Na Habib Miradji
SEPTEMBA 7, 2026 taifa letu liliondokewa na Muungwana nambari wani asiyetiliwa mashaka katika matendo yake. Huyu ni Marehemu Maalim Hafidh Ameir Hassan aliyekuwa Mume wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan Suluhu.
Aghalabu, watu hupenda kuandika sifa za waliotingisha kwa nyanja za siasa. Uchumi, ushujaa wa vita, wasanii na michezo. Lakini, kwangu namwona Marehemu Mzee Hafidh Ameir ni shujaa kama wengine kwa matendo bora aliyeishi wakati wa uhai na mfano wa kuigwa.
Shabani Robert aliwahi kuandika “Hawafi wafao katika matendo bora kwa sababu majina na sifa zao hazisahauliki na wala kifo cha mwili hakikomeshi maisha yao”. Marehemu Mzee Hafidh Ameir ni Mwalimu anayetufundisha kuishi maisha ya uadilifu na asiyependa makuu.
Pamoja na utandawazi, Marehemu Mzee Hafidh Ameir aliridhika na kila alichojaaliwa, abadani hajatajwa hata kwa uzushi kuwa kutumia madaraka ya wengine kujinufaisha au kufuja mali za umma. Huu ni ucha mungu wa hali ya juu ambao tumefundishwa na Mzee huyu.
Tuna lukuki ya watu ambao jamaa zao wakiwa na Madaraka SerikalinI hutumia msemo wa kiarabu “Mbwa wa mfalme naye ni mfalme,” kutisha watu walio chini na mamlaka ili kujipatia mali au na hadhi. Hakuwa Jirani na matajiri ili kuchochea rushwa, aliogopa dhulma.
Mzee wetu hakutaka kutoa shinikizo kwa Mkewe Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya kazi zake za Urais. Hakuwa na makuu na hata kutumia Urais wa Dkt. Samia umjengee kufahamika kila pembe ya dunia. Itoshe kusema Marehemu Maalim Hafidh aliridhika na alichojaaliwa.
Miaka aliyoishi hapa duniani kama Binaadamu, alitumia maisha yake katika siasa na dini na taaluma ya Kilimo na Ualimu kuwalea na kutengeneza matarajio ya watu mbalimbali, bila shaka kazi aliyoianza lazima iendelezwe na wengine kwa kupokezana kwa zamu kama mwenge uliowashwa. Lazima tuenzi uadilifu wake.
Kuna mafunzo mengi tumeyapata kwa Marehemu Maalim Hafidh kwa jamii waipitia kwake aliwafundisha watu kujipatia Riziki kwa njia ya kilimo na kupambana na ujinga na umaskini. Itoshe kilimo cha minazi alichosomea Malaysia kimeletea mapinduzi Tanzania visiwani.
Kwangu, Marehemu Maalim Hafidh ni shujaa na fahari kwa nchi yetu. Namfananisha na baadhi ya watu maisha yao waliyapoteza katika elimu, uvumbuzi na matendo mengine ya thamani, jina lake linapaswa kuwa kwenye orodha ya wazalendo Daraja la juu nchini.
Marehemu Maalim Mzee Hafidh kama Mkuu wa familia alisimama kwenye mstari wa Uadilifu na kustahili jina la Muungwana nambari wani. Nchi mbalimbali duniani zinapaswa kujifunza kutoka kwa namna bora ya kuishi na Mamlaka bila ubadhirifu.
Kutokana na utumishi wake kwa umma Maalimu Hafidh alikuwa mfuasi mzuri wa falsafa za Marehemu Mahatma Ghandi wa India aliyedhamiria kuwafanya wahindi wenzake wawe matajiri kwanza na viongozi wao wawe watu wa mwisho kupata utajiri.
Maalim Hafidh amekwepa kikombe cha matajiri kuhaha pembe ya dunia ukwasi wao kutoa zawadi na kamisheni na rushwa kwa viongozi na wanasiasa, alikwepa mitego hii yenye vishawishi kwa ujasiri mkubwa Familia ya Marehemu imepoteza memba wake muhimu sana.
Viongozi wetu wa sasa wanamiliki mali na majumba yenye thamani usiolingana na mchango na umri wao katika utumishi wa umma. Viwanda na mashirika ambayo viongozi wetu ni wanahisa, wafanyakazi wake wanaishi katika hali za kukatisha tamaa hushindwa hata mlo mmoja tu japo vinatengeneza faida na hawana utetezi wa dhati.
Kizazi hiki cha Marehemu Maalim Hafidh ni mmoja wa wafuasi bora marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Abeid Aman Karume kuitumia kijamii na kuliondoa taifa katika hali ya unyonge na kulifanya taifa la wenye nguvu ni shujaa wa kukumbukwa.
Najua katika zama hizi za sasa, asasi ya Siasa inatumika kujilimbikizia mali kufuja mali za umma na raslimali kujitajirisha bila Wazee wetu kama marehemu Hafidh wanaona eti wamekunywa maji ya bendera, tutamwenzi kuwa amefariki na matendo bora ya kupigania uhuru wa taifa, kusaidia watu wenye shida wanaodhulumiwa na kudhalilishwa bila shaka kifo ni kitukufu kwake.
Inna Lilahi wa Inna Ilahi Rajoooni