📌ATAKA FEDHA ZA BARABARA ZITUMIKE KWA KAZI HIYO TU
📌KUANZA KUPIMA MAMENEJA KWA UBORA WA VIWANGO VYA BARABARA
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa maelekezo kwa mameneja wa TANROADS kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zinatumika kwa kazi hiyo pekee na si vinginevyo.
Pia, waziri huyo ametaka kusiwe na ucheleweshaji wa utekelezaji wa kazi hizo kwa kisingizio cha taratibu za kiutendaji, ili wananchi waendelee kupata huduma bora za miundombinu kwa wakati.
Ulega ametoa maelekezo hayo wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara, ambapo amekagua ujenzi wa barabara ya Karatu- Mbulu – Hydom – Sibiti – Meatu – Lalago – Maswa (km 389) sehemu ya Mbulu – Garbabi na Labay – Hydom kwa kiwango cha lami pamoja na barabara ya zege ya Mbuyu wa Mjerumani – Mlima Magara hadi Mbulu.
“Fedha zinakuja kwa ajili ya barabara za wananchi. Sitaki kusikia fedha zimefika mkoani halafu naambiwa mchakato unaanza au unaendelea wakati barabara ziko katika hali mbaya. Sitavumilia hali hiyo,” amesema Ulega.
Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora na kwa wakati pamoja na kusimika taa za barabarani katika barabara za Mbulu ili kuchochea maendeleo ya wananchi.
Aidha, Waziri Ulega amesema kuwa viongozi na watendaji watakaoshindwa kusimamia matumizi ya fedha za barabara kwa wakati na kwa ufanisi wataondolewa katika nafasi zao.
Ulega amesema barabara hiyo ni muhimu na ni ya kimkakati kwani sehemu ya mtandao muhimu wa usafiri unaounganisha mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga na Simiyu, hivyo inapaswa kukamilishwa kwa wakati.
“Nimekagua mradi kutoka Mbulu kuelekea Garbabi kupitia Tlawi na kujionea maendeleo yake. Niwahakikishie Serikali itaendelea kuujazia fedha mradi huu ili mkandarasi akamilishe kazi kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema Ulega.
Katika hatua nyingine, Ulega ameiagiza TANROADS, wasimamizi wa miradi na wakandarasi wote nchini kuhakikisha ujenzi wa barabara unazingatia viwango vya ubora ili fedha za umma zitoe thamani inayostahili na miundombinu idumu kwa muda mrefu.