WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameanza ziara barani Asia kwa lengo, miongoni mwa mengine, la kukutana na kuvutia wawekezaji kuja Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa barabara za kimkakati kupitia mfumo wa Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Barabara za kimkakati ni zile zinazounganisha Tanzania na nchi jirani, bandari za Tanzania na maeneo yenye uzalishaji pamoja na masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia zinahusisha barabara zinazounganisha maeneo yenye shughuli za kibiashara, ikiwamo mikoa yenye kukuza sekta ya utalii.
Ziara hiyo inamfikisha Waziri Ulega nchini China na Korea Kusini, ambako baadhi ya wawekezaji kutoka nchi hizo tayari wameonyesha nia ya kuwekeza Tanzania.
Nchini China, Ulega tayari amekutana na baadhi ya wawekezaji na kujionea miradi mikubwa inayotekelezwa kwa kutumia mfumo wa PPP.
Kupitia PPP, Kampuni binafsi zinaweza kujenga barabara, madaraja na miundombinu mingine kwa makubaliano maalumu na Serikali.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, baada ya mwekezaji kurejesha gharama za uwekezaji pamoja na kupata faida iliyokubaliwa, miundombinu hiyo hubaki kuwa mali ya Serikali.
Nchini Korea Kusini, Ulega anatarajiwa kuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika Kongamano la Kimataifa la Miundombinu Duniani, linalotarajiwa kuanza leo jijini Seoul.
Kongamano hilo hukutanisha wadau muhimu katika sekta ya miundombinu na ujenzi, wakiwamo wawakilishi wa taasisi za kifedha, Serikali, wawekezaji na wataalamu kutoka sekta hiyo.
Ziara hiyo inalenga pia kuongeza fursa za ushirikiano wa kimkakati na kuvutia mitaji ya sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu itakayochochea biashara, usafirishaji, utalii na maendeleo ya uchumi nchini.