Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Komredi Mbeto Khamis Mbeto ameridhia kampeni ya ‘Baba Hatukudai Vijana’ inayo akisi kazi kubwa za maendeleo zilizotekelezwa na zinazotekelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza Ofisi Kuu CCM, Kisiwandui ambako vijana wanaoratibu kampeni hiyo ambao ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu UVCCM Taifa na wa Baraza Kuu Wilaya, walifika ofisini kwake kujitambulisha na kuomba ridhaa ya chama, Mwenezi Mbeto alisema kuwa anaridhia uwepo wa kampeni hiyo ambayo inaeleza utekelezaji wa Rais Dkt. Mwinyi katika kuwahudumia wananchi waliomchagua.
“Nabariki slogan (kaulimbiu) yenu ya ‘Baba hatukudai Vijana’, ni kweli Baba hatumdai kwani ndani ya miaka sita, mitano ya awali na mmoja wa sasa amefanyakazi kubwa” alisema Komredi Mbeto.
Alibainisha kuwa ili uchumi wowote ulimwenguni hujengwa kwa miundombinu imara na Zanzibar ina wastani wa barabara zenye kilometa 1,380 na hadi sasa zaidi ya kilometa 1,000 zimejengwa kwa lami.
“Hatumdai, kuna barabara kila sehemu, daraja la Uzi na barabara za juu (Flyover) katika maeneo mbalimbali leo zimeibadili Zanzibar” alisema na kuongeza kuwa katika afya amefanya mambo mengi makubwa.
Alibainisha kuwa Rais Dkt. Mwinyi amejenga hospitali za kisasa zenye vifaa tiba vyote muhimu kila wilaya na za mikoa na sasa vinajengwa vituo vya afya takribani 120 Zanzibar nzima.
Kwenye elimu amejenga shule zenye majengo ya ghorofa tatu (3G Plus) na kumaliza changamoto ya watoto kusoma kwa awamu mbili hadi tatu kwa siku na bado shule 61 za kisasa zinajengwa na uchumi wa buluu umeimarishwa.
“Serikali imewakopesha wavuvi boti za uvuvi, kumejengwa masoko ya samaki na Dago za wavuvi” alisema Mbeto huku akitaja masoko mapya ya kisasa ya Kimataifa yaliyojengwa sehemu mbalimbali hivyo kuwaondoa wajasiriamali hao pembezoni mwa barabara na sehemu zingine zisizo na stara.
“Ujenzi wa masoko mengine unaendelea sanjari na mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wajasiriamali hao na kuboresha huduma za jamii kwa nyongeza ya mishahara na posho mbalimbali,” alisema Mwenezi huyo.
Pia, viwango vya pensheni jamii na kwa wastaafu vimeongezwa ili kuendana na gharama halisi za maisha na kwa mantiki hiyo mwenezi hiyo anakubaliana na vijana hao kuwa Baba hadaiwi.