MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba amesema wameandaa mpango mpya ambao umejikita katika kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika maeneo ya uchumi shindani, maendeleo ya watu na uendelevu wa mazingira.
Mshomba ameyasema hayo leo Septemba 21, 2026 katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, uwekezaji wa NSSF utalenga maeneo salama yenye faida kwa wanachama na Taifa, huku miradi mbalimbali ikiendelea kuchangia katika uzalishaji wa ajira na kukuza uchumi.
Mkurugenzi huyo amesema, NSSF imejiwekea lengo la kuzalisha zaidi ya ajira 13,729 katika kipindi cha mpango mpya kupitia shughuli na uwekezaji mbalimbali.
Katika eneo la mazingira, Mshomba amesema, NSSF imeanza kuzingatia masuala ya ESG-Environmental, Social and Governance, katika shughuli zake.
Amesema, taasisi hiyo inalenga kufanya uwekezaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira, huku majengo mapya yakielekezwa katika dhana za majengo rafiki kwa mazingira.
Pia, Mshomba amesema shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zitaendelea kuzingatia ulinzi wa mazingira na mahitaji ya jamii.
Wakati huo huo, Mshomba amesisitiza kuwa, msingi wa hifadhi ya jamii ni kuhakikisha mwananchi anakuwa na ulinzi wa kipato baada ya uwezo wake wa kufanya kazi kupungua kutokana na uzee, ulemavu au sababu nyingine zinazotambuliwa kisheria.
Amesema, tangu kuanzishwa kwake, NSSF imepitia mabadiliko mbalimbali ya kisheria na kiutendaji, kutoka mfumo uliokuwa ukijikita zaidi katika malipo ya mkupuo hadi kuimarisha dhana ya pensheni na uendelevu wa kipato.
Mshomba amesema, hatua za sasa za kupanua uanachama, kuboresha mafao, kutumia teknolojia na kuongeza uwekezaji zinalenga kuifanya hifadhi ya jamii iwafikie Watanzania wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri aliyemwakilisha Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema, taasisi na Mashirika ya umma yana nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050.
Kosuri amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza tena awamu ya mikutano kati ya taasisi na mashirika ya umma na wahariri wa vyombo vya habari baada ya mapumziko yaliyotokana na maandalizi ya Serikali baada ya uchaguzi.
Amesema, kuanza kwa awamu hii katika kipindi ambacho nchi inaanza kutekeleza Dira 2050 ni fursa muhimu ya kujadili namna taasisi za umma zilivyojipanga kutekeleza malengo ya kitaifa.
Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema, taasisi na mashirika ya umma yana mchango mkubwa kupitia uwekezaji, ufanisi katika utoaji wa huduma na mchango wake katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.
Kosuri amesema, zaidi ya taasisi 40 tayari zimethibitisha kushiriki katika awamu ya kwanza ya mikutano hiyo.
Amesema, lengo ni kujenga uhusiano mzuri kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari, lakini pia kuonesha kwa umma namna taasisi hizo zilivyojiandaa kutekeleza Dira 2050.