Na Mwandishi Wetu
MAPEMA mwaka huu, Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization-WMO), Prof.Celeste Saulo aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kusimamia vyema utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Pongezi hizo zilitolewa jijini Geneva, Uswisi wakati wa kikao cha pembezoni mwa kikao cha 70 cha Kamati Kuu Tendaji ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Seventieth Session of the Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC (70th IPCC Bureau).
Prof. Celeste Saulo alitoa pongezi hizo kwa Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la IPCC.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwenu. Sisi kama WMO tuko tayari kuendelea kushirikiana ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na taasisi nyingine zilizopiga hatua zaidi ili kubadilishana ujuzi zaidi,” alisema Prof. Celeste Saulo.
Kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Dkt. Chang’a alirejea kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa WMO, huku akiweka wazi kwamba, nchi mbalimbali zimevutiwa na utendaji wa TMA ambapo wanahitaji msaada wa mafunzo ili kuboresha utoaji wao wa taarifa.
Hata hivyo, pomoja na kuelezea mchango wa vyombo vya habari katika kufikia malengo hayo na kutajwa kuwa moja ya nchi za mfano kwenye utoaji wa taarifa za hali ya hewa, anasema Serikali imeisaidia Mamlaka hiyo vifaa vya kisasa ambavyo vinawasaidia kutoa taarifa za uhakika na mara kwa mara, huku akiweka wazi mkakati wa kuboresha zaidi utoaji taarifa.
Moja ya mkakati huo, ni kuweka nguvu kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano na kwamba tayari watalaamu wao wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi kwa ufanisi ikizingatiwa, taarifa sahihi za hali ya hewa si anasa, bali ni hitaji muhimu kwa usalama wa maisha ya watu, uchumi na maendeleo ya Taifa.
Hapa ndipo umuhimu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) unapojitokeza, kupitia jukumu lake la kufuatilia hali ya anga, kutoa utabiri na kuwawezesha wananchi pamoja na taasisi mbalimbali kufanya maamuzi kwa wakati.
Kwa maana hiyo, kwa TMA kutajwa kuwa miongoni mwa Mamlaka zinazotoa taarifa kwa wananchi kwa wakati, hatua hiyo inatoa fursa ya kutathmini umuhimu wa huduma zake, namna taarifa zinavyowafikia watumiaji na mchango wake katika kujenga jamii inayojipanga kukabiliana na athari za hali mbaya ya hewa.
Uongozi katika utoaji wa taarifa hauishii katika kutoa matangazo mengi; unajengwa na usahihi wa taarifa, muda wa kuzifikisha kwa wananchi, lugha inayoeleweka, upatikanaji kwa makundi mbalimbali na uwezo wa taarifa hizo kusaidia watu kuchukua hatua zinazofaa.
TMA na mageuzi katika utoaji wa taarifa kwa umma
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni taasisi yenye jukumu muhimu katika kuisaidia Tanzania kuelewa mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake. Kupitia utabiri, tahadhari na takwimu za hali ya hewa, mamlaka hiyo inatoa taarifa zinazoweza kutumiwa na wananchi, Serikali na sekta mbalimbali kupanga shughuli zao.
Huduma zake zinajumuisha utabiri wa kila siku, utabiri wa siku tano na siku kumi, mwelekeo wa hali ya hewa wa mwezi na msimu, pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa. Taarifa hizo hupatikana kupitia tovuti ya mamlaka hiyo na njia nyingine za usambazaji.
Wigo huo wa huduma unaonesha kwamba, TMA si taasisi ya kutangaza tu uwezekano wa mvua au jua. Ni chanzo muhimu cha taarifa zinazoweza kusaidia wananchi kupanga shughuli zao na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Ubora wa mamlaka ya hali ya hewa haupimwi kwa uwezo wake wa kutabiri tu, bali pia kwa jinsi inavyowafikishia wananchi taarifa kabla hatari haijatokea. Tahadhari ya mvua kubwa, upepo mkali, mawimbi makubwa au matukio mengine hatarishi inaweza kusaidia wananchi kuchukua hatua za kujilinda, kuimarisha usalama wa mali zao na kuepuka maeneo yanayoweza kuwa hatarini.
Kwa mfano, wakazi wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko wanaweza kutumia taarifa za mapema kujiandaa, huku wavuvi na wasafiri wa majini wakihitaji taarifa za hali ya bahari na maziwa kabla ya kuanza safari.
Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 inaweka msingi wa utoaji wa utabiri na tahadhari kwa umma. Sheria hiyo pia inaelekeza vyombo vya habari kusambaza kwa wakati tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazoweza kuhatarisha maisha na mali.
Hii inaonesha kwamba, utoaji wa taarifa za hali ya hewa ni sehemu ya mfumo mpana wa usalama wa wananchi, unaohitaji ushirikiano kati ya TMA, vyombo vya habari, mamlaka za Serikali na jamii.
Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kutafsiri taarifa za kitaalamu na kuzifikisha kwa wananchi kwa lugha rahisi, bila kupotosha maana yake.
Taarifa za ukaguzi wa utendaji kuhusu usimamizi wa huduma za hali ya hewa nchini zimejadili matumizi ya njia mbalimbali za habari kusambaza utabiri na taarifa za hali ya hewa, pamoja na changamoto zinazohusu ufanisi wa usambazaji na matumizi ya taarifa hizo.
Hapa ndipo umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya TMA na wahariri, waandishi wa habari na watangazaji unapojitokeza. Taarifa za hali ya hewa zinapowasilishwa kwa wakati, kwa lugha inayoeleweka na kwa maelezo ya athari zinazoweza kutokea, wananchi wana nafasi nzuri ya kuelewa hatari na kuchukua hatua.
TMA na mchango katika sekta ya kilimo
Kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotegemea hali ya hewa. Mabadiliko ya wakati wa kuanza kwa mvua, kiasi cha mvua kinachotarajiwa na muda wa ukame yanaweza kuathiri uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.
Kupitia taarifa za hali ya hewa na ushauri unaohusiana na kilimo, TMA huwapatia wakulima na wadau wengine taarifa zinazoweza kuwasaidia kupanga wakati wa kupanda, kufanya maandalizi ya mashamba na kutumia maji kwa ufanisi.
Umuhimu wa taarifa hizo unaongezeka katika kipindi ambacho mabadiliko ya tabianchi yanaweza kufanya misimu ya mvua kuwa na changamoto kubwa zaidi kwa shughuli za kilimo.
Mkulima anayepata taarifa mapema ana nafasi nzuri ya kufanya maandalizi kuliko anayesubiri mvua ianze ndipo aanze kupanga shughuli zake. Ili manufaa haya yafike kwa wakulima wengi zaidi, ni muhimu taarifa ziambatane na ushauri unaoeleweka kwa lugha rahisi na unaozingatia tofauti za hali ya hewa kati ya maeneo mbalimbali nchini.
Teknolojia na upatikanaji wa taarifa
Katika zama za kidijitali, wananchi wanahitaji kupata taarifa kwa urahisi, bila vikwazo vinavyoweza kuchelewesha maamuzi muhimu. TMA imeboresha njia za upatikanaji wa taarifa kupitia tovuti yake, ikiwemo utabiri, tahadhari, video na machapisho yanayohusu hali ya hewa.
Taarifa hizi zinajumuisha mwelekeo wa hali ya hewa kwa vipindi tofauti, jambo linalowawezesha watumiaji kuchagua taarifa inayohusiana na mahitaji yao.
Hii ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa umma. Hata hivyo, ubora wa mifumo ya kidijitali unapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha taarifa zinawafikia pia wananchi wasio na intaneti ya uhakika, wasiokuwa na simu janja au wanaoishi katika maeneo ya mbali.
Redio, televisheni, magazeti, simu na mifumo ya mawasiliano ya jamii vinaweza kusaidia kuziba pengo hilo. Taarifa muhimu hazipaswi kubaki kwa wananchi wenye uwezo wa kutumia teknolojia
Kukabiliana na maafa na mabadiliko ya tabianchi
Mabadiliko ya tabianchi yameongeza umuhimu wa taarifa zinazowezesha jamii kujiandaa mapema. Katika mazingira hayo, utabiri wa hali ya hewa ni nyenzo ya kuimarisha maandalizi na kupunguza madhara, ingawa hauwezi kuondoa hatari zote.
TMA hushirikisha wadau wa sekta mbalimbali katika kujadili athari na ushauri wa hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu. Ushirikiano huu una umuhimu katika kuunganisha taarifa za kitaalamu na mahitaji halisi ya watumiaji.
Taarifa za mvua kubwa zinaweza kusaidia mamlaka za miji kufanya maandalizi ya mifereji ya maji, kutambua maeneo hatarishi na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mafuriko. Lakini taarifa hizo zitakuwa na manufaa makubwa zaidi pale zitakapofuatwa na hatua za maandalizi, utekelezaji wa tahadhari na ushirikiano wa wananchi.
Kwa maana hiyo, TMA ina jukumu muhimu katika kutoa utabiri na tahadhari zinazohitajika na wakulima, wavuvi, wasafiri, wafanyabiashara, taasisi za umma na wananchi kwa ujumla. Katika jamii inayokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, taarifa za hali ya hewa ni zaidi ya utabiri wa mvua au jua. Ni nyenzo ya kupanga maisha, kulinda mali, kupunguza madhara na kujenga Taifa lenye uwezo wa kujiandaa kwa hatari za kesho.