AICC yajipanga kuwa kiungo muhimu biashara ya utalii

0
MTENDAJI Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Ephraim Mafuru.

Na Mwandishi Wetu

MTENDAJI Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Ephraim Mafuru amesema kituo hicho kinajipanga kuhakikisha kinakuwa kiungo muhimu katika biashara ya utalii nchini. 

Mafuru ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, Septemba 14,2023 wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwa ni mwendelezo wa vikao kazi baina ya Taasisi na Mashirika ya umma ambayo yapo chini Ofisi ya Msajili wa Hazina, kuelezea mafanikio ya Taasisi hizo tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.

Mkurugenzi huyo alisema, Arusha ni kitovu cha utalii nchini, hivyo AICC inashiriki kikamilifu katika kuhakikisha wanafanikisha shughuli hizo ili kuimarisha mnyororo wa thamani na kuhakikisha wanaboresha huduma zao ili kuvutia wageni wengi zaidi wanaokuja kufanya mikutano yao. 

Alisema, kituo chake kinashiriki kwa kuwatangazia wageni wanaofika kwenye kituo chao fursa mbalimbali za utalii zilizopo nchini, ikizingatiwa kwamba wanapokea idadi kubwa ya wageni wanaokuja kwenye vituo vyao viwili; AICC na JNICC, huku akipongeza jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi kiuchumi na kuhamasisha Diplomasia ya Uchumi.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua nchi Kiuchumi, kwa upande wetu tunapata wageni wengi wanaokuja kufanya mikutano hapa nchini jambo ambalo linachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza Pato la Taifa,” alisema Mafuru huku akisisitiza kwamba, wanaweza kutoa nafasi ya kufanya mikutano kwa idadi ya watu tofauti kuanzia watu 10.

Alisema, kwa sasa wageni wanaipenda Tanzania na wanakuja Tanzania kwa wingi, na imekuwa chaguo muhimu na kuvutia mikutano mbalimbali ya Kimataifa, huku akiweka wazi kwamba, wanaweka mikakati ya kuongeza idadi ya mikutano kutoka mikutano 18 kwa mwaka hadi kufika 30 na ikibidi wavuke zaidi idadi hiyo. 

“Lengo letu ni kuhakikisha Diplopmasia ya Mikutano inaendelea kuwa nguzo muhimu katika Diplomasia ya Uchumi wa nchi yetu, kwani ndio sehemu pekee ambayo nchi inaweza kupata fedha nyingi za kigeni kupitia wageni wanaokuja nchini,” alisema Mafuru huku akitoa historia fupi ya kituo hicho ambacho kilianzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969 kwa agizo la Rais kupitia tangazo la Serikali namba 115, lililochapishwa 25 Agosti mwaka 1978. 

Mafuru alisema, kituo hicho kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania na kinafanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo walikabidhiwa miaka tisa iliyopita.

“Kituo hiki kinafanya kazi kibiashara, mbali na kusimamia kumbi mbalimbali za mikutano, tuna ofisi ambazo tunakodisha, tunaendesha Hospitali na tunamiliki nyumba za kupangisha kwa ajili ya kukiongezea kituo Mapato,” alisema Mafuru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here