Kifo cha Malkia wa kwanza na
mwisho wa Tanganyika huru

0

Na Syd. Chifu Mussa Bwakila Lukwele IV

ALIYEKUWA Mkuu wa kwanza wa nchi yetu upande (yaani Tanganyika), mara tu baada ya kupata uhuru, Malkia Elizabeth Alexandra Mary (Elizabeth II) amefariki Dunia Septemba 8, 2022 akiwa na umri wa miaka 96.

Malkia Elizabeth II amefariki akiwa Mkuu wa Taifa la Kifalme la Uingereza na nchi nyingine kadhaa zilizo hiyari awe kiongozi wao, pamoja na Jumuiya ya Madola.

Mwanawe wa kwanza Charles, mwanamfalme wa zamani Wales na Mrithi wa zamani wa Ufalme wa Tanganyika huru, sasa ndiye Mfalme Charles III na mkuu mpya wa Uingereza, pia wa nchi zilizokuwa chini ya Mama yake, aidha anakuwa kiongozi mpya wa Jumuiya ya Madola.

Ikumbukwe kuwa, Ufalme wa Tanganyika chini ya Mama huyu kama mkuu wa nchi huru uliundwa kisheria chini ya Sheria ya Uhuru (the Tanganyika Independence Act 1961), ambayo iliibadili nchi toka chini ya dhamana ya Umoja wa mataifa (trust territory), kuwa mamlaka huru ya ufalme wa kikatiba (independent sovereign constitutional monarchy).

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa Waziri Kiongozi kabla ya Uhuru, akawa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika ya Kifalme.

Sir. Richard Turnbull, akawa mwakilishi wa Malkia (Governor-General), aliyeteuliwa kikatiba na Malkia Elizabeth II kwa ushauri wa Waziri Mkuu Mwalimu Julius Nyerere.

Ifahamike kuwa, chini ya sheria ya Uhuru (Tanganyika Independence Act 1961), Uingereza haikuwa tena na mamlaka wala madaraka kwa Tanganyika, kwani nchi ilikuwa huru, na hakuna Waziri au afisa yeyote wa Taifa hilo aliyekuwa na mamlaka au madaraka ya kumshauri Mkuu wa nchi (Malkia Elizabeth II) juu ya masuala ya Tanganyika.

Kinyume chake ni baraza la mawaziri na maafisa wa serikali ya Tanganyika tu ndiyo wenye madaraka na mamlaka ya kisheria kumshauri mkuu wa nchi (Malkia Elizabet II) juu ya msuala ya Taifa lao huru.

Malkia Elizabeth II alikuwa mtawala wa Tanganyika iliyo chini ya dhamana ya umoja wa mataifa tangu mwaka 1952 hadi 1961.

Mama huyo wa watoto wanne, wajukuu wanane na vitukuu 12, aliongoza Ufalme wa Tanganyika mwaka 1961 hadi 1962, ambapo nchi ilibadili mfumo wa kisiasa na kuwa Jamuhuri.

Baada ya kuwa Jamuhuri sio tu kulimfanya Malkia Elizabeth II kundoka kwenye Uongozi, bali pia tawala zetu za Kichifu zikaondolewa kikatiba kwenye Uongozi wa nchi, hivyo kubaki kwenye jamii zao kama viongozi wa hiyari wa kitamaduni tangu wakati huo hadi sasa.

Familia ya Kifalme haikuwa na jinsi, pale Watanganyika walipoamua waachane na mfumo wa kisiasa wa kifalme (Monarchy) na kuwa Jamuhuri (Republic), ambapo Jarida la Jumuiya ya Madola la Masuala ya Kimataifa “The Round Table” liliandika:

“Tarehe 9 Disemba 1961, Tanganyika ilipopata uhuru, ikawa nchi ya kifalme huku mtawala (Monarchy) akiwa ni Malkia wa Tanganyika. Lakini ufalme wa Uingereza ulionekana kama taasisi ya kigeni ………………… Hata hivyo, inawekwa wazi kwamba pendekezo la kuwa jamhuri halimaanishi dharau yoyote kwa Malkia, ambaye nafasi yake kama Mkuu wa Jumuiya ya Madola inaendelea……. Chifu, kama kiongozi wa kabila, bado anashikilia nafasi ya umuhimu mkubwa katika maeneo mengi… kwa kiasi kikubwa Machifu wamedumisha mapenzi na uaminifu kwa watu wao chini ya mfumo wa kifalme. Inaweza kudhaniwa kuwa wazo la ufalme lilikubalika kwa watu, na kwamba katika baadhi ya maeneo lilikuwa limeimarishwa.

