Na WMA – DODOMA
WAKALA wa Vipimo (WMA) umemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Selemani Mwenda kuwa utaongeza kasi ya utendaji kazi wa masuala ya vipimo katika wilaya hiyo ili kulinda uchumi wa wakulima na wafugaji.
Hakikisho hilo limetolewa jana Agosti 8, 2026 alipotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Dodoma, na kupatiwa elimu ya vipimo.
Meneja wa WMA Mkoa wa Singida, Willie Amosi alisema kuwa “WMA itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuratibu na kutoa elimu ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya Iramba kwa lengo la kufikia wakulima wa mahindi, alizeti na pamba pamoja na wafugaji kwenye minada na masoko.
Aidha, alimjulisha Mkuu wa Wilaya kuwa WMA itajipanga ili kuanzisha Klabu za Vipimo (Vipimo Clubs) katika shule mbalimbali za msingi na sekondari ikiwa ni mikakati ya kufika Tanzania nzima, hususan Tanzania Bara ambao ndiyo uwanda wa WMA.
Vilevile, Meneja Amosi alisema, WMA itaendelea kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili wananchi wa Iramba waweze kuripoti moja kwa moja matumizi ya vipimo visivyo rasmi vinavyotumika katika masoko na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa uharaka
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya alisema:
“Nimefurahishwa sana. Kama Serikali ya Wilaya tuko tayari kushirikiana na WMA ili kuhakikisha vipimo sahihi vinatumika na wananchi waweze kupata stahiki ya jitihada zao. Ningetamani Iramba iwe miongoni mwa Wilaya zinazotumia vipimo sahihi katika sekta za kilimo.uvuvi pamoja na ufugaji.”
Wataalamu wa WMA walimkabidhi pia vipeperushi vyenye elimu ya vipimo ili vimsaidie kuendelea kujenga uelewa wa elimu ya vipimo.