Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, amewataka watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujitathmini katika utendaji wao wa kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazolingana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miradi ya maendeleo.
Abdi ameyasema hayo wakati akiendelea na ziara ya kukagua uhai wa Chama na miradi ya maendeleo katika Kisiwa cha Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuwaondolea wananchi changamoto za muda mrefu, hivyo ni muhimu watendaji kuhakikisha miradi hiyo inatoa huduma iliyokusudiwa kwa ufanisi.
Amesema hali ya baadhi ya huduma kutotolewa kwa kiwango kinachotarajiwa inapaswa kuwafanya watendaji kujitathmini na kutafuta sababu za changamoto hizo badala ya kuwaacha wananchi wakiendelea kulalamika.
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji Tumbatu, Abdi amesema haileti mantiki Serikali kutumia fedha kujenga mradi wa maji kwa lengo la kuondoa tatizo la muda mrefu, lakini baada ya mradi kukamilika wananchi bado wakaendelea kukosa huduma ya uhakika.
“Wawakilishi wetu walipitisha bajeti na ukajengwa mradi huu, lakini nasikitika mradi huu bado unalalamikiwa kwamba maji yanatoka kwa awamu. Kwa nini iwe kwa awamu? Au wataalamu wetu hawakutushauri vizuri Serikali?,” amesema.
Amesema CCM haitaridhishwa na hali ya baadhi ya miradi mikubwa kutofanya kazi kwa ufanisi kutokana na changamoto za usimamizi, akisisitiza umuhimu wa wataalamu wenye sifa kusimamia huduma zinazohitaji utaalamu.
Aidha, Abdi amekosoa utaratibu wa kutumia askari katika kusimamia ufunguaji na ufungaji wa huduma za maji badala ya kuweka wataalamu wenye dhamana ya kusimamia huduma hiyo.
Amesema hatua hiyo si sahihi na kwamba Serikali inapaswa kuhakikisha wataalamu wanapewa nafasi ya kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia taaluma na utaalamu wao.
Katika hatua nyingine, Abdi amesema CCM tayari imetoa maelekezo kwa Waziri mwenye dhamana ya maji kuandaa kikao maalum kitakachowakutanisha wataalamu kutoka Wizara pamoja na wataalamu kutoka CCM, kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa haraka wa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Tumbatu na maeneo mengine ya Zanzibar.
Amesema kikao hicho kitasaidia kubaini chanzo cha changamoto hizo na kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika na kwa kiwango kinachostahili.
Abdi anaendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa CCM na kukutana na wanachama katika matawi na majimbo mbalimbali ya Zanzibar. Kwa sasa ziara hiyo imefika siku ya nne katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.