Na Mwandishi Wetu – WMTH
SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeeleza hatua iliyofikiwa katika kuimarisha miundombinu na huduma za mawasiliano nchini, ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa minara 758 iliyowezesha vijiji 1,400 kupata huduma za simu na intaneti na kunufaisha zaidi ya wananchi Milioni 8.5.
Mradi huo uligharimu Shilingi Bilioni 126, ambapo Shilingi Bilioni 55 zilitoka Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 71 kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Hayo yameelezwa Bungeni, Dodoma Agosti 14, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (mb) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu wakati akiwaslisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Mawasiliano (TTCL), Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).
Waziri Kairuki ameongeza kuwa, Serikali kupitia TTCL imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma hadi Kalemie nchini DRC kupitia Ziwa Tanganyika.
Mkongo huo wenye urefu wa Kilomita 183 unagharimu Dola za Marekani 11,568,429 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2027. Tayari malipo ya awali ya Dola 4,302,386.7 yamefanyika na dhamana ya mkataba ya Dola 7,265,862.3 imetolewa.
Kwa upande wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) hadi Juni 2026 imesajili jumla ya wakusanyaji na wachakataji 14,826, huku 7,131 kati yao wakisajiliwa katika kipindi hicho. Tume pia imepokea malalamiko 95 na kushughulikia 76, sawa na asilimia 80, pamoja na kutoa vibali 69 kati ya maombi 75 ya kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi.
Aidha, tathmini ya ubora wa huduma za minara 758 iliyofanyika Januari hadi Juni 2026 imeonesha kuwa watoa huduma wengi wamefikia na kuvuka viwango vilivyowekwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), huku huduma hizo zikiendelea kuchochea upatikanaji wa elimu, afya, biashara na huduma za Serikali Mtandao.