Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza hatua mpya za kuirejesha Dar es Salaam katika hali ya usafi huku akisisitiza, jukumu la kulisafisha jiji halitaachwa kwa Serikali pekee.
Alitaja makundi ambayo yatakuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huu ni pamoja na Wananchi, wafanyabiashara, wakandarasi, sekta binafsi na vyombo vya habari.
Chalamila alitoa kauli hiyo Septemba 17, 2026, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari, ambapo alikiri kwamba, jiji limekumbwa na changamoto ya uchafu na kusema, viongozi walikuwa wamejisahau kwa kipindi fulani katika kusimamia suala hilo.
“Tulisahau kwa muda, jambo ambalo limepelekea Mheshimiwa Rais kwa jicho lake kuona Dar es Salaam ni chafu. Tunakiri kwamba, Rais alichokiona kwetu hajatuonea,” alisema Chalamila.
Chalamila alisema, Mkoa umeamua kubadili mfumo wa ukusanyaji na uchakataji wa taka, kuongeza matumizi ya teknolojia na kuimarisha usimamizi wa sheria za usafi.
Pia, alisema wanataka kulishughulikia suala hilo kwa mfumo unaolenga kubadili tabia za wananchi pamoja na kuboresha uwezo wa mamlaka za usafi.
Katika mpango huo alisema, elimu kwa wananchi itakuwa sehemu muhimu, huku wataalamu wakitumika kutoa elimu kuhusu usafi na utenganishaji wa takataka, ambapo ametoa miezi mitatu kwa wakandarasi wa uzoaji taka kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kisasa na teknolojia inayokidhi mahitaji ya Dar es Salaam.
Alisema, lengo ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa takataka na kuwezesha usafi kufanyika hata nyakati za usiku, pia Mkoa umeweka mkazo katika kuwepo kwa mifumo bora ya kuondoa maji taka, sambamba na kuboresha miundombinu ya maji safi na maji taka.
Vile vile, Chalamila ameagiza kila kaya kuwa na madumu mawili kwa ajili ya kutenganisha takataka, ambapo mpango huo unalenga kuwezesha taka kutenganishwa tangu zinapozalishwa nyumbani kabla ya kupelekwa katika maeneo ya ukusanyaji.
“Kwa wale wakandarasi wote ambao wako ‘serious’ kufanya kazi katika jiji la Dar es Salaam, wanapaswa kuhakikisha wanatafuta vifaa vya kisasa hata kama sio kwa ukubwa, lakini vinavyoweza kusaidia,” alisema na kuongeza kuwa, usafi unapaswa kufanyika usiku.
Alisema, zoezi la usafi nyakati ambazo magari yanapita na hakuna utulivu, kunasababisha ukusanyaji taka usioridhisha, lakini kunaweza kusababisha ajali hivyo, utaratibu unapaswa kubadilika.
Katika hatua nyingine, Chalamila aliitaka sekta binafsi kuingia katika uchakataji wa takataka kwani zinaweza kutumika kama malighafi, kutengeneza bidhaa nyingine na hata kuzalisha nishati. “Kwa sasa tuwe na mpango wa kuanza kuchakata takataka ili ziweze kuzaa matunda mengine takataka kuwa gesi, takataka kuwa oil.”
Chalamila alisema, huu ni sehemu ya mkakati wa kupunguza utaratibu wa kutupa taka bila kuzichakata na tayari Mkoa umekuwa ukitafuta ushirikiano na wawekezaji binafsi katika miradi ya kuchakata taka katika eneo la Pugu, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuzalisha mbolea na gesi.