WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na viwanda kwa kufanya mageuzi ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya utoaji huduma ili kuiwezesha sekta binafsi kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema hayo leo, Jumanne Juni 30, 2026, alipokuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mwaka 2026 lililoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kuhama kutoka katika mfumo wa kudhibiti biashara kwenda katika mfumo wa kuwezesha biashara kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kupunguza urasimu, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa taasisi zinazotoa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Ajenda ya sekta binafsi ni ajenda ya Taifa. Hatuwezi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila sekta binafsi yenye nguvu, inayowezeshwa na inayoshirikiana kwa karibu na Serikali,” amesema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi mapendekezo ya sekta binafsi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Waziri Mkuu amesema amani, utulivu na mshikamano wa Taifa ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuendelea kuvilinda ili kuwezesha biashara, uwekezaji na uzalishaji kustawi.
Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga alisema Serikali inaendelea kujenga mazingira rafiki ya biashara kwa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa mtazamo wa kuwezesha biashara badala ya kuzikwamisha.
Kwa upande wake, Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Bw. Vincent Minja alisema chemba hiyo imeendelea kufanya mageuzi ya kiutawala na kidijitali yanayolenga kuboresha huduma kwa wanachama, kuimarisha uwakilishi wa sekta binafsi na kuongeza ushindani wa biashara za Tanzania.
Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu alizindua rasmi Mfumo wa Kidijitali wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania, utakaorahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za chemba hiyo, ikiwemo usajili wa wanachama, utoaji wa vyeti vya asili ya bidhaa na huduma nyingine za biashara kwa njia ya mtandao.
Aidha, alishuhudia utiaji saini wa hati mbalimbali za makubaliano ya ushirikiano kati ya Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania na taasisi za umma pamoja na sekta binafsi, hatua inayolenga kuimarisha biashara, uwekezaji, utafiti, ubunifu na maendeleo ya sekta binafsi nchini.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi za umma, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, mabalozi, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.