π Asisitiza Kuthaminiana, Umoja na Mshikamano wa Watanzania
Mbogwe
NAIBU Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, amewataka Watanzania kuendelea kuuenzi na kuudumisha utamaduni wa amani, upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumza wakati wa ibada na mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ilolangulu, Kabula Ndabacha, yaliyofanyika wilayani Mbogwe, Dkt. Biteko alisema nyakati za mafanikio na changamoto zinahitaji wananchi kuendelea kuthaminiana, kusaidiana na kuishi kwa upendo bila kujali tofauti zao.
βAmani ni urithi wetu mkubwa na ndiyo msingi wa maendeleo tunayoyashuhudia leo. Tuilinde kwa kuendelea kuishi kwa upendo, umoja na kuheshimiana, kwani maendeleo ya Taifa letu yanategemea mshikamano wa wananchi wake,β alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akieleza kuwa kifo cha Mhe. Kabula Ndabacha ni pigo kwa familia, wananchi wa Kata ya Ilolangulu na Chama Cha Mapinduzi kutokana na mchango wake katika kuwatumikia wananchi.
Dkt. Biteko aliwahimiza wananchi kuendeleza mema yaliyoachwa na marehemu kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuendelea kuilinda amani ambayo imeendelea kuwa tunu na fahari ya Tanzania.