Jamii iliyokengeuka utaijua kipindi cha majanga

0

Na Yahya Msangi

NIANZE kwa kutoa pole kwa wahanga wote wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision iliyotokea katika eneo la Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba, Mkoani Kagera ambapo watu 19 walipoteza maisha na wengine 26 waliokolewa.

Kwanza, nimpe pole maalum Mwana – diaspora mwenzetu anayeishi Abuja Nigeria aliyepoteza watoto wake wawili wa kike ambao walikwenda Mkoani humo kwa ajili ya kushiriki shughuli za mazishi.

Lakini, kwa upande mwingine ajali hiyo kwa mara nyingine imetuonyesha jinsi jamii yetu ilivyokengeuka. Pili, ukiwasoma baadhi ya wanasiasa hususani wa vyama vya upinzani kupitia kwenye mitandao ya Kijamii, utagundua jinsi walivyogeuza msiba kuwa sehemu ya mtaji wa kisiasa.

Ni kama wamefurahi ajali hiyo kutokea. Kwa mtizamo wao eti ajali imeonyesha jinsi Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) isivyokuwa makini. Hata ingekuwa madai yao ni ya kweli, lakini msibani? Kwamba, nyumba ya jirani kuna mtoto kapoteza maisha kwa maralia, wewe unaanza kusema ‘hakununua chandaruaaa…’

Ni hawa hawa akipoteza maisha mwanachama au kiongozi wao wanaanza kusema ‘Serikali inabaguaaa.’ Kisa Serikali haikushiriki mazishi. Thamini misiba ya wengine na wako utathaminiwa.

Tatu, watu wamejikita kuhusu uokoaji. Mara sijui eti wavuvi ndiyo wameshiriki. Mara ndege imevutwa kwa kamba. Mara vyombo duni! Hivi wavuvi si huvua samaki muda wote? Mlitegemea Nani waone ndege iliyozama kuliko wao? Flight 370 Malaysia Airlines waliyoiona ikiyumba walikuwa wavuvi karibu na Pwani ya Kisiwa cha Penang.

Ndiyo waliotoa taarifa kwamba, kuna ndege ina matatizo. Hiyo peke yake inawaweka katika kundi la uokoaji. Si ajabu wavuvi kushiriki uokoaji. Hivi wangekaa wasubiri kikosi cha uokoaji kije? Kwa kuwa wale wavuvi wana akili kuzidi nyie waliona kutumia kamba kuivuta itoke kwenye kina kirefu itasaidia.

Ndege iliyoanguka mtoni Hudson New York ilivutwa kwa kamba. Hakuna cha ajabu. Kwenye tukio la ajali chochote kinachoweza kuokoa hutumika. Watu wanajadili matokeo badala ya chanzo. Wanaangalia walipoangukia wanasahau kuangalia walipojikwaa Kwa akili hii ajali hazitaisha Tanzania.

Hatusikii watu wakijadili kuhusu ubora wa ndege, ujuzi wa marubani, ubora wa kiwanja na vifaa, ujuzi wa waongoza ndege pale kiwanjani. Je, protocol ya uokoaji ilifuatwa? n k. Watu wenye fikra finyu wamejikita kujadili kamba na wavuvi.

Ni kwa nini walipofika Misenyi marubani waliamua kurudi Bukoba Airport badala ya kwenda Entebbe? Hawakuongea na ‘control tower’? Kwa Nini walipofika na kuona hali haijabadilika hawakwenda Chato au Mwanza? Je, ndege za Precision zinapata matengenezo ipasavyo?

Wanatengenezea wapi? Kuna rekodi za kuonyesha ilipata matengenezo ya mwisho lini? Ndege ilikuwa na vifaa vya kuiwezesha kutua usiku? Tumewasikia viongozi wa Precision wakitoa taarifa ya ajali ya ndege yao bila kuweka maelezo muhimu. Je, kiwanja kina vifaa vya kuongoza ndege usiku au wakati wa mvua? Je, pilot waliongozwa vyema?

Nne, tujitahidi kufuata ‘protocol’ ya Zimamoto au Vikosi vya uokoaji. Sio kila anayejisikia anatoa taarifa yake. Tumekengeuka mno, na majanga yanaonyesha udhaifu wetu kama jamii ya Kitanzania. Narudia kutoa pole.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here