Eswatini, waathirika wa UKIMWI wanaanzia miaka 15 hadi 45

0

Na Charles Charles

WAKATI ambapo serikali nyingi duniani hufikiria kuongeza bajeti zake za kila mwaka kwa ajili ya maendeleo mpaka maradufu, hali hiyo nchini Swaziland (hivi sasa inajulikana kama Eswatini) iko kinyume.

Inafahamika kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa unaoitwa Upungufu wa Kinga Mwilini, maarufu kwa kifupi cha UKIMWI yanazitikisa nchi masikini, nyingi kati yake zikitoka Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Unatikisa uchumi wa nchi kwa sababu unaathiri nguvukazi nyingi kwa kushambulia zaidi watu wenye umri wa kufanya kazi kuanzia mashambani, ofisini, viwandani, migodini na sehemu nyingine zikiwemo zinazoihusu moja kwa moja sekta ya biashara.

Hata hivyo, athari za magonjwa nyemelezi yatokanayo na virusi vya UKIMWI hutegemea miundombinu ya uchumi kutoka nchi moja hadi nyingine, lakini kubwa kuliko zote ni kupungua kwa nguvukazi na kuongezeka kwa gharama za maisha ya watu.

Utafiti unaonyesha kuwa, kuathirika kwa idadi kubwa ya vijana wanaombukizwa virusi vinavyosababisha maradhi nyemelezi ya ugonjwa huo, ndiko kunakoathiri kwa kiwango kikubwa zaidi uchumi mpaka shughuli nyingine za kidunia, kibara na nchi moja moja.

Kutokana na hali hiyo, pale inapotokea kuwa UKIMWI umeenea kwa kiwango kikubwa zaidi katika nguvukazi ya Taifa au katika jamii, madhara yake huwa ni makubwa kuliko inavyokuwa kwa takwimu zinazohusu vifo.

Utafiti unaonyesha kwamba, gharama za moja kwa moja zitokanazo na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni kuongezeka kwa matumizi yanayogusa matibabu na mazishi, lakini zisizokuwa za moja kwa moja zinajumuisha pamoja na mambo mengine; kupotea kwa muda mwingi zaidi unaotumika kuuguza wagonjwa, mafunzo kwa watumishi wapya wanaoziba mapengo yanayoachwa na waathirika mahali pa kazi na matunzo kwa watoto wanaofiwa na wazazi wao.

Lakini, kama gharama hizo zinafanyika nje ya taratibu za kibenki, hapo mara nyingi pato ama uchumi wa Taifa unaathirika au unakumbwa na mtikisiko.

Nje ya shughuli zinazohusu mzunguko wa fedha kupitia benki, kilimonchini Swaziland nacho kimeathiriwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo ambapo kwa mfano, utafiti uliofanywa mara ya kwanza mwaka 1996 ulionyesha kwamba, ingawa sekta hiyo pekee ilikuwa imeajiri asilimia 33 ya nguvukazi yote, lakini ilikuwa ikichangia asilimia 11.6 pekee katika pato la Taifa.

Mazao makubwa ya biashara nchini humo ni miwa na pamba huku sekta ya mifugo ikikua, lakini pia viwanda vya bidhaa za kibiashara navyo vinazidi kuwa muhimu.

Ndiyo maana, utafiti uleule wa kwanza kuhusu athari za maambukizi yatokanayo na virusi vya UKIMWI ulionyesha kwamba, sekta hiyo ilikuwa ikichangia asilimia 33.1 ya pato la Taifa huku vingi vikiwa ni vya bidhaa za chakula, mazao ya mifugo na ya misitu. Lakini, iliyo kubwa zaidi ni sekta ya huduma za jamii iliyokuwa ikichangia wastani wa asilimia 47 ya ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo, takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa sekta ya kilimo, uwindaji, shughuli za misitu na uvuvi inaongoza kwa kuajiri asilimia 23.13, migodi na madini asilimia 2.41 huku viwanda vikiajiriasilimia 10.91.

