Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutekeleza matakwa ya Katiba ya Zanzibar kwa kumteua Makamu wa Kwanza wa Rais, huku chama hicho kikisema hatua hiyo imekamilisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kisiwandui kuhusu uteuzi huo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Hamisi, amesema CCM kinampongeza Rais kwa kutekeleza matakwa ya Katiba na pia kimepongeza Chama cha ACT-Wazalendo kwa kuwasilisha jina la mgombea wao kwa nafasi hiyo.
Mbeto amesema, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ina msingi wa kikatiba unaotaka uwepo wa nafasi za Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais.
Amesema, Ibara ya 39 ya Katiba inaeleza kuhusu uwepo wa nafasi hizo pamoja na majukumu yake, huku ikieleza utaratibu wa uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Mbeto amesema, ACT-Wazalendo kwa kuungana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sasa inapaswa kutekeleza majukumu yake ndani ya serikali kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazoanzisha na kuendesha Serikali hiyo.
“Kwa sisi kama Chama Cha Mapinduzi, kwanza tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutekeleza takwa la Katiba alilopewa,” amesema Mbeto.
Amesema, uteuzi huo umefanyika baada ya kuwepo kwa mchakato wa kisiasa na kikatiba kuhusu kujazwa kwa nafasi hiyo, akisisitiza kuwa sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekamilika katika muundo wake wa kiuongozi na kiutendaji.
Mbeto amesema, CCM inatarajia Makamu wa Kwanza wa Rais, pamoja na mawaziri watakaoteuliwa, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Ilani ya CCM ambayo chama hicho kilishinda kupitia uchaguzi, sambamba na Dira ya Taifa ya 2050 na miongozo mingine ya kitaifa.
Amesema, utekelezaji wa majukumu hayo unapaswa kulenga zaidi kuwahudumia wananchi na kuleta maendeleo kwa Zanzibar.
“Kwa sasa tunatarajia kusikia kauli za kujenga zaidi, kauli zinazolinda umoja na mshikamano, lakini pia kauli zinazochochea maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema.
Aidha, Katibu huyo amevitaka vyama vya siasa na wafuasi wake, hususan katika mitandao ya kijamii, kuepuka kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko miongoni mwa wananchi.
Amesema, pamoja na vyama vya siasa kuendelea kusimamia misingi na sera zao, hilo halipaswi kuathiri mshikamano unaohitajika katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Vyama vitabaki kama kawaida na tutaendelea kufanya shughuli zetu za kisiasa, lakini tuzingatie kwamba tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo inaunganisha Zanzibar,” amesema.
Mbeto amesema, CCM iko tayari kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akiwemo Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais pamoja na mawaziri na watendaji wengine wa serikali, ili kuhakikisha majukumu ya kuwatumikia wananchi yanatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema, hatua hiyo inalenga kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi na wananchi kutumia kipindi hiki kujenga mazingira yatakayoiwezesha Zanzibar kupiga hatua zaidi.