika wakatafuta njia mbadala ya kuendeleza kamari nchini.

Kama tutazuia kamari, basi hatutakuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo. Nchi ya jirani ya Uganda imezuia mchezo wa kubeti baada ya Rais Yoweri Museveni kuagiza kuwa mchezo huo upigwe marufuku kwa sababu unawapotosha vijana na kuwafanya waaache kufanya kazi. Serikali ya Uganda imesema, haitatoa leseni mpya kwa kampuni za kamari, na kwa wale wenye leseni hawataongezewa muda zitakapomalizika.

Mnamo Decemba 2018 Uingereza ilizuia matangazo ya kamari katika mtandao kwa sababu jambo hilo lina madhara kwa watoto na vijana. Wakati mechi za mpira zinapotangazwa mubashara katika runinga watu wengi wamekuwa wakibeti. Hii ilifika kiwango hatarishi na inakisiwa zaidi ya watu 430,000, wengi wao wakiwa watoto, wameingia mtegoni.

Gazeti moja nchini Uingereza lilifanya utafiti na kuona kuwa wakati kombe la dunia likichezwa kwa muda wa dakika 90, watoto walielemewa na matangazo ya kamari, kiasi kwamba wengi wao walishindwa kujizuia. Vituo vya kurushia matangazo ilikuwa ikivuna takriban Dola milioni 200 kutokana na matangazo haya.

Kampuni za kamari pia zilikuwa zikiingiza mamilioni. Sasa yote haya yamesimamishwa nchini Uingereza. Nchini Marekani kamari imekuwa chanzo cha magonjwa. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 ulidhihirisha kuwa takriban watu milioni sita walikuwa wanahitaji matibabu kutokana na mazoea ya Kamari.

Jambo hili limehakikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo kwa mara ya kwanza limeorodhesha kamari kuwa ni chanzo cha ugonjwa wa akili. Baadhi ya nchi kama Uingereza tayari zimeanzisha kliniki maalum za kuwasaidia watu wenye ugonjwa huu.

Daktari Richard Graham ni mtaalamu wa magonjwa haya katika hospitali ya Nightingale jijini London. Yeye ameipongeza serikali kwa kutambua janga hili la kamari. Yeye anawatibu wagonjwa 50 kila mwaka ambao maisha yao yameathirika kutokana na Kamari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here