Hata hivyo, kuna tofauti kati ya wazo la kifalme la Uchifu na lile la mfalme mgeni ambaye ni Mzungu, na anayeishi maelfu ya maili na haonekani mara kwa mara. Siku zimepita ambapo mtawala wa Kiingereza anaweza kutarajiwa kuamuru uaminifu wa kibinafsi wa raia wa Kiafrika kwa njia sawa na watu wa asili ya Uingereza”. Rejea; “The Republic of Tanganyika: A Break with the Colonial Past”. The Round Table: The Commonwealth Journal of International Affairs. 52 (208): 339–347, 1962.

Malkia nae kwa kuheshimu maamuzi ya Watanganyika kuchagua mfumo wa kisiasa wanaoutaka, alimuandikia Mwalimu Nyerere barua akisema;

“Nakutakia salamu njema katika hafla ya kuasisiwa Jamhuri ya Tanganyika, na kushika madaraka yako kama Rais wa kwanza. Nimefuatilia maendeleo ya nchi kwa umakini mkubwa, na daima nitatazama juhudi na mafanikio ya Tanganyika katika miaka ijayo. Nimeridhika sana kuona kwamba nchi inasalia ndani ya Jumuiya ya Madola, na nina hakika urafiki na maelewano kati ya watu wetu utadumishwa na kuimarishwa”. Rejea; ‘African World’, African Publications, 1963, Ukurasa wa 15.

Tanganyika ikaungana na Zanzibar na kuwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, miezi michache tu baada ya kupinduliwa Ufalme wa Sayyid Sultan Jamshid Bin Abdallah Bin Khalifa Al-Said.

Ikumbukwe kuwa, Zanzibar ilipata uhuru tarehe 10 Disemba 1963 toka himaya ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza, hivyo Jamshid aliongoza Zanzibar kabla na baada ya uhuru (kuanzia tarehe 1 Julai 1963 hadi 12 Januari 1964 alipopinduliwa).

Sultan Jamshid alipewa hifadhi Uingereza kwa hisani ya Elizabeth II, baada ya Ufalme wa Oman kumkatalia chini ya Sayyid Sultan Taimurn na hata baadaye Sayyid Sultan Qabus kushikilia msimamo huo; aliishi Jijini Portsmouth kwa miaka 50, na hatimae ombi lake la kuishi Oman lilikubaliwa na Sultani wa sasa Sayyid Haitham bin Tariq, mwaka 2020, hivyo mwaka wa pili sasa anaishi jijini Muscat.

Malkia Elizabeth II aliwahi kuzuru Tanzania mwaka 1979 (Julai 19 hadi 22) akitembelea mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, na visiwani Zanzibar.

Tunamkumbukaje?

Mtawala huyo wa kifalme, ameweka rekodi ya kuiongoza Uingereza kwa muda mrefu zaidi (miaka 70), na kuwa mmoja wa watawala wachache duniani wa zama za karibuni kukaa mamlakani na madarakani kipindi kirefu.

Kwa watawala wa Kifalme wa zama za karibuni, ametanguliwa kutawala muda mrefu na Mfalme Sobhuza II, wa Swaziland sasa inaitwa Eswatini (kuanzia 22 Julai 1899 hadi 21 Agosti 1982), yaani amekaa madarakani na mamlakani kwa miaka 82 na siku 254.

Ningeweza kusema babu yangu mtawala wa Choma (Himaya ya kale ya Uluguru iliyogusa kijiografia sehemu fulani za wilaya ya Morogoro, Mvomero na Kilosa) Lukwele II Mdimang’ombe Mwana-Msumi Mwana-Kulinyangwa, ndiye aliyetawala muda mrefu zaidi kuliko wawili hao (1865 hadi 1971) yaani miaka 106 (amekufa akiwa na miaka 120 na alianza kutawala akiwa na miaka 14).

Lakini, kiuhalisia aliongoza “nchi huru” (himaya ya Waluguru ya Choma) yenye mamlaka na madaraka kamili kwa miaka 20 tu, kwani Wajerumani walitwaa ardhi yote ya Falme zaidi ya 50 za jadi ikijumuisha eneo lote la Tanzania bara ya sasa (ukiacha ukanda wa bahari uliokokuwa himaya ya Zanzibar), kisiwa cha Mafia, Rwanda na Burundi, baada ya mkutano wa Berlin wa Wazungu “kugawana” bara la Afrika kama kipande cha Papa.

Hivyo, Syd. Lukwele II hakuwa mtawala wa nchi huru tangu ukoloni unaingia hadi uhuru, ambapo jamii ilikubaliana kuwe na taifa moja kubwa na imara linaloitwa Tanganyika, badala ya kurejea kwenye falme ndogondogo za kabla ya ukoloni.

Sisi tunamkumbuka Malkia Elizabet II kwa yote, mema na yale yenye hitilafu. Historia ya Waluguru chini ya Waingereza inakumbuka madhila ya ukoloni hasa wa Mjerumani na Muingereza.

Mwingereza aliziweka chini ya utawala wake himaya 10 za jamii ya Waluguru rasmi kuanzia mwaka 1918, kufuatia Ujerumani kushindwa vita ya kwanza ya dunia. Uluguru kama ilivyokuwa wakati wa Wajerumani, ikajumuishwa kwenye eneo kubwa lililoitwa Tanganyika chini ya Mfalme George V, aliyetawala ardhi yetu hadi alipofariki Januari 20 mwaka 1936.

Uluguru kama sehemu ya Tanganyika ikawa chini ya Mamlaka ya Mfalme Edward VIII (Edward Albert Christian George Andrew Patrick David); kuanzia tarehe 20 Januari 1936 na kuachia madaraka mwaka huohuo tarehe 11 Disemba, kwa ajili ya kuoa mwanamke wa Kimarekani aliyetalikiwa Bibi Wallis Simpson (ambapo ni kinyume cha taratibu za Ufalme wa Kiingereza)!

Kama sehemu ya Tanganyika, Uluguru ikawa chini ya Mamlaka ya Mfalme George VI (Albert Frederick Arthur George) kuanzia tarehe 11 Disemba 1936 hadi alipofariki tarehe 6 Februari 1952, na nafasi hiyo kuchukuliwa na binti yake Malkia Elizabeth II hadi mwaka 1961 tulipopata uhuru (Japo Elizabeth II pia akawa kiongozi wa kwanza wa Tanganyika huru kuanzia 1961 hadi 1962).

Mara baada ya Uingereza kuchukua nchi kikamilifu mwaka 1918, Kiongozi wa Himaya ya Waluguru wa Choma Syd. Salum Lukwele II alilazimishwa kwenda kuishi uhamishoni kando ya mto Zambezi huko Caprivi nchini Namibia, kufuatia upinzani wake wa kijeshi dhidi ya Wakoloni hao wapya kushindwa vibaya na Ikulu/ Kasri zake mbili (Royal Palaces) kusambaratishwa na moja kutaifishwa.

Baada ya mkataba wa amani na Waingereza, alirejea nchini mwaka mmoja baadaye na kuwa chini ya Uangalizi wa Waingereza, akilazimishwa kuishi nje ya makao makuu ya himaya yake kwenye shamba lake, ambalo baadaye mwaka 1950 alijitolea lijengwe Soko kuu la Morogoro, lililofunguliwa mwaka 1953 na kujengwa upya wakati wa rais Dkt. John Magufuli hivi karibuni.

Kwa hivyo kwa Wanamorogoro, na kwa jamii ya Uluguru, Malkia Elizabeth II alikuwa alama ya Ukoloni na ukandamizaji dhidi yao kwa upande mmmoja, na kwa upande wa pili kuna mema yake pia.

Serikali yake ilishiriki kikamilifu katika mauaji ya watu kadhaa, wengine kujeruhiwa na wengine kutiwa mbaroni baada ya wakaazi wa Milima ya Uluguru kupinga uporaji wa ardhi, kwa kisingizio cha kuhamasisha kilimo cha matuta milimani ili kuhifadhi mazingira; Rejea: Young, R. and Fosbrooke, H. (1960), “Smoke in the Hills. Political Tension in the Morogoro District of Tanganyika”. North-Western University Press, Evanston.

Serikali ya Malkia Elizabeth II pia ilivuruga tawala za kijadi kwa kulazimisha mifumo yake ya kisiasa na kijamii kuwa juu ya Utamaduni wa wenyeji.

Aidha, ilisambaratisha uchumi wa wenyeji, mathalani wanajami walioishi kwenye milima ya Uluguru na tambalare yake, zao lao kuu la bishara la Kahawa lilisambaratishwa kimfumo!

Zaidi ya hayo, ifahamike vizuri kuwa, serikali ya Uingereza chini ya Malkia Elizabeth II, baba zake na babu yake haikuwahi kujenga barabara wala madaraja kwenye safu ya milima ya Uluguru, badala yake wenyeji wenyewe chini ya falme zao za jadi walifanya hivyo kwa kutumia rasilimali zilizowazunguuka (mawe, chokaa na udongo). Wenyeji pia walijenga miundombinu yao ya ulinzi, elimu, afya na maji.

Ikumbukwe pia kuwa, baada ya Ukoloni kuchukua nafasi ya serikali za kijadi, vijiji na miji nayo kupanuka kufuatia idadi ya watu kuongezeka kutegemea wakati, hitajio jipya la huduma za jamii hususan barabara za kisasa za zege hasa kwenye maeneo korofi hazikufanyiwa kazi na Wakoloni, na zilisubiri hadi wakati wa serikali ya Tanzania ndipo zilipoanza kujengwa kwenye maeneo machache.

Si kila mja ana kasoro peke yake, bali pia ana mema yake, hivyo Malkia Elizabeth II ingawa aliifanya Uluguru, Morogoro, na Tanganyika kwa ujumla kuwa “Shamba la Bibi”, ambapo maliasili zake zilivunwa kuijenga Uingereza na himaya yake kwenye maeneo mengine ya dunia, lakini zipo baadhi ya athari nzuri alizowacha.

Baadhi ya maeneo aliyaendeleza kimiundombinu, japo kwa lengo la kutaka kurahisisha kuzifikia maliasili zetu na kuzichukua kwa wepesi, lakini imetufaidisha baada ya uhuru.

Pili, japo Utawala wake uliendeleza elimu ngeni iliyoasisiwa na watangulizi wake wa Kijerumani, iliyodumaza na inayoendelea kudumaza akili za wanaoitwa “Wasomi” kuwa tegemezi kwa kila kitu cha Wakoloni wetu wa zamani (badala ya kuwa na fikra mbadala za kutumia rasilimali zilizotuzunguuka kuondoa unyonge na umasikini wa aina zote kwenye jamii); lakini kwa kiasi fulani sehemu ya elimu hiyo nayo ina athari chanya.

Kwa mfano elimu mpya ya sayansi na teknolojia kwenye masuala anuai, imesaidia kurahisisha kazi na maisha kwenye Nyanja karibu zote (kinachokwaza ni masalia ya fikra za kikoloni kuwa tegemezi zaidi wa karibu kila kitu na kila jambo).

Malkia Elizabeth II ametangulia mbele za haki, kwa nchi yake na kwa Dunia alikuwa na mchango hasi na chanya kama ilivyo kwa kila binaadamu.

Tunapotoa rambirambi zetu kwa Waingereza na mataifa mengine yaliyo chini ya Himaya yake, basi hatuna budi pia kuona umuhimu na udharula wa kurejea kwenye “Elimu Jadiiya”, kwa kutumia nyenzo na sehemu ya elimu ya kimamboleo yenye uchanya, kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo ya jamii.

Ukoloni ulishaondoka miaka mingi chini ya Elizabeth II, tutakuwa na akili finyu tukiendelea kuunyooshea kidole bila kuchukuwa hatua.

Athari hasi za ukoloni hazitaondoka hadi pale vichwa vyetu vitakapojitathmini na kuzinduka usingizini, kurejea historia na kurithishana mambo chanya, huku tukiachana na mambo hasi yanayoirejesha nyuma jamii kwenye maendeleo ya kila sekta.

*Mwandishi wa Makala hii Sayyid Mussa Bwakila Lukwele IV Mdimang’ombe Mwana Msumi Mwana Kulinyangwa, ni Chifu wa jamii ya Waluguru wa himaya ya Choma (ufalme wa kale uliokuwa kwenye eneo la kijiografia la ilipo sasa Manispaa ya Morogoro, sehemu ndogo ya wilaya ya Kilosa, sehemu ndogo ya Mvomero, na sehemu ndogo Morogoro vijijini tangu mwaka 1850). Kitaaluma ni mwanahabari, anapatikana kwa E.Mail: lukwelepalace@gmail.com au Simu namba +255 657 185468.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here