Rais Samia aongoza maadhimisho ya siku ya sheria

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiongea na wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Na Faustine Kapama, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Sheria na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji mkubwa wa huduma za utoaji haki kwa wananchi unaoendelea.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini hapa, Rais Samia ameonyesha kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati ulioanza kutekelezwa toka mwaka 2015.

“Naipongeza sana Mahakama kwa maboresho mnayoendelea nayo toka mwaka 2015 pale mlipoamua kuandaa Mpango Mkakati wa Kwanza ambao umeleta mafanikio chanya,” alisema.

Dkt. Samia alitoa mfano kwa mwaka 2022 ambapo Mahakama ilifunga mwaka ikiwa na mashauri 64,001, yakasajiliwa mengine 244,292 katika ngazi zote, hivyo kufanya mwaka huo kuwa na mashauri 304, 293, lakini yaliyomalizika yalikuwa 253,495.

“Ni kazi kubwa sana imefanyika, hongereni sana. Nakubaliana nanyi kuongezeka kwa idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu toka 78 hadi 100 Agosti 2022 imekuwa chachu ya mafanikio hayo. Hili pia linachangiwa na dhamira ya dhati ya uongozi uliopo na Mahakimu wenyewe,” alisema.

Rais Samia alibainisha kuwa kwa sasa Majaji wamejielekeza kwenye utendaji wa haki na wanaendelea kutoa haki jinsi nafsi na sheria zinavyowatuma. “Hongereni sana Majaji, tunawashukuru sana. Naomba tuongeze kasi ili takwimu hizo zishuke lakini pia tujikite kuangalia ubora wa uamuzi unaotoka kwa kila kesi ama shauri,” alisema.

Dkt. Samia alieleza kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi suala la upungufu wa watumishi na maslahi na kuwahakikishia Majaji kuendelea kufanya kazi kwani maslahi yao yataendelea kuboreshwa.

Aidha, Rais Samia ameipongeza Mahakama kwa ujenzi wa miundombinu na kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi. “Nimefurahi kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa huduma za Mahakama Kuu katika Mikoa minane ya Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe, Simiyu na Lindi na mpango wa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneno mengine, ikiwemo Pemba,” alisema.

Kadhalika, amewapongeza watendaji wa Mahakama kwa kutumia vizuri fedha zilizotolewa kukamilisha miradi mbalimbali itakayoimarisha utendaji.

Rais Samia ameeleza kutambua uwepo wa fedha kutoka Benki ya Dunia ambazo zimeimarisha miundombinu ya Mahakama, ikiwemo Mahakama za Mwanzo 60 na majengo mengine 18 ambapo kati ya hayo, 11 ni Mahakama za Wilaya na saba ni Mahakama za Mwanzo.

“Hii ni ishara nyingine ya azma ya Mahakama ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi. Rai yangu kwa uongozi wa Mahakama ni kwamba miradi hiyo izingatie ubora unaoendana na fedha. Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama kwa kuwezesha miradi hiyo ili kuweka mazingira wezeshi ya kufanyia kazi na kusaidia wananchi kupunguza gharama katika kutafuta haki,” alisema.

Rais Samia ameelezea azma ya Serikali yake kuhakikisha taasisi zinazoshirikiana na Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zinapata pia miundombinu wezeshi. Amesema azma yake ni kuona shauri linalofunguliwa polisi linasomeka hivyo hivyo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na pia mahakamani ili kusiwe na hali ya kupindisha haki.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wa Rais Samia, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama, Wilbert Chuma pamoja na watumishi wengine.

Wageni wengine walikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro na Mawaziri wengine pamoja na Naibu Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Prof. Edward Hosea na wananchi kwa ujumla.

Rais Samia aliwasili katika Viwanja vya Chinangali majira ya saa 3:10 hivi asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake pamoja na viongozi wa Mahakama na Serikali. Baada ya kufika jukwaa kuu Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki ulipigwa kabla ya Mshereheshaji Mkuu, ambaye ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kuwakaribisha viongozi wa dini kuyaweka maadhimisho hayo mbele za Mungu.

Baada ya sala hizo, Rais wa TLS alikaribishwa kutoa salamu. Katika salamu zake, Prof. Hosea alisema kuwa chama chake kimeweka dhana ya suluhu kwa vitendo kwa kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro Tanzania.

“Tunaamini kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria Kituo hiki kitaiweka Tanzania katika ramani ya Afrika na Dunia kwa kutekeleza dhana ya kutatua migogoro ya kibiashara za kimataifa na ile inayohusu wawekezaji kwa njia ya suluhu. Hatua hii itaimarisha kwa vitendo na kukuza mazingira Rafiki kwa wawekezaji na wananchi wa Tanzania na kujenga imani katika mifumo ya utoaji haki na maendeleo,” alisema.

Katika salamu zake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kuanzishwa kwa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi kitafungua ukurasa mpya, hivyo kuwawezesha wadaawa na wanasheria kwenye migogoro kuweza kuishughulikia na kuimaliza pasipo kulazimika kwenda kwenye mabalaza ya nje katika mashauri hayo.

Dkt. Feleshi alibainisha kuwa wakati umefika wa kubadilisha Sheria ya Mwenendo wa Madai ili shauri la madai lipate sifa ya kusajiliwa mahakamani mara baada ya kupata uthibitisho kwamba zile ngazi za kupitia usuluhishi zimeshindikana.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Alimweleza Rais Samia kuwa ofisi yake na ile ya Wakili Mkuu wataendelea kusimia vyema kwa niaba ya Serikali matakwa ya sheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na wataendelea kusimamia kwa karibu maelekezo aliyoyatoa kuhusu jambo hilo ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi.

“Nitoe rai kwa Majaji na Mahakimu kuwa tayari kuwasilisha ofisini kwangu kwenye dawati linaloshughulikia utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali, kuhusu Wakili yoyote au mtendaji yoyote serikalini, ambaye kwa namna yoyote ile atathibitika kudhoofisha juhudi za Serikali na Mahakama za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi,” alisema.

Kabla ya Jaji Mkuu wa Tanzania kupanda jukwaani kuongea na Watanzania, Chuma alikaribisha kikundi cha Kwaya ya Mahakama, maarufu Ng’aring’ari ambacho kilikonga nyoyo za wananchi waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Chinangali. Mawaziri na Naibu Mawaziri na wananchi wengine walishindwa kujizuia, wakaamua kuachia viti vyao na kujimwaga uwanjani kufuatia burudani safi ya nyimbo iliyokuwa inatolewa na kwaya hiyo.

Wakati anazungumza na Taifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa yanarushwa mubashara na vituo mbalimbali vya runinga, Rais Samia aliwazawadia shilingi millioni moja Wanakwaya hao baada ya kukoshwa na uimbaji murua katika hafla hiyo.

Katika kukamilisha maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria yanayoashiria mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania alikagua gwaride maalumu lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kwa ajili ya shughuli hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here