Nyingine na viwango vya asilimia zake vikionyeshwa kwenye mabano ni sekta za nishati ya umeme, gesi na maji (1.41), ujenzi (5.36), biashara, migahawa na hoteli (7.49) huku sekta ya usafiri, mawasiliano na uchukuzi ikiwa ni asilimia 5.67.

Sekta nyingine ni za shughuli za kibenki, huduma za bima, mashamba makubwa na biashara (3.44) huku shughuli mbalimbali za kijamii zikiajiri asilimia 16.8 ya nguvukazi yote na kufanya asilimia 61.50, takwimu ambazo hata hivyo hazikujumuisha majeshi na watu waliokosa au wanaotafuta ajira.

Aidha, utafiti uliofanywa kuhusu janga hili kiuchumi unaonyesha kuwa waathirika wa kwanza huwa ni wahusika wenyewe walioambukizwa virusi hivyo na familia zao, kisha inafuatia jamii inayowazunguka na hatimaye linagusa uchumi na biashara katika ngazi nyingine.

Madhara kwa uchumi yatokanayo na maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanaanzia kwa mwathirika mwenyewe, kisha inafuatia familia yake na kuenea katika ngazi nyingine za kijamii.

Mathalani, gharama za matibabu kwa familia yenye mwathirika huongezeka pindi akigundulika. Wengine wanaoathirika ni waume, wake au wapenzi wa waathirika kwa kukosa haki zao za ndoa katika upande wa kwanza, halafu watoto kwa kupungukiwa au kukosa huduma mbalimbali wanazopaswa kupata ambazo ni pamoja na mahitaji ya elimu.

Hata hivyo, athari nyingine zinazoweza kufuatia ni kama mwathirika atapoteza maisha yake kwa vile pengo lake linakuwa la kudumu. Hapo watoto kwa mfano watakosa moja kwa moja fursa muhimu ya kupata elimu kwa kukosa au kupungukiwa na mzazi mmoja, hasa ikitokea kwamba ndiye aliyekuwa tegemeo katika masomo yao kwa kuwalipia ada au kuwasimamia kupata mahitaji mengine hasa ya lazima ili waweze kusoma.

Ikitokea hivyo, watoto hao si tu kwamba wanaweza kuyumba ama hata kuacha kabisa shule au chuo, lakini janga hilo huharibu kila kitukatika maisha yao ya baadaye kwao binafsi au ya familia zao endapo watakuja kuwa nazo mbele ya safari.

Kwa mfano, nchini Swaziland ambako utafiti unaonyesha kuwa asilimia 90 ya waathirika wa maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi wana umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 49, uwezo wa familia zao kiuchumi hupungua kwa vile kizazi hicho kinakuwa ni cha nguvukazi inayotegemewa.

Takwimu za waathirika zinatisha zaidi kwa sababu maambukizi nchini humo yanapanda kwa wastani wa asilimia 102 kwa mwaka ambapo kwa mfano mwaka 1994, wananchi wa Swaziland walioambukizwa virusi hivyo walikuwa 10,060 na miaka 12 baadaye ilipofika mwaka 2006 walikuwa wameongezeka na kufikia 85,910.

Hali hiyo pia na kama ilivyobainishwa hapo mwanzo ni kuwa tatizo la watoto yatima waliofiwa na wazazi wao kukosa ada, sare, vitabu na mahitaji mengine linaongezeka kwa kasi kila mwaka, hatua inayoathiri masomo yao na kuharibu mpaka maisha yao ya baadaye.

Mbali na hilo, maambukizi ya virusi hivyo nchini humo yanaonyesha kwamba, sekta ya kilimo ambayo kama ilivyo Tanzania na sehemu nyingine Afrika kwamba ndiyo inaajiri watu wengi zaidi imeathirika pia.

