Je, asili ya muziki wa taarabu ni Misri?

0

Na Adeladius Makwega

TAARABU ni muziki unaopendwa na wenye umaarufu mno katika Mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi, Zambia, Malawi na hata Msumbiji na maeneo mengi ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Inakadiriwa kuwa, muziki huu umekuwepo katika eneo hili kwa zaidi ya karne moja yaani miaka 100 sasa.

Wachunguzi wa masuala ya muziki wanasema kuwa, muziki huu umepata mabadiliko makubwa kuanzia miaka ya 1990 kutokana na ukuaji mkubwa wa taarabu ya kileo yaani modern taarabu. Jambo hili likasababisha kuwepo na aina mbili za taarabu nayo ni taarabu Asilia na taarabu ya Kileo.

Ili kuufahamu vizuri muziki huu, ni vizuri kutambua kwa kina asili ya neno lenyewe taarabu ni nini? Neno hili lina asili ya lugha ya Kiarabu na linaweza kunyambuliwa kama ifuatavyo; – Taariba, Yatiriba, Taraba; Maneno haya yote yana maana inayoshabiana nayo ni starehe, furaha, burudani au raha.

Maana hii inalingana kabisa na lengo la kuwepo muziki huu wa taarabu yaani ni kutumbuiza na kutoa burudani japokuwa malengo mengine yanakuwepo hapo na hiyo burudani mara zote inatolewa katika sherehe kama vile ndoa, kukaribisha wageni na hata katika shughuli za kisiasa wakati wa sultani.

Kwa hakika burudani yoyote ile ni mali ya jamii husika ndiyo maana Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na MIchezo inaamini pia katika kuwepo kwa aina hizo mbili za taarabu yani ile asilia na ya kileo.

“Nakubaliana na aina hizo mbili za taarabu, na aina hizo zinatokea kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali haswa kutokana na kuwepo na jambo linaloizunguka jamii, ile asilia kwa sehemu kubwa ina kuwa na ujumbe fulani, lakini ile ya kileo yenyewe inalenga katika vijembe, kufurahisha na wakati mwingine inafundisha pia,” anasema Amne Kassam ambaye ni Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na MIchezo.

Je, muziki una asili ya Arabuni kama lilivyo neon lenyewe? Majibu ya swali hili yanaweza kuwa ndiyo, lakini pia na hapana. Lakini, nakuuma sikio kuwa tamati ya yote ile habari ya mwamba ngoma, ngozi huvutia kwake inaweza kuwepo hapa.

Mtazamo wa kwanza unashikilia kuwa asili ya taarabu ni Misri, kwani Sultan wa Zanzibar Seyyid Barghash ambaye aliingoza Zanzibar tangu 1870 hadi 1888 aliwaalika wanamuziki wa taarabu kutoka Misri ili waende kwenye kisiwa hicho cha Marashi ya Karafuu wamchezee muziki wao yeye na watu wake katika makazi yake Beit-el-Ajaib.

“Baadaye alimpeleka Misri mwanamuziki Mohammed Ibrahim ili aweze kujifunza ustadi wa nyimbo za taarabu na pindi tu aliporejea Zanzibar, alipanda mbegu ya taarabu Afrika Mashariki. Mohammed Ibrahim aliunda chama cha watribu cha nyumba ya mfalme. Sultan Seyyid Bargash alitimiza mahitaji yote ya kikundi hiki na hivyo kikundi hiki hakikuruhusiwa kucheza nyimbo zake kwingineko isipokuwa katika ikulu ya mfalme pekee.” anasema Amne Kassam.

Wanachama wengine wa kikundi hiki ni pamoja na Ajmi Bin Abdalla na Mussa Bulushi ambaye alikuwa mwalimu wa Siti Binti Saad, Shaib Abeid na Mohammad Liyas. Nyimbo zao zote ziliimbwa kwa Kiarabu. Mtazamo huu wa asili ya taarabu unajikita katika imani kuwa kila kilicho kizuri kililetwa kutoka nje ya Afrika.

Mtazamo wa pili, muziki huu ulitokana na mwingiliano wa utamaduni wa Waswahili na tamaduni nyingine mbalimbali. Aidha, muziki wa taarabu umeathiriwa pakubwa na utamaduni wa Kihindi kama inavyodhihirika katika miundo ya baadhi ya tamaduni maarufu za Waswahili. Hili linadhihirika katika filamu za Kihindi ambazo huakisi msingi thabiti wa toni za baadhi ya nyimbo za taarabu zinazovutia sana katika miji ya Pwani ya Bara Hindi.

“Wageni kutoka Uarabuni, Uchina, Misri na Indonesia waliozuru Pwani ya Afrika Mashariki waliathiriwa na utamaduni wao ambao ni pamoja na muziki na ala za kuuchezea muziki huo. Baada ya kutambua kuwa wangepumzika katika pwani hii kwa muda, walianza kujitumbuiza kwa nyimbo zao na wenyeji wa Pwani.” aliongeza Amne.

Taarabu iliibuka kutokana na mtangamano kati ya utamaduni wa Kibantu na ule wa Kiarabu. Miji wa Lamu ambao umo kaskazini mwa Kenya ndio unaohusishwa na kitovu cha nyimbo za taarabu kabla ya nyimbo hizi kusambaa na kuenea kwingineko mathalani visiwa vya Pemba.

Hivyo basi, taarabu ilienea katika Afrika Mashariki kutokana na mwingiliano wa mitindo ya miziki ya kiasili na miziki ya watu wenye tamaduni za Ulaya, Kiajemi na Marekani waliokutana na Waswahili.

“Mwanachama na mwanamuziki wa kikundi cha taarabu Zanzibar; Ikhwani safaa, Sheikh Abeid aliyeishi kati ya miaka ya 1890-1974 alikiri kufunzwa nyimbo za taarabu kwa mitindo ya Kilamu. Mtazamo huu unashikiliwa na wengi wa wasomi wa Kiafrika ambao kwa pamoja wanaendeleza dhana kuwa hata Afrika imekuwa na utamaduni mzuri,” anadokeza Hadija Kisubi, Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.

Muziki wa taarabu umekuwa na historia ya kuwa na aina nyingi za taarabu kama vile taarabu ya Zanzibar, taarabu ya Dar es Salaam, taarabu ya Mombasa na taarabu ya Tanga. Mpaka leo mabadiliko katika uwasilishaji wa taarabu yangali yanaendelea.

Taarabu imekuwa pia ni ya kucheza na si kusikiliza ujumbe tu kama ilivyokuwa zamani. Hivyo, kuna uwezekano kuwa muziki wa taarabu katika Afrika Mashariki ulikuwa na mitindo mingi tofauti ya uchezaji na majina tofauti kadri ulivyokua na kuenea.

Kisubi anamalizia kwa kusema taarabu asilia ipo inayochezwa na wanawake tu na ipo ile inayochezwa na wanaume tu. Naweka kalamu yangu chini katika kutazama asili ya muziki wa taarabu iwe Misri au Pwani ya Bahari ya Hindi. Kazi kwako wewe msomaji wa makala haya kuchagua upande, nakutakia siku njema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here