RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata elimu, ujuzi, ajira na fursa za kujiajiri ili kutumia uwezo na vipaji vyao katika kuchangia maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, 19 Septemba 2026, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Mafunzo, Elimu na Michezo cha Tanzania Youth Icon (TAYI), Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali kupitia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 inaendelea kuweka msisitizo katika elimu na mafunzo, utafiti na ubunifu, ajira, utamaduni na michezo kwa lengo la kukuza vipaji na kuongeza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza TAYI kwa kuwekeza katika maendeleo ya vijana, akieleza kuwa kituo hicho kitasaidia vijana kupata elimu, ujuzi, kukuza vipaji vya michezo na sanaa, pamoja na kuwaendeleza katika ubunifu na ujasiriamali.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amepokea hundi ya Shilingi Milioni 100 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ametoa tuzo mbalimbali ikiwemo kwa wajumbe wa Bodi ya TAYI kwa mchango wao katika maendeleo ya taasisi hiyo na kuwawezesha vijana, huku yeye mwenyewe akikabidhiwa tuzo maalum ya kutambua mchango wake katika maendeleo na uwezeshaji wa wananchi.