Na Iddy Mkwama
SEKTA ya uhifadhi na utalii nchini Tanzania inaendelea kuchukua nafasi muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa. Kwa miaka mingi, hifadhi za Taifa zimekuwa zikijulikana zaidi kama maeneo ya kulinda wanyamapori, misitu, mazingira na urithi wa asili.
Hata hivyo, mwelekeo mpya unaojengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) unaonesha kuwa uhifadhi unaweza kuwa zaidi ya jukumu la kimazingira; unaweza kuwa injini kubwa ya uchumi na ustawi wa jamii.
Mikakati inayotekelezwa na Serikali kupitia TANAPA inaonesha dhamira ya kutumia rasilimali za asili zilizopo nchini kama mtaji wa kiuchumi unaoweza kuzalisha mapato, kutoa ajira, kuvutia watalii na kufungua fursa mpya za uwekezaji.
Katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2026, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa aliweka bayana mafanikio na mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali za hifadhi.

Kilichoonekana katika maelezo hayo ni mabadiliko ya namna uhifadhi unavyotazamwa, kutoka katika mtazamo wa kulinda rasilimali pekee kwenda katika matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Moja ya vikwazo vinavyoweza kuathiri ukuaji wa utalii ni changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya vivutio. Hifadhi inaweza kuwa na vivutio vya kipekee duniani, lakini ikiwa watalii wanapata ugumu wa kufika huko, uwezo wake wa kuchangia uchumi unabaki kuwa mdogo.
Ndiyo maana, uwekezaji katika miundombinu ya usafiri una umuhimu mkubwa katika mkakati wa kukuza utalii.
Kwa mujibu wa TANAPA, miradi ya kimkakati ya ujenzi wa viwanja vinne vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi na Ruaha, ambako Ruaha itakuwa na viwanja viwili, pamoja na uwekezaji wa Serikali katika reli ya kisasa ya SGR na uimarishaji wa barabara zinazounganisha maeneo ya hifadhi, imeongeza urahisi wa kufikika kwa hifadhi hizo.
Hatua hii ina maana kubwa kiuchumi. Kadiri maeneo ya utalii yanavyofikika kwa urahisi, ndivyo uwezekano wa kuvutia watalii wengi zaidi unavyoongezeka.
Kwa mtalii wa Kimataifa mwenye muda mfupi wa kutembelea Tanzania, upatikanaji wa usafiri wa haraka na wa uhakika unaweza kuwa sababu muhimu katika kufanya uamuzi wa kutembelea hifadhi moja au nyingine.
Vilevile, miundombinu bora inaweza kuchochea uwekezaji katika hoteli, kambi za kitalii, huduma za usafiri, migahawa na biashara nyingine zinazohusiana na utalii.
Hii inaonesha kuwa uwekezaji katika miundombinu ya utalii hauishii katika kuboresha safari za watalii, bali unaweza kuwa kichocheo cha shughuli nyingi za kiuchumi zinazozunguka maeneo hayo.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa uhifadhi hauonekani kama shughuli inayowanufaisha wageni pekee, wakati jamii zinazozunguka maeneo hayo zikikosa fursa za kiuchumi.

Katika eneo hili, TANAPA inaeleza kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa shule, mabweni, zahanati, vituo vya polisi, visima na mabwawa ya maji. Pia, kuna uwekezaji katika viwanda vidogo vya kukamua mafuta ya alizeti na kusindika asali.
Huu ni mwelekeo muhimu kwa sababu maendeleo ya jamii yanapaswa kuwa sehemu ya mafanikio ya uhifadhi. Wananchi wanapopata huduma za kijamii, miundombinu na fursa za kiuchumi, wana nafasi kubwa zaidi ya kuona umuhimu wa kulinda rasilimali zinazowazunguka.
Kwa upande mwingine, uwekezaji katika viwanda vidogo unaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wananchi, kufungua masoko na kuongeza kipato cha kaya.
TANAPA pia imeeleza kuwa, inaendelea kuwawezesha wananchi kupitia benki za jamii za COCOBA, ambazo zinatoa mikopo kwa wananchi ili kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi. Uwezeshaji huo unalenga kuwasaidia wananchi kupata ajira, kufungua biashara na kuongeza kipato.
Vitendo vya ujangili, uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ni changamoto zinazohitaji mbinu madhubuti za ulinzi na ufuatiliaji. Katika kukabiliana na changamoto hizo, TANAPA imeeleza kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika doria, ufuatiliaji wa wanyamapori na kudhibiti ujangili.

Pia, wananchi wamewezeshwa kutoa taarifa kuhusu matukio yanayohusisha wanyamapori wakali na waharibifu kupitia namba maalumu za mawasiliano zilizowekwa katika kanda mbalimbali za shirika hilo.
Mkakati huu unaonesha umuhimu wa kuunganisha teknolojia na ushirikiano wa jamii katika kulinda rasilimali za Taifa. Teknolojia inaweza kusaidia kuboresha ufuatiliaji, kuongeza ufanisi wa doria na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusu usalama wa wanyamapori.
Katika hatua nyingine, TANAPA imepanua wigo wa vivutio vya utalii kwa kuwekeza katika uwanja wa gofu uliopo Fort Ikoma, pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Huu ni uwekezaji unaolenga kuunganisha utalii wa wanyamapori na michezo, hasa mchezo wa gofu ambao unaweza kuvutia watalii kutoka masoko mbalimbali ya Kimataifa.
Kwa kawaida, Tanzania imekuwa ikitambulika zaidi kupitia utalii wa kuona wanyamapori, mandhari ya asili na mapori makubwa yenye sifa ya kipekee. Lakini, kuingiza michezo katika bidhaa za utalii kunafungua nafasi ya kutengeneza vifurushi vipya vinavyoweza kuwavutia wageni wenye mahitaji na maslahi tofauti.
Uwanja huo unatarajiwa kuvutia wapenzi wa gofu na watalii wa hadhi ya juu, sambamba na kuongeza fursa za uwekezaji na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii wa gofu duniani.

