Na Mwandishi Wetu
NIMEMSIKILIZA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Heche akiponda shughuli za michezo nchini na kazi za sanaa.
Kwanza, kabla sijasahau niseme kama huu ndio mtazamo, fikra na akili za viongozi wa upinzani, basi demokrasia ya nchi hii ina safari ndefu!!
Demokrasia ina safari ndefu kwa sababu vyama hivi badala ya kuwa ‘pinga pinga’ vilipaswa kuwa vyama mbadala vyenye hoja mbadala katika kuwaendeleza wananchi.
Ni akili ndogo ya kutaka kuaminishana eti kujadili mambo ya Simba na Yanga na Sanaa na Tamasha kama miaka 30 ya Bongo Fleva ni kujipumbaza.
Hii ni akili ndogo isiyopaswa hata kuongoza Chadema ngazi ya shina. Heche amejidhihirisha kuwa kiongozi lopolopo, mfokaji bila hoja.
Anachopaswa kujua ni kwamba, sekta anayoiponda ndiyo sekta inayokua kwa kasi hapa nchini na duniani na ndiyo inayoajiri vijana wengi na inayochangia kutoa matajiri wengi moja kwa moja au kupitia namna mbalimbali.
Forbes imeongeza Mabilionea 22 wapya wanaotokana na sekta za sanaa na michezo kati ya mwaka jana na juzi pekee!
Ni kiongozi asiyejielewa ndiye anaweza kusema eti Simba (1936) na Yanga (1935) zinatumika kupumbaza watu. Klabu hizi zimekuwepo hata kabla ya uhuru wala hata kabla CCM wala Chadema hawajazaliwa. Chadema hawajui hili?
Zina mchango wake usiomithilika katika jamii na kamwe zisihusishwe na ujinga wa Heche. Kwamba, kila mtu aache kuendelea na masuala yake ya kijamii ikiwemo kushabikia au kushiriki michezo eti ajadili na kuwaza Katiba mpya?
Yani yeye anavyolala na kuamka kwenye siasa kwa sababu kaajiriwa kuwa mwanasiasa, ndio kila mtu aache kazi zote awe mwanasiasa? Ujinga mtupu!
Simba na Yanga zipo hata kwenye dunia iliyoendelea; hazipo Spain, Ufaransa, Marekani, Uingereza nk? Timu za michezo za nchi hizo zenye demokrasia ya juu kwa akili hii finyu ya Heche nazo zinatumika kule Laliga, NBA, EPL, League 1 kuwapumbaza watu? Huu ni ujinga wa fikra.
Katika kuthibitisha Chadema wakichukua nchi kila kitu cha ubunifu kitapotea nchini, kiongozi wa ngazi ya juu chama hicho anaumizwa hadi na Matamasha makubwa ya muziki kwa madai kwamba yanazuia watu kuhoji Katiba mpya!
Je, kwa mawazo haya finyu, huyu anafaa kuwa hata kiongozi wa shina? Kwa hiyo anataka kutuambia ile ‘Samba Carnival’ kule Brazil ni Tamasha la kuzuia watu wasijadili Katiba?
Sasa hivi wasanii wakongwe Usher Raymond na Snoop Dogg Doggy wa Marekani na nimeangalia hata mkongwe Sir Elton John wako kwenye matamasha mbalimbali wakizunguka sehemu mbalimbali za dunia, nao wanazuia watu huko kwao kujadili Katiba mpya?
Hawa vijana wanaohaha kujiajiri kupitia ubunifu na vipaji vyao wameikosea nini Chadema? Ndio wanaozuia Katiba mpya anayoona Heche ndio ajenda muhimu kwa Watanzania?
Kwani l, mwaka 2014 Chadema na wenzao walipokacha mwishoni kabisa mchakato wa Katiba mpya na Kuunda UKAWA hawa ‘Bongo Flavour’ nao walikuwepo Bungeni? Ndio waliozuia Katiba mpya isipatikane na kuanza kutumika mwaka 2015? Jibu ni hapana.
Sio kila Mtanzania lazima ajadili siasa au masuala ya kiharakati kama Katiba mpya au wote tuzungumze wanayozungumza Chadema! saa 24! Ni mtazamo tu wa kifikra. Tuheshemiane!
Kila mtu ana uhuru wa fikra na kufanya kazi yoyote halali nchini na si kupangiwa na Chadema.
Kama ni sera ya Chadema kufuta michezo nchini na shughuli zote za sanaa kwa hoja hii ya kijinga kuwa zinapumbaza wananchi, wasubiri zamu yao ikija na akili kama hizi ili wafute yote hayo ili wakati wa utawala wao watanzania wote wajadili siasa tuuuu saa 24 na waajiriwe na siasa tu.
Lakini, siishawishi Serikali ya sasa kusikiliza hata kwa sekunde ujinga huu wa Heche na wenzake na kamwe isiufanyie kazi. Haitatokea labda tusubiri Serikali yao ya Chadema watulazimishe nchi nzima tulale na kuamka tukijadili siasa. Haiwezekani!