Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Mark Kihulla
Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo (WMA) umeweka wazi nia ya kuanza uhakiki wa vipimo vyote vinavyotumika kutoa huduma ya afya nchini ili kuhakikisha wagonjwa wanapa matibabu sahihi.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Mark Kihulla, alisema mbali na kulenga kulinds afya za watanzania, lakini ni katika kutekeleza sheria zinazowaongoza.
Alisema, WMA wana sheria ya vipimo Sura ya 340, pia wanaangalia sheria za Kimataifa na sheria za Kanda, ambapo sheria ya Afrika Mashariki inaelekeza taasisi zote zinazojihusisha na vipimo kufanya uhakiki wa vipimo vya biashara, afya, usalama na mazingira.
“Afya ndio kila kitu, tumeanza kwenye sekta ya afya, ingawa hatujaanza kwa kiwango kikubwa, lakini tunatarajia kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha vipimo vyote kwenye sekta ya afya vinafanyiwa uhakiki,” alisema Kihulla.
Aliendelea kusema, ni hatari kutofanya uhakiki kwenye vipimo vinavyotumika kwenye huduma za afya, ambapo lengo la WMA ni kuhakikisha kama mtu amepima uzito, uwe sahihi ili daktari aweze kutoa dozi inayoendana na uzito wa mgonjwa.
“Isije ikaonyesha presha yako ni kubwa, kumbe hauna presha, kwahiyo tunafanya uhakiki ili kusaidia wenzetu wanaotoa dawa, pia tunataka kufanya uhakiki kwenye mashine za mionzi ili upigwe mionzi sahihi, usije ukapigwa mionzi mingi, unapona ugonjwa huu, kesho una ugonjwa mwingine,” alisema Mtendaji Mkuu huyo.