Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila
Na Mwandishi Wetu
KUNA wakati jiji halihitaji tamko jingine kuhusu usafi, linahitaji mfumo mpya. Huo ndio mwelekeo unaojitokeza katika hatua mpya zinazochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika kukabiliana na changamoto ya takataka na uchafu jijini.
Katika kikao chake na wahariri na waandishi wa habari Septemba 17, 2026, Chalamila alitangaza mfululizo wa hatua zinazolenga kubadili namna jiji linavyoshughulikia takataka; kuanzia zinapozalishwa majumbani hadi zinapofikishwa katika maeneo ya mwisho ya utupaji na uchakataji.
Hatua hizo zinazochukuliwa, ni matokeo ya kauli iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa na Katibu Tawala wa Mkoa.
Rais Samia alisema, ni aibu kwa miji kuendelea kuwa michafu wakati nchi inalenga kukua kiuchumi na kuvutia watalii ambapo ili kukabiliana na changamoto hiyo, aliwataka viongozi hao wapya na mamlaka zinazohusika kuchukua hatua za haraka kwa kusimamia usafi kikamilifu.
Aidha, alikosoa utaratibu wa halmashauri na wilaya kuwapa mikataba ya usafi madiwani au watu wasio na vifaa na uwezo badala ya wakandarasi wenye sifa, huku akiagiza kuwa walioshindwa kutekeleza wajibu wao waondolewe na mikataba ipewe watu wenye uwezo wa kuweka miji safi.
Kwenye mkutano wake na wahariri, Chalamila alikiri kuhusu suala la jiji analoliongoza kukithiri kwa uchafu, “Tulisahau kwa muda, jambo ambalo limepelekea Mheshimiwa Rais kwa jicho lake kuona Dar es Salaam ni chafu. Tunakiri kwamba, Rais alichokiona kwetu hajatuonea.”
Chalamila akatangaza mikakati kadhaa ya kurejesha hadhi ya jiji hilo linalokua kwa kasi ambalo ni wazi suala la usafi haliwezi kutatuliwa kwa magari ya taka pekee. Kila siku taka huzalishwa majumbani, masokoni, kwenye migahawa, vituo vya usafiri, maeneo ya biashara na maeneo mengine ya mikusanyiko.
Kama taka hizo hazitenganishwi, hazikusanywi kwa wakati na hazipelekwi kwenye mfumo sahihi wa uchakataji, tatizo huendelea kujirudia. Ndiyo maana mpango wa Chalamila unagusa mlolongo mzima likiwemo pia suala la kubadili tabia za wakazi wake n ahata teknolojia.
Mkoa umewataka wakandarasi wa uzoaji taka kuboresha vifaa na teknolojia ndani ya miezi mitatu, huku kukiwa na mpango wa kufanya baadhi ya shughuli za usafi nyakati za usiku. Hapa ndipo utekelezaji utakapokuwa kipimo cha kwanza. Wananchi hawataona teknolojia kwenye karatasi. Wataiona kwenye magari yanayokusanya taka.
Wataiona kwenye ratiba. Wataiona kwenye mitaa, wataiona katika kasi ambayo taka zitaondolewa. Katika hatua nyingine, Chalamila amesisitiza utenganishaji wa taka tangu zinapotoka majumbani. Kila kaya imeelekezwa kuwa na angalau madumu mawili kwa ajili ya kutenganisha taka.
Pia, mpango umetaja kuwepo kwa kontena kwa kila kaya mbili na vifaa vya kuhifadhia taka katika maeneo ya umma na magari ya abiria. Hili ni badiliko muhimu la mtazamo. Kwa mfumo wa kawaida, mwananchi hutupa taka, mkusanyaji huja kuzoa, kisha taka hupelekwa dampo. Mfumo mpya unaanza kabla ya hapo.
Taka itenganishwe kwanza. Hapo ndipo thamani ya taka inaweza kuanza kuonekana. Taka zinazoweza kuchakatwa zinaweza kutenganishwa na taka nyingine, hivyo kuwezesha hatua zinazofuata za urejelezaji na uchakataji.
