Bashungwa aagiza waliomshambulia Padri Kitima wapatikane

0

📌Polisi watakiwa kumtafuta aliyeandika mtandaoni: “Siku za Kitima zinahesabika”.

📌 Waliochapisha na kusambaza Waraka feki wa TEC watafutwe.

📌 Akemea vitendo vya uhalifu na wanaohusika

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amelaani vikali tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima.

Pia, ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumhoji mtu aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa “siku za Kitima zinahesabika”,pamoja na watu wote waliohusika na uhalifu huo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka, yule mtu aliye-tweet kwenye mitandao ya kijamii kwamba, ‘siku za Kitima zinahesabika’. Mtu huyu atafutwe haraka, ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, kwa watu wote watakaobainika kuhusika katika tukio hili.” amesema Bashungwa.

Bashungwa alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa viongozi wa dini nchini katika kudumisha amani, mshikamano wa kijamii, na maadili ya Taifa.

“Tunalaani vikali shambulio hilo la kinyama dhidi ya kiongozi wa Dini na tunamuombea Padre, Dkt. Charles Kitima uponaji wa haraka na urejeaji salama katika majukumu yake muhimu kwa taifa” alisema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta waliotengeneza na kusambaza waraka feki uliodaiwa kutolewa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), waraka ambao ulilenga kuchochea mgongano kati ya Kanisa na Serikali.

“Kumekuwepo na ‘Waraka feki’ uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukidaiwa ni waraka wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Maaskofu Tanzania kupitia taarifa yake kwa umma imekanusha kuwa waraka huo haukutolewa na TEC, na kuwataka wananchi, waumini na watu wote wenye mapenzi mema kupuuza kabisa waraka huo” lisema Bashungwa.

Ameeleza hayo, Mei 02, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaaga Watumishi wa umma waliostaafu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo alikumbusha kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao kupitia Vyombo vyake vya Usalama.

Bashungwa amewaelekeza Watendaji wote wa Wizara na vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wao kwa weledi, kwa kuzingatia sheria, ili kulinda amani na usalama wa nchi.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kuchukua hatua zinazositahili dhidi ya wahalifu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi yetu” alisisitiza Bashungwa.

Vilevile, Bashungwa amekemea vikali vitendo vyote vinavyochafua taswira ya taifa, vikiwemo vya kudhuru watu au kusambaza taarifa zenye kuchochea uhasama wa madhehebu ya kidini.

“Ni wakati muafaka sasa, Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kusimamia sheria zinazohusu mitandao ya kijamii ili kuhakikisha watu wote wanatii sheria bila shuruti na hivyo kuendelea kuwa na jamii yenye ustaarabu na kuheshimu utu wa kila mtanzania na hata mgeni” alisisitiza.

Amewahakikishia Watanzania kuwa nchi iko salama na kuwasihi kuendelea kutii sheria bila kushurutishwa, ili kudumisha hali ya amani, utulivu na usalama nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here