Na WAF -Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa kushirikiana na shirika la afya Duniani chini mradi wa pandemic fund imeendelea kuimarisha uwezo wa nchi katika kugundua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa kuwajengea wataalamu wa maabara ujuzi wa matumizi ya teknolojia ya kisasa ya Pathogen Genomic Sequencing, inayowezesha kubaini kwa usahihi vimelea vya magonjwa, kufuatilia mabadiliko yake na kusaidia maamuzi ya haraka katika afya ya umma.
Akifunga rasmi mafunzo hayo Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Mwafulango, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa pamoja na maendeleo ya rasilimali watu ili kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa na kuongeza utayari wa taifa kukabiliana na milipuko.
Amesema mafunzo hayo yameongeza uwezo wa wataalamu wa maabara kutumia mbinu za kisasa za uchunguzi wa vinasaba, hatua itakayosaidia kubaini milipuko katika hatua za awali, kufuatilia chanzo chake na kuwezesha utekelezaji wa hatua stahiki za kudhibiti maambukizi.
“Mafunzo haya yamekuwa chachu kubwa katika kuongeza uelewa na ujuzi kwa wataalamu wetu wa maabara. Tunataka kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kubaini milipuko mapema, kufuatilia chanzo chake na kuchukua hatua za haraka za udhibiti,” amesema Mwafulango.
Aidha, Mwafulango amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya sekta ya afya ya binadamu, afya ya wanyama na taasisi nyingine za kitaalamu katika kutekeleza dhana ya One Health, inayotambua uhusiano wa karibu kati ya afya ya binadamu, afya ya wanyama na mazingira katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake, mtaalamu wa maabara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Huduma za Maabara, Ritha Yodos, amesema ushirikiano wa sekta mbalimbali ni nguzo muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, kwani magonjwa mengi yanayoibuka yanahusisha uhusiano kati ya binadamu, wanyama na mazingira.
“Jitihada hizo zinaendelea kuakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kugundua, kufuatilia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, ushirikiano wa sekta mbalimbali na uwekezaji endelevu katika wataalamu wa afya, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa afya nchini na duniani,” ameongeza Ritha.