Na Hamis Shimye
TANGU alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mwezi Desemba 2024, James Kaji ameonekana kuleta mwelekeo mpya wa kiuongozi ulioambatana na mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za utambulisho wa Taifa.
Ndani ya kipindi kifupi, NIDA imeanza kujijengea taswira mpya mbele ya wananchi kwa kuboresha huduma na kupunguza changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.
Kwa miaka kadhaa, NIDA ilikumbwa na malalamiko ya ucheleweshaji wa huduma, urasimu na msongamano wa wananchi waliokuwa wakihitaji Vitambulisho vya Taifa.
Hali hiyo ilifanya mamlaka hiyo ionekane kama taasisi yenye changamoto nyingi za kiutendaji. Hata hivyo, hali hiyo inaanza kubadilika kutokana na maboresho yaliyoletwa chini ya uongozi wa Kaji.
Mabadiliko haya yanaakisi dhamira ya uongozi wa NIDA ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma sambamba na kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga taasisi za umma zinazowajibika, zenye ufanisi na zinazotumia teknolojia katika kuwahudumia wananchi.
Katika kipindi hicho, NIDA imeongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa Vitambulisho vya Taifa huku ikiboresha mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali. Hatua hizo zimechangia kupunguza muda wa kusubiri huduma na kuongeza urahisi kwa wananchi kupata haki yao ya msingi ya utambulisho.
Moja ya mafanikio yanayoonekana wazi ni kuongezeka kwa idadi ya wananchi waliopatiwa Vitambulisho vya Taifa, ambapo zaidi ya Watanzania milioni 20 wamekwisha kupata vitambulisho hivyo.
Mafanikio haya yanatokana na uwekezaji wa Serikali katika kuongeza uwezo wa uzalishaji wa vitambulisho pamoja na usimamizi madhubuti wa zoezi la usambazaji.
Aidha, maboresho ya huduma za kidijitali yameongeza ufanisi katika utoaji wa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), kurahisisha maombi ya huduma mbalimbali na kuwezesha taasisi za umma na binafsi kuthibitisha taarifa za wananchi kwa njia ya kielektroniki. Mfumo huo umeongeza kasi ya utoaji wa huduma na kuimarisha matumizi ya utambulisho wa taifa katika sekta mbalimbali za uchumi na kijamii.
Uongozi wa Kaji pia umeweka mkazo katika kusafisha taarifa za utambulisho kwa kubaini na kurekebisha taarifa zisizo sahihi, pamoja na kuharakisha ugawaji wa vitambulisho ambavyo vilikuwa havijachukuliwa kwa muda mrefu.
Hatua hizo zimeongeza uaminifu wa mfumo wa utambulisho wa taifa na kuimarisha ubora wa huduma zinazotegemea taarifa za NIDA.
Katika eneo la mapato, NIDA imeendelea kuonyesha mafanikio yanayoakisi ufanisi wa taasisi hiyo. Kuongezeka kwa gawio kutoka Shilingi bilioni 38 mwaka jana hadi Shilingi bilioni 61 kwa mwaka huu ni ishara ya kuimarika kwa utendaji na usimamizi wa rasilimali za mamlaka hiyo. Mafanikio hayo yameifanya NIDA kuwa miongoni mwa taasisi za umma zinazochangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Serikali.
Bila shaka, maboresho ya huduma za kidijitali, ongezeko la matumizi ya huduma za uthibitishaji wa taarifa na upanuzi wa matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa yataendelea kuimarisha mapato ya taasisi hiyo huku yakiongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ni wazi kuwa bado kuna kazi ya kufanya ili kuhakikisha kila Mtanzania anayestahili anapata huduma kwa wakati. Hata hivyo, hatua zilizopigwa ndani ya kipindi kifupi zinaonyesha kuwa NIDA ipo katika mwelekeo sahihi.
Mageuzi haya yanastahili kuungwa mkono na wadau wote ili kujenga mfumo imara wa utambulisho wa taifa wenye kuaminika na unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi.
Kwa msingi huo, pongezi kubwa anastahili ‘Jenerali’ James Kaji na timu yake kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya katika kuibadilisha NIDA.
Kasi kubwa iliopo sasa ndani ya mamlaka ni mwanzo wa mfano bora kwa taasisi ya umma inayoweka mbele huduma bora, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia kwa manufaa ya wananchi.