Kwa maneno mengine, Dar safi inaanzia ndani ya nyumba kabla haijafika barabarani. Katika mpango huu, dampo la Pugu linapata nafasi muhimu. Chalamila ametaka sekta binafsi kushirikishwa katika uchakataji wa taka ili kuzalisha bidhaa nyingine, zikiwemo mbolea na nishati. Hapa ndipo dhana ya taka kama rasilimali inapokuwa muhimu.
Hii ndiyo dhana ya uchumi wa mzunguko, ambapo kile kinachochukuliwa kuwa taka kinaweza kuingizwa tena katika mnyororo wa uzalishaji. Kwa hiyo, Pugu inaweza kuwa sehemu muhimu ya kupima kama Dar es Salaam itaweza kuhama kutoka mfumo wa “kusanya na tupa” kwenda kwenye mfumo wa “kusanya, tenga, chakata na tumia tena.”
Vile vile, mpango huo pia umehusisha vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Vijana hao wanatarajiwa kusaidia katika kampeni ya usafi na udhibiti wa utupaji wa taka hovyo. Hii inaongeza nguvu katika eneo ambalo limekuwa changamoto; utekelezaji wa sheria na ufuatiliaji wa tabia za wananchi.
Lakini, hapa pia kuna jambo moja la msingi. Mwananchi akitakiwa asitupe taka hovyo, lazima awe na mahali sahihi pa kutupa taka. Ndiyo maana uwepo wa ‘dustbin,’ makontena na ratiba nzuri ya ukusanyaji ni sehemu ya mfumo huo.
Mjadala wa taka hauishii kwenye usafi wa barabara, unagusa pia mifereji na njia za maji. Chalamila amesisitiza usafishaji na uboreshaji wa mifereji na mito pamoja na miundombinu ya maji taka.
Hii inaunganisha moja kwa moja suala la usafi na maandalizi ya jiji kukabiliana na mvua kubwa. Taka zinapoingia kwenye mifereji zinaweza kuzuia mtiririko wa maji. Mtiririko unapozuiwa, maji yanaweza kutafuta njia nyingine. Na hapo ndipo tatizo la taka linaweza kugeuka kuwa tatizo la mafuriko. Kwa hiyo, mto safi na mfereji safi ni sehemu ya usalama wa jiji.
Katika kuanza safari hiyo, mkoa umetangaza kampeni maalumu ya usafi inayotarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (Tanzania Editors Forum – TEF), Deodatus Balile, akizungumza kwenye mkutano huo amesisitiza kwamba, kampeni ya usafi inapaswa kuwa endelevu na isiwe ya msimu. Hii ni hoja inayogusa kiini cha tatizo.
Usafi wa Dar es Salaam haupaswi kutegemea uwepo wa kamera, viongozi au kampeni. Unapaswa kuwa utaratibu wa kawaida. Aidha, Miezi mitatu si muda mrefu katika ujenzi wa mfumo mpya wa huduma za jiji. Kwa hiyo, agizo la Chalamila kwa wakandarasi linaweka kipimo kinachoeleweka.
Mpango wa usafi pia unagusa upangaji wa wafanyabiashara katika maeneo rasmi. Chalamila amesema wafanyabiashara wanaofanya shughuli katika maeneo yasiyoruhusiwa wataelekezwa kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa kwa biashara.
Hii inaonyesha kwamba, usafi hauwezi kutenganishwa na mpangilio wa jiji. Barabara zikiwa na biashara zisizopangwa, njia za watembea kwa miguu zikizibwa na maeneo ya biashara yasiyokuwa na mfumo mzuri wa taka, kazi ya usafi huwa ngumu zaidi.
Mwisho wa yote, mafanikio ya mpango huu yatapimwa na kitu kimoja, ikiwa taka zitakusanywa kwa wakati, mifereji ikawa safi, makontena yakapatikana, utenganishaji ukaanza kufanyika, uchakataji ukaongezeka na utupaji holela ukapungua, wananchi wataona tofauti.
Hata hivyo, naamini mikakati hii iliyotangazwa na Chalamila itafanikiwa iwapo kila mwananchi kwenye jamii atatimiza wajibu wake, kama alivyosema Mkuu wa Mkoa, suala hili sio la Serikali peke yake, jamii inapaswa kushiriki kufanikisha kampeni hii muhimu ya kusafishaji jiji la Dar es Salaam na kurejesha hadhi yake.