Kutokana na kupungua kwa nguvukazi inayokuwa mashambani, shughuli mbalimbali na muhimu za kilimo cha mazao yakiwemo ya chakula, biashara na ufugaji zinaathirika na kusababisha uchumi wa nchi kutikisika.

Kana kwamba haitoshi, kupungua kwa nguvukazi ya kilimo hakuishii katika kulima au kupanda peke yake isipokuwa pia inagusa mpaka maeneo mengineyo kama ya mavuno, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao yanayovunwa na kadhalika.

Mbali na mazao ya chakula, mfano mmojawapo utokanao na athari za maambukizi ya virusi hivyo nchini Swaziland unaohusu mazao ya biashara ni ule wa Kiwanda cha Sukari cha Mhlume, kile ambacho kimeajiri wafanyakazi wa kudumu na wa muda mfupi mpaka kwenye mashamba yake chenyewe.

Kiwanda hicho ambacho kinatoa hadi huduma ya makazi kwa wafanyakazi wake na familia zao kilikumbwa pia na janga hilo, hatua iliyosababisha kitikisike kwa mapato yake kuporomoka.

Kiliathirika kutokana na baadhi ya wafanyakazi wake kupata maambukizi yaliyopelekea kupungua kwa nguvukazi na hasa iliyokuwa mashambani, kuongezeka kwa gharama za matibabu na matunzo yao huku hayo yakienda sambamba na kupungua kwa uzalishaji wa sukari na kuathiri mapato yake kibiashara.

Inaelezwa kwamba asilimia 30 ya vifo vyote vya wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa miaka mitatu iliyopita vilitokana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Pamoja na mambo mengine, hali hiyo ilisababisha kupungua kwa uzalishaji na kuongezeka kwa gharama za matibabu.

Gharama hizo zinajumuisha matibabu na matunzo, ada za maisha na mafunzo kwa ajili ya wafanyakazi wapya wanaopaswa kuajiriwa mara kwa mara ili kuziba mapengo yanayoachwa na watangulizi wao.

Serikali ya Swaziland ikiongozwa na Mfalme Mswati wa Pili ambaye aliingia madarakani mwaka 1986, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na baba yake mzazi, marehemu Mfalme Sobhuza wa Pili imekuwa ikitoa likizo ya miezi sita kwa watumishi wenye maradhi yatokanayo na virusi vya Ukimwi.

Hatua hiyo inakwenda sambamba na malipo ya mshahara kamili kwao, kisha hufuatiwa na miezi sita mingine wanayolipwa nusu mshahara kabla ya kuja kuachishwa kazi kwa ugonjwa na kulipwa mafao yao yote.

Lakini, kwa vile kila mtumishi huwa na faida zake mwenyewe, kuondoka kazini kwa baadhi yao huwa kunaacha athari kubwa kutokana na fani zao ambapo kwa mfano, kundi hili linaweza kujumuisha wahandisi wa kada tofauti, wataalamu mabingwa wa uchumi na hata vinginevyo.

Sekta ambazo zinatajwa kwamba kuna wakati huathirika zaidi kutokana na kupoteza nguvukazi yake ni pamoja na uchukuzi na usafirishaji, madini, afya, elimu, maji na viwanda.

Inaelezwa kuwa katika sekta ya afya, athari kubwa zinatokana na janga hilo ni mbili; kuongezeka kwa idadi ya waathirika na kupanda kwa mahitaji ya huduma kwao na huduma za matibabu na mahitaji mengine kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi huwa za juu kuliko zinazohusu wagonjwa wengine, hivyo pia hugharimu fedha nyingi zaidi.

Ukweli huo unathibitishwa na gharama za kutibu mgonjwa mmoja tu wa Ukimwi nchini Swaziland kuwa Euro 4,000 kwa mwaka, fedha ambazo ni sawa na wastani wa Shilingi Milioni 10.4 za Kitanzania na hivyo kusababisha asilimia 13 ya bajeti ya Wizara ya Afya kutumika kwa ajili hiyo pekee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here