RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihimiza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, usalama wa mifumo ya kifedha, ubunifu wa bidhaa na huduma, pamoja na matumizi ya Akili Mnemba (AI), ili kuongeza ufanisi na ushindani katika utoaji wa huduma.
Akizungumza leo, tarehe 30 Juni 2026, katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya PBZ yaliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar Airport, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza benki hiyo kwa mafanikio katika huduma za kidijitali na kuitaka iongeze juhudi ili iwe miongoni mwa benki bora nchini.
Aidha, ameihimiza PBZ kuimarisha mtaji wake, kuendelea kubuni bidhaa na huduma za kifedha, kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi, kuwekeza katika rasilimali watu, kuimarisha utawala bora na usimamizi wa vihatarishi, pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema gawio la Shilingi Bilioni 15.3 lililotolewa na PBZ kwa Serikali linaonesha uimara wa benki hiyo na mchango wake katika maendeleo ya taifa, huku akieleza matarajio yake ya kuiona PBZ ikiwa “Benki ya Watu na Chaguo la Watu”, yenye ubora, ubunifu na mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.