Mkakati huo unaweza kusaidia kuongeza muda ambao watalii wanatumia nchini, jambo linaloweza kuongeza matumizi yao katika hoteli, safiri na huduma nyingine za utalii.
Kwa muda mrefu, sehemu kubwa ya utalii wa Tanzania imekuwa ikihusishwa na maeneo maarufu ya Kaskazini mwa nchi, mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii wa kukuza utalii Kusini na Magharibi mwa Tanzania unaonesha dhamira ya kupanua wigo wa vivutio vinavyotangazwa na kutembelewa.
Maeneo yanayolengwa ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha, Kitulo, Katavi, Gombe, Milima ya Mahale, Milima ya Udzungwa na Rubondo. Mkakati huu ni muhimu katika kupunguza utegemezi wa maeneo machache ya utalii na kusambaza fursa za kiuchumi katika maeneo mengi zaidi ya nchi.
Kwa mtazamo wa maendeleo, utalii unapopanuka kijiografia, unaweza kuchochea uwekezaji katika maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na shughuli nyingi za kitalii. Hali hiyo inaweza kuongeza mahitaji ya huduma za usafiri, malazi, chakula, bidhaa za ndani na ajira kwa wananchi.
Aidha, mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi imara na shindani.
Katika kutumia fursa zinazotokana na mashindano ya AFCON, TANAPA kwa kushirikiana na wadau wa utalii imepanga kuandaa vifurushi maalumu vya utalii kwa mashabiki wa soka watakaotembelea Tanzania.
Vifurushi hivyo vitawawezesha mashabiki kutembelea Hifadhi za Taifa za Serengeti, Nyerere, Saadani, Mikumi, Tarangire, Arusha na Manyara katika siku ambazo hawatakuwa viwanjani kufuatilia mechi. Huu ni mkakati wenye umuhimu mkubwa katika kutangaza vivutio vya Tanzania kwa watu kutoka mataifa mbalimbali.
Badala ya wageni kuja nchini kwa ajili ya kushiriki au kutazama mashindano ya michezo pekee, wanaweza kutumia nafasi hiyo kutembelea maeneo ya utalii na kujifunza zaidi kuhusu urithi wa asili wa Tanzania.

Hii ni fursa ya kuongeza matumizi ya wageni ndani ya nchi na kuingiza fedha katika sekta mbalimbali. AFCON inaweza kuwa jukwaa la kuitangaza Tanzania zaidi ya mipaka yake ya kawaida ya michezo na kuifanya nchi kuwa kivutio cha utalii kwa wageni wanaotembelea Afrika.
Mkakati mwingine wenye mwelekeo wa kupanua bidhaa za utalii ni kuanzishwa kwa utalii wa majini katika Ziwa Victoria. Kwa mujibu wa TANAPA, mpango huo unalenga kuunganisha maeneo ya Serengeti kupitia Ghuba ya Speke, Kisiwa cha Saanane, Kisiwa cha Rubondo na Burigi-Chato.
Huu ni mkakati unaoweza kuongeza thamani ya Ziwa Victoria katika sekta ya utalii na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa mikoa inayolizunguka. Utalii wa majini unaweza kusaidia kupanua shughuli za kitalii na kuwapa wageni uzoefu tofauti na ule wa kawaida wa kutembelea hifadhi kwa magari.
Pia, unaweza kuchochea uwekezaji katika usafiri wa majini, huduma za malazi, biashara ndogondogo na huduma nyingine zinazohitajika na watalii. TANAPA pia imeeleza mkakati wa kujenga barabara ya Kilomita 6.69 kwa kiwango cha lami kutoka lango kuu la Hifadhi ya Taifa Manyara hadi Minjingu.
Ingawa inaweza kuonekana kuwa mradi wa barabara wa umbali mfupi, umuhimu wake unapaswa kutazamwa katika muktadha wa kuboresha huduma na kurahisisha shughuli za utalii. Barabara bora zinaweza kupunguza changamoto za usafiri, kuboresha uzoefu wa wageni na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika maeneo ya utalii.
Aidha, miundombinu hiyo inaweza kunufaisha wananchi na biashara zinazofanya shughuli zao katika maeneo yanayozunguka hifadhi. Mikakati iliyowekwa wazi na TANAPA inaonesha kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kutumia urithi wake wa asili kujenga uchumi imara na shindani.
Kuanzia ujenzi wa viwanja vya ndege, SGR, maboresho ya barabara, matumizi ya teknolojia katika kudhibiti ujangili, uwanja wa gofu Serengeti, utalii wa majini Ziwa Victoria hadi vifurushi maalumu vya AFCON, hatua hizo zinaonesha jitihada za kupanua wigo wa utalii na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa.
Kwa Tanzania, ujumbe mkuu ni kwamba wanyamapori, misitu, maziwa, milima na mandhari ya asili si urithi wa kutunzwa kwa ajili ya kizazi cha sasa pekee, bali pia ni mtaji wa kiuchumi unaoweza kujenga maisha bora kwa vizazi vijavyo.