Na Subira Ally
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), kuangalia pengo la Kisera katika mfumo wa ukusanyaji mapato nchini na kuufanyia mageuzi sahihi ili kuongeza ufanisi na kukuza kiwango cha mapato Zanzibar.
Othman alisema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, alipozungumza na Kamshina wa ZRB Ramadhani Juma Mwenda aliyefika ofisini kwa Makamu kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala mbali mbali yanaoweza kuchangia ufanisi na kukuza kiwango cha mapato yanayokusanywa Zanzibar.
Makamu amefahamisha kwamba, yapo maeneo mengi ya Mapato ambayo yanaweza kufanyiwa mageuzi zaidi ya  kisera na kisheria jambo litakalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa kupitia vyanzo tofauti vilivyopo nchini.
Aidha, Othman amesema hatua ya hiyo pia itasaidia sana kuwepo vyanzo zaidi vya mapato yatakayoweza kuchangia kasi zaidi ya maendeleo ya nchi kutokana na kiwango kikubwa zaidi cha mapato kuweza kukusanywa.
Othman alisema, yapo maeneo mengi ambayo baada ya mageuzi ya kisera na kisheria kufanyika yataweza kutumika kukusanyia mapato zaidi na nchi ikaweza kuendelea kwa kasi kubwa  kwa kiwangpo cha mapato yatakayopatikana kuliko ilivyo sasa.
Pia, Othman alisema kuna haja ya kuchambua zaidi viwango vya malipo vinavyokana na ushuru wa ‘stamp’ hasa katika kutafautisha mapato ya aina hiyo kupitia miradi mikubwa na inayoanzishwa nchini ile ya kawaida, ambapo viwango vyake vinaweza kuwa tofuato kuliko ilivyo sasa.
Aidha, alisema kwamba kuna fursa nyingi za mikopo ya kifedha katika mabenki mbali mbali nchini zinazoweza kutumika kibiashara lakini zimekuwa zikitumika zaidi kwa bikopo ya watu binafsi  kuliko mashirika ambayo yanaweza kuwa  na kiwango cha tija zaidi katika kasi ya ukusanyaji mapato nchini.
Amefahamisha kwamba, pia eneo la utayarishaji wa mikataba ya kibisashara kupitia watu binafsi, mashirika na taasisi nalo ni muhimu kuangaliwa kwani linaweza kusaidia kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato na kuchangia kasi zaidi ya kukuza uchumi wa Zanzibar. Â
Othman alishauri, katika jitihada za kuongeza kiwango cha mapato bodi hiyo kuangalia uwezekano katika utaratibu wa Benki za Kiisalamu kwa kuwa bado kunachangamoto kwenye eneo hiilo na itakapotatuliwa itachangia kiwango cha mapato kuongezeka nchini.
Naye, Kamishna wa Bodi hiyo Ramadhani Juma Mwenda, ameeleza kwamba, ZRB inaendelea kufanya mageuzi katika mifumo yake ya ndani  ya ukusanyaji mapato jambo linalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa Zanzibar kupitia bodi hiyo.
Alisema, kutokana na hali hiyo wamefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu kimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 131 hadi 135 kwa kipindi cha miezi mitatu.
Mwenda alisema, jitihada kubwa imefanywa katika kudhibiti udanganyifu na uvujaji wa mapato sambamba na kutengeneza mazingira bora ya ulipatiji kodi za aina mbali mbali jambo linalochangia kuongeza ufanisi na mafanikio zaidi ya kukusanya kodi.