Halmashauri zatakiwa kuzuia uchimbaji holela wa mchanga

0

SERIKALI imezitaka halmashauri zote nchini kuendelea kusimamia kikamilifu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 ili kuzuia uchimbaji wa mchanga holela kudhibiti kupanuka kwa mito huku ikiendelea kutenga fedha za kukabiliana na changamoto hiyo.

Sanjari hilo imezitaka halmashauri hizo kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira ili kudhibiti upanukaji wa mito na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ametoa wito huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Askofu Dkt. Josephat Gwajima katika swali lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalumu Mariamu Kisangi kuhusu lini ahadi ya kupeleka fedha za ujenzi wa mito iliyopanuka katika Jimbo la Kawe itatekelezwa.

Akijibu swali hilo alisema, Serikali inatambua changamoto ya kupanuka kwa mito iliyopo katika Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam ikiwemo Nyakasangwe, Tegeta, Mbezi, Mlalakuwa, Mpiji na Ndubwi inayotiriririsha maji yake katika Bahari ya Hindi.

Aidha, Khamis amefafanua kuwa kupanuka kwa mito hiyo ni kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kufanyika kwa shughuli za kibinadamu zisizo endelevu ndani ya mita 60 kinyume cha kifungu namba 57 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, alisema Serikali itaendelea kutenga na kutafuta fedha kupitia Mifuko mbalimbali Mazingira ikiwemo Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ya Kijani (GCF) pamoja na Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (AF) kwa ajili ya ujenzi wa mito hiyo.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis aliongeza kuwa, Serikali itaanza ujenzi wa mito iliyopanuka katika Jimbo la Kawe kadri fedha zitakavyopatikana.

Akijibu swali la nyongeza la Mariamu kuwa Serikali ina mpango gani wa dharula wa kunusuru nyumba zinazoanguka kutokana na mafuriko, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imejenga vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka maeneo korofi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here