Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimetaja msingi wa Tamasha la Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja , umebeba maudhui ya kuhifadhi na kuendeleza Utamaduni, Mila na Desturi za watu wa Zanzibar .
Aidha, Tamasha hilo hukusudia kuanzisha , kuendeleza na kuibua miradi ya kiuchumi na kimaendeleo katika jamii.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto khamis, alipozungumza na Waandishi wa habari waliofika ofisini kwake Kisiwandui.
Mbeto alisema, Tamasha hilo halina sura ya Kisiasa bali limejielekeza kuonesha ustaarabu, Mila, Utamadumi, silka akhlaq, michezo na shughuli za watu Mkoa Kusini Unguja.
Alisema, kila jamii hutofautiana kwa tabia zao, kazi za Uzalishajimali, Kiuchumi na kijamii ,zikiwemo ngoma, unyago, jando, harusi na mikusanyiko ya Jadi na Asili za watu wake.
“Kuna mikusanyiko isiopishana sana kwa Mila , Utamaduni, ustaarabu, ngoma za Asili, lahaja na matamshi ya Lugha ya Kiswahili baina ya Mkoa hadi Kisiwa kimoja na kingine,” alisema Mbeto.
Aidha, alisema ndani kiini cha Tamasha hilo, Tamasha huonesha aina ya mapishi ya Mkoa wa Kusini Unguja, shughuli jumuishi za Uzalishajimali, Sanaa, Ufundi stadi, kazi za mikono na maeneo ya Kihistoria.
“Kuna hadithi na simulizi za kihistoria kwa wenyeji na wageni wahamiaji wa Kale waliofika na kuishi Kizimkazi. Hadithi hizo hutofautiana na zile zilizoko kisiwa cha Unguja, Tumbatu na Pemba,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi alisema, hata mapokeo ya harakati za Kisiasa pia kuna mitazamo na ushiriki wake, kwakuwa Siasa haitenganishwi na maisha ya jamii, juhudi na harakati za kujikomboa kwao.
“Tamasha la Kizimkazi la kila mwaka huwaunganisha wana jamii na kuwaweka pamoja. Mikusanyiko hiyo huhimiza Umoja ,Ushirikiano, Upendo na Udugu,” alisistiza.
“Hatua ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupita mitaani ndani ya Hifadhi ya Mji Mkongwe, akisalimiana na wenyeji na watalii ni katika kuhimiza Umoja na upendo. Dunia ya leo inahitaji maelewano si migawanyiko,” alieleza Mwenezi huyo.