Johanesburg, AFRIKA KUSINI
RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amechaguliwa tena kuwa kiongozi wa chama cha ANC katika mkutano wa chama uliofanyika Johanesburg, Afrika Kusini.
Wakati matokeo yanatangazwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Khalema Motlanthe watu waliokuwepo kwenye chumba cha mkutano walipiga kelele za kushangilia.
Ramaphosa amekwepa changamoto ya uongozi wa chama chake, siku chache baada ya vuguvugu lililozuka kutaka kumuondoa madarakani kufuatia kashfa ambapo alishutumiwa kuwa alificha pesa katika shamba lake kashfa iliyopewa jina la Farmgate.
Ramaphosa aliingia madarakani mwaka 2018 baada ya kuchaguliwa kiongozi wa chama mwaka 2017 akiahidi kutokomeza rushwa na kurekebisha uchumi.
Lakini, mara alipotaka kuanza kampeni ya muhula wake wa pili, alipata mwito wa kutakiwa kujiuzulu baada ya jopo la ushauri kugundua ushahidi wa awali kuwa anaweza kuwa amefanya makosa.
Alikanusha kufanya kosa lolote na hajashtakiwa kwa tuhuma zozote za uhalifu.
Ramaphosa alikuwa mpatanishi mwandamizi wa ANC wakati wa mazungumzo yaliyopelekea kumalizika kwa amani kipindi cha ubaguzi wa rangi mwaka 1994, ambapo ilimwezesha Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini.