Mseto wa dini na siasa ni hatari, tuutenganishe

0

Na Ahmad Mmow

MAKANDE ya mseto wa dini na siasa yatatupalia, tutenganishe mapema. Naendelea kufuatilia siasa zetu kwa maslahi mapana ya Taifa letu pendwa la Tanzania.

Ni wajibu wangu wa msingi kufanya hivyo, kwani mimi sio miongoni mwa wanaofanya siasa (siyo mwanasiasa). Natambua kwamba siasa ni kila kitu.

Ni kutokana na urithi tuliopata kwa waasisi wa Taifa hili, ambao walituambia ili tuendelee tunatakiwa kuwa na watu, ardhi, uongozi bora na siasa safi.

Kwa hakika ardhi tunayo, watu tupo wakutosha (wengi), uongozi bora tunao pia. Ushahidi wa kuwepo uongozi bora ni amani na utulivu uliopo.

Kwa hakika, kusingekuwa na uongozi bora kusingekuwa na amani na utulivu. Kila kitu kingekwenda harijojo.

Kuhusu siasa safi nayo ipo. Hata hivyo, zipo dalili ya siasa kuanza kuchafuka na kubadilika kuwa siasa chafu. Bado hatujafika hatua hiyo ya siasa yetu kuwa chafu. Bali zipo dalili kuwa na siasa chafu iwapo hazitachukuliwa hatua thabiti na madhubuti za mapema ili tusifike huko.

Binafsi naona siasa yetu inaweza kuchafuka kutokana na mseto wa siasa na dini. Ingawa mseto huu sio rasmi, lakini inaonesha una nguvu. Japo kumekuwa na nadharia ya kutenganisha siasa na dini.

Hata hivyo, ni nadharia tu. Lakini vitendo vinaonesha siasa na dini bado havijatenganishwa kikamilifu. Serikali tulizo nazo ni zao la siasa. Watumishi wa umma (watumishi wa Serikali) wanatekeleza maamuzi ya wanasiasa ambao bila shaka ndiyo wanaofanya siasa.

Wote tunajua kwamba, wabunge ni wanasiasa. Wabunge hao pamoja na mambo mengine, wajibu wao ni kutunga sheria. Sheria ambazo zinazalisha kanuni, miongozo, taratibu, sera nk.

Bado naamini, siasa na dini vimechangamana sana. Kwani wanaofanya dini (viongozi wa dini) na viongozi wa kisiasa (wanasiasa) wananisukuma niamini kuna mseto wa siasa na dini, ingawa tunaambiwa siasa na dini havitakiwi kufanywa pamoja, lakini bado vitu hivyo havijatenganishwa kikamilifu na kwa kiasi kikubwa vinategemeana.

Si mara moja wala mbili, viongozi wa kisiasa na viongozi wa umma ambao ni zao la siasa, wanawaomba viongozi wa dini kusaidia mambo kadhaa; ikiwamo kuhusu maadili na kuombea amani.

Kwa upande mwingine tumeshuhudia viongozi wa dini wakiwaalika wanasiasa kwenye shughuli zao za kidini. Mara kadhaa tumesikia viongozi wa kisiasa na hata Serikali wakiwa wageni rasmi kwenye shughuli za kidini. Bila shaka wanakwenda na nyadhifa zao, ambapo wakiwa katika shughuli hizo wanafanya siasa.

Uswahiba huu sasa umekuwa mkubwa. Kiasi cha viongozi wa dini kufanya kazi ya siasa katika maeneo yao ya kuabudia (Majumba ya ibada). Ni kwasababu ya kujiamini kupita kiasi kuliko sababishwa na uswahiba huu.

Kwa kuwa viongozi wa kisiasa wanapoalikwa kwenda kwenye shughuli za dini katika maeneo ya kufanyia ibada na kufanya siasa, basi viongozi wa dini nao wanaona hakuna ubaya wa kufanya siasa kwenye maeneo hayo ya ibada.

Uswahiba huo umeanza kuwa wa mashaka na kumeanza kusikika lawama kutoka upande mmoja dhidi ya upande mwingine. Kwamba, baadhi ya viongozi wa dini wanachanganya dini na siasa.

Kwamba, badala ya kuhubiri mambo ya kiroho wanahubiri siasa kwenye majumba ya ibada. Ingawa mialiko ya viongozi wa dini kwenda kwa viongozi wa siasa na Serikali wanashiriki kama wanasiasa na viongozi wa Serikali.

Ndipo najiuliza inawezekanaje mwanasiasa anakubali kualikwa kwenye shughuli za dini kama kiongozi wa kisiasa! Na vipi kiongozi wa dini akizungumzia siasa anakuwa amechanganya siasa na dini? Kwani kiongozi wa dini kutoa mwaliko kwa mwanasiasa au kiongozi wa Serikali sio kuchanganya siasa na dini?

Kwa hakika, huu ni mkorogo wa hali ya juu. Kwani haileweki ni muda gani wa kiongozi wa dini kufanya siasa ni halali na muda gani kufanya siasa ni haramu?

Halikadhalika, wanasiasa na viongozi wa Serikali wamekuwa wakiwaalika viongozi wa dini katika shughuli na hafla za kiserikali, ambapo viongozi hao wa dini wanapokwenda kwenye shughuli hizo wanazungumzia imani zao. Kwahiyo, wanachanganya siasa na dini kwenye shughuli za kiserikali ambayo haina dini.

Binafsi, nadhani kuna kosa limefanyika pande zote kwa maswahiba hawa. Mipaka ya utendaji kazi yao ipo wazi kabisa. Kwamba, viongozi wa kidini ni kuwaongoza waumini wao katika mambo ya kiroho. Wana katiba na miongozo yao ya kale kabisa. Yaani Quraan na biblia.

Viongozi wa kisiasa na Serikali wana Katiba ya nchi ambayo hata viongozi wa dini wanatakiwa kutii. Lakini, licha ya uwazi huo wa mpaka wa asili. Viongozi wa dini na wanasiasa wameamua kupita njia tofauti.

Kwa hakika, njia wanayopita imeanza kuleta shida. Njia ya kuchanganya siasa na dini na dini na siasa. Ni sawa na makande ya mseto wa dini na siasa. Mseto huu haukubaliani na hautoi chakula kitamu tunachotaraji. Kwani kimekuwa kigumu, kichungu, hakiliki na hakimezeki.

Ushauri wangu, turudi haraka kwenye mipaka halisi. Kwamba, viongozi wa dini wafanye kazi za dini tu kwa mujibu wa katiba zao ili wasichanganye dini na siasa. Pia, viongozi wa kisiasa na hata Serikali wasikubali kualikwa na viongozi wa dini kwenye shughuli zao kidini.

Hali kadhalika viongozi wa dini wasiwaalike wanasiasa. Kwani watakuwa wanachanganya dini na siasa. Hali kadhalika viongozi wa dini na Serikali wasiwape mialiko viongozi wa dini kwenye shughuli za kiserikali.

Viongozi wa kisiasa na Serikali wasimamie wajibu wao wa msingi uliopo ndani ya katiba. Ikiwa ni pamoja kusajili madhehebu ya dini na kufuatilia yanayofanywa na madhehebu hayo ili kuhakikisha kama hayakengeuki sheria za nchi.

Kiongozi wa kisiasa aende kwenye shughuli za kidini husika iwapo yeye ni mfuasi wa dini hiyo, asiende kutokana na wadhifa wake. Hali kadhalika kiongozi wa dini aende kwenye shughuli za Serikali kama mwanamchi au raia wa kawaida. Sio kwasababu ya kuwa ni kiongozi wa dini.

Haitakuwa jambo baya Serikali kutowaalika viongozi wa dini kwenye shughuli zake. Kwani nchi yetu haina dini, bali watu wake wana dini zao. Kwahiyo, hakuna haja ya maombi wala dua za viongozi wa dini.

Wala haitakuwa vibaya kwa viongozi wa dini kuto waalika viongozi wa Serikali na kisiasa. Kwani Serikali haina dini. Bila shaka kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetenganisha siasa na dini kikamilifu. Vinginevyo haya makande ya mseto wa dini na siasa yatatupalia. Tutenganishe haraka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here