KONGAMANO la Pili la Kitaifa la Wanamipango 2026 limehitimishwa kwa kuweka msisitizo mpya katika hatua muhimu ya utekelezaji wa Dira 2050 ambao ni kuhakikisha mipango ya Taifa inabadilika kuwa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Akizungumza katika kilele cha kongamano hilo jijini Arusha, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wanamipango kusimamia kwa umakini miradi ya maendeleo ili mipango iliyowekwa iweze kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Mwigulu, amesisitiza umuhimu wa kuondokana na mtazamo kwamba Tanzania inaweza kuwa bora katika kupanga kuliko kutekeleza.
Ujumbe huo unaweka wazi kiini cha kongamano hilo lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango kwamba, Dira 2050 haihitaji mipango pekee bali inahitaji mifumo inayounganisha mipango, rasilimali, utekelezaji, ufuatiliaji na matokeo.
Kwa siku mbili, zaidi ya wataalamu 1,300, wakiwemo wanamipango, wachumi, watakwimu na wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, walijadili namna ya kuimarisha upangaji jumuishi, utekelezaji na maendeleo.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu pia amesisitiza nafasi ya sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira 2050, akitaka mazingira ya biashara na uwekezaji yaimarishwe ili sekta hiyo iwe mshirika na kutoa mchango wake katika kuleta maendeleo na ajira.
Kwa wananchi, maana ya mjadala huu ni rahisi: mipango bora inapaswa kuonekana katika huduma, fursa, ajira, uwekezaji na ustawi wa maisha.
Hivyo, ujumbe wa Arusha ni mmoja: Dira 2050 lazima itoke kwenye nyaraka, iingie kwenye utekelezaji na ionekane katika matokeo.